Ticker

10/recent/ticker-posts

TARURA MBINGA YALALAMIKIWA NA WANANCHI KWA UBOVU WA BARA BARA

MVUA  zinazoendelea kunyesha kwa wingi katika wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma,zimesababisha kuharibika kwa miundombinu ya barabara katika mtaa wa Kipika kata ya Matarawe wilayani humo na hivyo kutishia kukata mawasiliano kati ya mtaa huo na maeneo mengine ya mji wa Mbinga.

Kutokana na uharibifu uliotokea,baadhi ya wakazi wa mji wa Mbinga wameiomba Serikali kuwachukulia  hatua ikiwemo kuwafikisha mahakamani  makandarasi na wahandisi wa wakala wa barabara vijijini na mijini Tanzania (TARURA) kwa kushindwa kusimamia majukumu yao ikiwemo ujenzi wa mradi huo chini ya kiwango.

Walisema, ni kawaida baadhi ya barabara  katika mji wa Mbinga kuharibika ndani ya muda mfupi tangu zinapojengwa  na hali hiyo inatokana na wahandisi kushindwa kutumia  taaluma zao wakati wa kutekeleza miradi  ya Barabara katika wilaya hiyo.

Wamesema,  kupeana kazi za ujenzi wa miradi ya barabara kwa misingi ya urafiki na kujuana kwa kiasi kikubwa kumechangia miradi mingi ya barabara katika mji huo kujengwa chini ya kiwango na hivyo kushindwa kuleta tija.

Aidha,wameiomba taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (Takukuru) kuchunguza mikataba inayoingiwa kati ya Tarura na Makandarasi ili kufahamu juu ya uwezo wa wakandarasi wanaopewa kazi katika Mji wa Mbinga.

Wakiongea kwa nyakati tofauti,wakazi hao Antonia Komba,Daud Shija na Suzana Ndomba wamesema,  baadhi ya miradi inayojengwa  haimalizi kero za wananchi  licha ya kutekelezwa kwa fedha nyingi za walipa kodi wa nchi hii.

Antonia Komba mkazi wa mtaa huo, alitolea mfano ujenzi wa mifereji iliyojengwa katika barabara ya Kipika mtaa wa Kipika  imedumu kwa miezi saba tu tangu ilipojengwa na sasa imeharibika kutokana na kusombwa na maji ya mvua na hivyo kushindwa kumaliza kero ya muda mrefu  ya wananchi wa kata  ya Matarawe.

Alisema, mifereji hiyo badala ya kuleta faraja kwa wananchi imeonekana sio salama hasa  kwa watoto wadogo wanaopita maeneo hayo  wakati mvua zinaponyesha ambapo maji kutoka maeneo  ya milimani yanapita kwa  wingi.

Mkazi mwingine Daud Shija amesikitishwa  kuona mifereji iliyojengwa kwa fedha nyingi imeanza kuharibika kabla ya mvua hazijawa kubwa na hivyo kuwa na  hofu kuhusu uwezo wa mkandarasi aliyejenga mifereji hiyo.

Shija ambaye ni Mchungaji wa Kanisa la TAG Mbinga, ameiomba Serikali  kupitia taasisi na idara zake kupima  na kujiridhisha juu ya uwezo wa wakandarasi wanaoomba kazi za ujenzi ili kuepusha  matumizi mabaya ya fedha za Serikali.

“kwa kweli  nilipoona mifereji inajengwa katika eneo hili  nilifurahi  na kuipongeza sana Serikali kwa hatua hii,lakini furaha yangu imepotea ghafla baada ya kuona mifereji yote imeharibika kwa muda mfupi tangu ilipojengwa, mimi kama Mtanzania  naishauri Serikali lazima iwe makini na waandisi wake na wakandarasi”alisema Mchungaji Shija.

Ditram Shabani alisema, uwezo mdogo wa makandarasi  ndiyo sababu ya mifereji hiyo kuharibika kwa muda mfupi, tofauti na matarajio ya wakazi wa mtaa huo kwani ni kama hakufanya kazi yoyote katika eneo hilo ambalo ni  kiungo muhimu kwa wakazi wa kata ya Matarawe na maeneo mengine ya Mji wa Mbinga.

Suzana Ndomba alisema, ‘’kila mvua inaponyesha  maji yanayopita katika eneo hilo yanakuwa na kasi kubwa hali inayo hatarisha maisha ya watoto wadogo na hivyo wanalazimika kuwafungia  ndani kama hatua ya kuwaepusha kusombwa na maji.

Meneja wa wakala wa Barabara(Tarura)Mji wa Mbinga Ismail Mafita hakupatikana  kutolea ufafanuzi wa malalamiko ya wananchi kwa kuwa yuko nje ya wilaya ya Mbinga na  hata alipotafutwa kwa njia ya simu alikataa kujibu chochote badala yake alituma ujumbe mfupi (sms)  yuko Hospitali.

Hata hivyo,Kaimu Meneja wa Tarura  Amos Agustine alikiri kuharibika kwa mifereji iliyojengwa katika eneo hilo,ambapo alisema hali hiyo imetokana na athari za mvua zinazo endelea kunyesha kwa wingi katika wilaya ya Mbinga.

Amos ameitaja kampuni iliyojenga mifereji ni Stumack Engineering Co Ltd ya Dar es salaam  huku akitaja gharama za mradi huo ni shilingi Milioni 33.6.

Kwa mujibu wake,kazi ya ujenzi wa mradi huo ilianza mwaka 2018 na kukamilika mwaka 2019 ambapo muda wa uangalizi umemalizika tangu tarehe 17 Novemba mwaka huu na mkandarasi ameshakabidhi mradi kwa Tarura.

Aidha alieleza,mpango uliopo kwa  sasa ni kumpata mkandarasi mwingine ambaye atajenga upya mifereji hiyo, hata hivyo alisisitiza kuwa, suluhisho la kudumu ni kujenga barabara kwa kiwango cha lami  katika eneo hilo  sambamba na kuimarishwa kwa mifereji.

Alisema, eneo hilo ni kati ya maeneo mengi katika Mji wa Mbinga ambapo barabara zake zimeharibika kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha kwa wingi katika mji wa Mbinga.

Mkandarasi wa mradi huo aliyefahamika kwa jina moja la Mwafyenga alipotafutwa kwa njia ya simu alisema hawezi kuzungumza lolote kwa sababu yuko Hospitalini amelazwa.

Mitaro iliyojengwa katika Mtaa wa Kipika kata ya Matarawe na Wakala wa Barabara mjini na vijijini(Tarura) Halmashauri ya Mji Mbinga mkoani Ruvuma ikiwa imeharibika vibaya na mvua zinazoendelea kunyesha kwa wingi katika wilaya hiyo,hata hivyo kuharibika kwa Mitaro hiyo kumetajwa na baadhi ya wakazi wa Mbinga kunatokana na ujenzi wake kuwa chini ya kiwango na kukosa usimamizi makini wa Tarura ambapo imeanza kuharibika katika kipindi cha miezi sita tu tangu mkandarasi akabidhi kazi hiyo.
Mhandisi wa wakala wa Barabara mjni na vijijini(Tarura)Mji wa Mbinga Amos Agustine akieleza jambo juu ya kuharibika kwa mifereji iliyojengwa katika mtaa wa Kipika kata ya Matarawe Halmashauri ya Mji Mbinga mkoani Ruvuma,


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/39yezE7
via

Post a Comment

0 Comments