Ticker

10/recent/ticker-posts

NHIF: TEHAMA imerahisisha upatikanaji wa huduma

Na Grace Michael, Kigoma
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umeimarisha utekelezaji wa majukumu na kurahisisha huduma kwa uwekezaji kwenye mifumo ya TEHAMA inayomwezesha mwanachama kupata huduma kwa haraka zaidi pamoja na Watoa huduma kuwasilisha madai yao kwa haraka.

Maboresho haya yamefanyika na yanaendelea kufanyika kwa lengo la kuwarahisishia wanachama upatikanaji wa huduma na kuondokana na changamoto ambazo awali zilikuwepo za ucheleweshaji wa huduma mbalimbali ikiwemo utoaji wa vitambulisho na upatikanaji wa taarifa za wanachama.

Akizungumza katika mkutano baina ya NHIF na Wanachama wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Kigoma, Meneja Uhusiano wa Mfuko, Bi. Anjela Mziray alisema kuwa uimarishaji wa mifumo ya huduma unaofanywa na Mfuko umewezesha kutatua changamoto za upotevu wa muda kwa wanachama wanapokuwa vituoni, kurahisisha utambuzi wa mwanachama kabla ya huduma, lakini pia kurahisisha uwasilishaji na ulipaji wa madai ya Watoa Huduma.

“Lengo la Mfuko ni mwanachama wetu apate huduma kwa haraka na aweze kuwasiliana nasi kwa haraka anapohitaji, uimarishaji huu wa Mifumo ambao umefanyika na unaoendelea kufanyika, kwanza kabisa unawezesha upatikanaji wa taarifa za wanachama kwa haraka wanapokuwa katika vituo vya kupata huduma na inapotokea changamoto yoyote inatatuliwa kwa haraka zaidi tofauti na awali,” alisema Bi. Mziray.

Alieleza kuwa Mfuko sasa unaendelea na jitihada za kuwaunganisha watoa huduma wengi zaidi na mifumo hiyo ili waweze kuwasilisha madai yao kila siku mara huduma inapotolewa kwa mwanacha bila kusubiri mwisho wa mwezi. Hii inasaidia kushughulikia dai la mtoa huduma kila linapowasilishwa na hivyo kupunguza muda unaotumika kuchakata madai na hivyo kuongeza ufanisi.

“Kwa sasa tayari kuna baadhi ya Watoa huduma ambao wameanza kutumia mfumo wa uwasilishaji wa madai kwa Mfuko kila siku na hatua hii mbali na kurahisha malipo lakini pia inaziba mianya ya udanganyifu na kuwezesha ulipaji wa madai halali yaliyotumiwa na wanachama,” alisema Bi. Mziray.

Akizungumzia suala la kuongeza wigo wa wanufaika wa huduma za NHIF, alisema kuwa Mfuko kwa sasa uko katika hatua za mwisho za kuanzisha utaratibu ambao utawezesha watu wengi kujiunga na kunufaika kwa namna mbalimbali kulingana na mahitaji yao.

 “Mipango yetu ni kuhudumia asilimia 50 ya wananchi ifikapo mwaka 2020 na badae kuwafikia wananchi wote hivyo maboresho na uimarishaji wa huduma tunaoufanya ni kujipanga na utoaji wa huduma kwa wananchi wote ili kila mtanzania aweze kupata huduma za matibabu kwa utaratibu rahisi wa bima ya afya,” alisema Bi. Mziray.

Naye Kaimu Meneja wa NHIF Mkoa wa Kigoma, Bw. Emmanuel Kileo alisema kuwa uwepo wa Ofisi ya NHIF mkoani hapo imesaidia kwa kiasi kikubwa kusogeza huduma kwa wananchi ambapo kwa sasa maofisa wa Mfuko wanawafikia wananchi mpaka ngazi ya kijiji na kuwapatia elimu ya umuhimu wa kujiunga na huduma.

Wakichangia hoja juu ya huduma za Mfuko, wanahabari wa Mkoa wa Kigoma, wameupongeza Mfuko kwa jitihada kubwa ambazo zimefanyika hususan katika kuyafikia makundi mbalimbali na kuboresha huduma za matibabu kwa wanachama wake.

Akitoa  shukrani kuhitimisha mkutano huo, Mwenyekiti wa Chama cha Wanahabari wa Kigoma Bw. Deogratius Nsokolo alisema watauendeleza uhusiano uliopo baina yao na Mfuko huu  hususan katika kuelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kuwa na bima ya afya kabla ya kuugua.


from MPEKUZI http://bit.ly/2Ttl4j3
via

Post a Comment

0 Comments