GST yarusha ndege nyuki hii angani kutafiti jiolojia ya miamba,Jionee Hapa

Yaanza kutekeleza Vision 2030 kwa vitendo

Jaribio la Utafiti wa High Resolution Airborne Survey waanza Dodoma

Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imeanza majaribio ya Utafiti wa Jiosayansi kwa kutumia njia ya High Resolution Airborne Geophysical Survey kwa kurusha Ndege Nyuki (Drone) kwa kushirikiana na Kampuni ya Ellygreentech katika Kijiji cha Mzogole kilichopo Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma.

Katika kutekeleza kwa vitendo dhana ya Vision 2030 "Madini ni Maisha na Utajiri",  GST imeanza kufanya majaribio ya kurusha Ndege Nyuki kwa ajili ya tafiti za rasilimali zilizopo chini ya ardhi ikiwemo Madini na Maji ili kubaini taarifa sahihi za rasilimali hizo.

Akizungumza hivi karibuni kuhusu dhana ya Vision 2030 Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde alisema uwepo wa  taarifa sahihi za kijiolojia ya miamba ndiyo imebeba dhana ya utajiri wa Tanzania ambapo alisisitiza GST kushirikiana na taasisi nyingine ili kutengenezea kanzidata ya taarifa sahihi za kijiolojia.

Akizungumza katika eneo la Utafiti Kaimu Mkurugenzi wa Kanzidata ya Taifa ya Rasilimali Madini Hafsa Maulid amesema GST imejipanga kikamilifu kutekeleza kwa vitendo dhana ya Vision 2030  kwa kufanya tafiti za kina kwa njia ya Jiofizikia angalau asilimia 50 ifikapo 2030 ambapo kwa sasa ni asilimia 16 pekee ambayo imefanyiwa utafiti huo.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ellygreentech Elbariki Nsenuka amesema Kampuni anayoiongoza inatumia teknolojia ya kisasa ya kutafiti madini kwa kurusha Ndege Nyuki ambapo Kampuni hiyo ni ya kitanzania na ina wataalamu wenye uzoefu mkubwa katika tasnia hiyo.

Nsenuka amesema faida za kutumia Ndege Nyuki ni pamoja na kuokoa muda pamoja na kupata taarifa sahihi na zenye uhakika na pia, ametoa wito kwa wadau wa Sekta ya Madini na Taasisi zinazohusika na tafiti   za miamba na udongo kutumia teknolojia hiyo.

Uwepo wa taarifa sahihi za Jiolojia utasaidia wachimbaji wadogo kuachana na uchimbaji wa kubahatisha na pia, kuwawezesha wawekezaji kuweza kupata taarifa zenye uhakika za Jiosayansi zinazofanywa na GST ili kuwawezesha kuchimba kwa tija na kuliletea taifa maendeleo kupitia Sekta ya Madini.

VISION 2030 MADINI NI MAISHA NA UTAJIRI



 

Previous Post Next Post

نموذج الاتصال