Ticker

10/recent/ticker-posts

KUMBE LILE NENO LA "BYE BYE" KWA DR.SLAA LILIKUWA NA MAANA YAKE, JIONEE MWENYEWE KWANINI ALIAMBIWA BYE BYE

Katibu Mkuu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Na Mwandishi Wetu
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Dk. Willibroad Slaa, (pichani) ambaye amekuwa ni kama alama ya chama hicho, anaweza kuwa ndiyo mwisho wake kufuatia ujio wa Edward Lowassa aliyejiunga Jumanne iliyopita na jana kuchukua fomu ya kuwania urais kupitia Chadema jijini Dar es Salaam.
Edward Lowassa na baadhi ya viongozi wa Chadema.
Dk. Slaa alionekana katika picha iliyopigwa Jumapili usiku wakati wa Kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho, ambayo pia ilimuonesha Lowassa akiwa amekaa pamoja na wajumbe hao katika meza kuu. Siku hiyo ilidaiwa kuwa alikuwa akitambulishwa kwa wajumbe hao. Wakati kukiwa na taarifa za kuwepo kwa mvutano kati ya wajumbe wa Kamati Kuu, ambazo zinamtaja Dk. Slaa kuongoza wanaokataa ujio wa aliyekuwa kada mkongwe wa chama tawala, Jumanne iliyopita, ambayo Lowassa alitambulishwa rasmi mbele ya wanahabari, katibu huyo mkuu hakuwepo sambamba na Naibu Katibu Mkuu Bara, John Mnyika na Mwanasheria Mkuu, Tundu Lissu.
SLAA, MNYIKA NA LISSU
Dk. Slaa, Mnyika na Lissu kwa miaka mingi walikuwa mstari wa mbele katika kumshambulia Lowassa kwa tuhuma za ufisadi na kutokuwepo kwao siku ya utambulisho huo, kulitajwa kama dalili za mpasuko unaodaiwa kuwepo ndani ya chama hicho kikubwa cha upinzani Tanzania Bara.
Inadaiwa Dk. Slaa haridhishwi na namna chama hicho alichokifanyia kazi kubwa hadi kukubalika miongoni mwa Watanzania, jinsi kilivyompokea pasipo masharti anayodaiwa kutaka yafuatwe na Chadema kuelekea kumpokea kwake.
Dk. SLAA KAJIUZULU?
Wakati gazeti moja (siyo la Global) jana liliripoti kuhusu kujiuzulu kwa kiongozi huyo aliyegombea urais mwaka 2010 na kuleta ushindani mkali kwa mshindi Rais Jakaya Kikwete, msemaji wa chama hicho, Tumaini Makene aliliambia gazeti hili kuwa habari hizo ni uzushi na kwamba Dk. Slaa alikuwa bado ofisini akiendelea na majukumu yake ya kawaida.
Alipoulizwa kwa nini hakuwepo katika hafla ile muhimu ya utambulisho wa Lowassa, Makene alisema chama kina shughuli nyingi, hasa wakati huu kikijiandaa kuelekea uchaguzi mkuu, hivyo kiongozi huyo alikuwa katika kutekeleza majukumu mengine.
LOWASSA KUCHUKUA FOMU ZA URAIS
Hata katika tukio kubwa zaidi lililotokea jana, la mbunge huyo wa Monduli kuchukua fomu ya kugombea urais kupitia Chadema, Dk. Slaa hakuonekana.
Gazeti hili lilipata taarifa za kususa kwa Dk. Slaa katika shughuli za chama hicho na kwamba tangu Jumanne asubuhi alikuwa amejichimbia nyumbani kwake, Mbweni, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
NYUMBANI KWA DK. SLAA
Uwazi Mizengwe lilifika nyumbani hapo na katika hali isiyo ya kawaida, ulinzi uliimarishwa tofauti na siku zingine na waandishi wetu walipojitambulisha na kuhitaji kuonana naye, waliambiwa jambo hilo halitawezekana.
“Mnaweza kurudi tu kwenu kwa sababu mzee hataki kuonana na mtu yeyote kwa sasa,” mlinzi mmoja wa nyumba hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Boniface aliwaambia waandishi wetu, ambao kuona hivyo, waliomba kuandika ujumbe mfupi kwenye karatasi ili umfikie, wakiamini kwa ukaribu wao, wangekaribishwa.
Nusu saa baadaye jana (saa 4.30 asubuhi) mke wa Dk. Slaa, Josephine Mushumbushi, alitoka nyumbani hapo akiwa na dereva wake ndani ya gari lake, lakini katika hali isiyo ya kawaida, hakuweza kusalimiana na waandishi wetu ambao kabla ya jana, walikuwa na uhusiano wa karibu wa kikazi.
Baada ya kukaa hapo kwa saa moja na nusu zaidi, kiasi cha saa sita, watu ambao walinzi waliwaelezea kama ni washauri wa Dk. Slaa walitoka nje ya geti na waandishi wetu walifanikiwa kumuona kiongozi huyo akirejea ndani kwake baada ya kuagana na wageni wake getini.
Hadi walipoondoka nyumbani hapo saa saba mchana, mwanasiasa huyo mwenye ushawishi hakuwa ametoka nje ya geti la nyumbani kwake.
MAKAO MAKUU YA CHAMA
Katika Ofisi ya Makao Makuu ya Chadema, zilizopo Mtaa wa Ufipa, Kinondoni jijini Dar es Salaam, mwandishi wetu aliwashuhudia viongozi mbalimbali wa chama hicho wakiwa katika shamrashamra za kumsubiri Lowassa kuchukua fomu hizo za kuwania urais kupitia chama hicho. Hata hivyo, Katibu Mkuu Dk. Slaa hakuwepo.
Baada ya Lowassa kuwasili ofisini hapo, aliingia Ofisi ya Katibu Mkuu ambako habari zinasema alikabidhiwa fomu hiyo kwenye uzio wa makao makuu na Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe.
Katika tukio hilo la uchukuaji wa fomu, mwanasheria wa chama hicho, Tundu Lissu alikuwepo na hivyo kuondoa uvumi kuwa naye alikuwa akimkwepa Lowassa.
Lakini katika hali ya kushangaza, baada ya shughuli za uchukuaji fomu kumalizika, Lissu alipoulizwa kuhusu kutoonekana kwa Dk. Slaa, alisema kuwa kiongozi huyo alikuwa ndani ofisini kwake akiendelea na vikao.
Lakini alipoelezwa kuwa mwandishi wetu alikuwa na mtendaji huyo wa chama nyumbani kwake, Lissu alikaa kimya na baadaye akajiondoa mbele ya mwandishi wetu bila kufafanua lolote.
Habari zaidi zinasema, tagu ‘kususa’ kwa Dk. Slaa, viongozi wa chama hicho wamekuwa na vikao vingi, vyote wakipanga ni namna gani wanaweza kumshawishi kiongozi huyo kurejea kundini.
Mipango hiyo inajumuisha kuundwa kwa jopo la watu wenye kuheshimiana na Dk. Slaa ili kukaa naye kukabili tatizo hilo, ambalo kama litathibitika kuwa kweli, linaweza kusababisha kuyumba kwa chama hicho tishio kwa CCM. Jana, mitandao mbalimbali ya kijamii ilisambaza habari kwamba Dk. Slaa amejiondoa ndani ya chama hicho. Hata hivyo, hakuna kiongozi aliyekuwa tayari kuelezea uvumi huo.
Imeandikwa na Makongoro Oging, Haruni Sanchawa na Brighton Masalu.