Ticker

10/recent/ticker-posts

HAWA MASTAA WATANO WA YANGA SASA RUKSA KUICHEZEA SIMBA.

 
Mchezaji wa Yanga, Haruna Niyonzima.
Na Wilbert Molandi
WAPO sokoni! Hivi ndivyo utakavyoweza kutamka baada ya wachezaji watano wa Klabu ya Yanga kubakiza miezi sita au chini ya hapo kwenye mikataba yao na timu hiyo.


Kila timu hivi sasa inaangalia nafasi ipi yenye upungufu inayohitaji kuboresha kwa kusajili wachezaji wenye uwezo kwenye usajili wa dirisha dogo linalofunguliwa Novemba 15 na kufungwa Desemba 15.
Wachezaji hao watano ruksa kutua kuichezea Simba kwenye mzunguko wa pili wa ligi kuu ni Mrwanda, Haruna Niyonzima, Mbuyu Twite, Mrisho Ngassa, Hussein Javu na Mganda, Hamis Kiiza.
Kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), wachezaji hao wanaruhusiwa kufanya mazungumzo na klabu nyingine kwa ajili ya kwenda kuichezea kwenye msimu ujao endapo tu watakuwa na mkataba wa miezi sita au chini ya hapo.
Kwa upande wa Twite, yeye anaweza asiwe kwenye kundi hili kwa kuwa alisaini mkataba wa mwaka mmoja ambapo kwa sasa ana miezi saba na ikitokea timu yoyote ikitaka kufanya naye mazungumzo kuanzia Januari, ruksa.

 
Mchezaji wa Yanga, Mbuyu Twite.
Wachezaji hao wanne wengine walisaini mikataba ya kuichezea timu hiyo msimu uliopita, hivyo hadi kufikia Januari, mwaka huu watabakiza miezi sita itakayowaruhusa kufanya mazungumzo na klabu nyingine itakayowahitaji.
Alipotafutwa Niyonzima kuzungumzia hilo, alisema: “Nilisaini mkataba wa miaka miwili msimu uliopita wa ligi kuu, unaotarajiwa kumalizika msimu huu, hivyo hadi kufikia kipindi cha usajili, nitakuwa nimebakiza miezi sita.
“Kwa mujibu wa kanuni za Fifa, nitakuwa ninaruhusiwa kufanya mazungumzo na klabu itakayonihitaji, lakini nisingependa kulizungumzia hilo kwa hivi sasa kutokana na hali niliyokuwa nayo kwenye timu.”