Ticker

10/recent/ticker-posts

Rais Mstaafu Kikwete: Upole, Ukali na Uvumilivu wa Rais mstaafu Mwinyi ni huu

 


Kwa tafsiri ya wengi, Rais wa pili wa Tanzania, Alhaji Ali Hassan Mwinyi, alikuwa mtu mpole, aliyejaaliwa subira na uvumilivu.

Mwinyi maarufu Mzee Rukhsa alifariki dunia saa 11:30 jioni ya juzi katika Hospitali ya Mzena, Kijitonyama jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu ya saratani ya mapafu.

Mwili wake umezikwa leo Mangapwani, Unguja Visiwani Zanzibar. Safari ya maisha ya Mzee Mwinyi imeacha simulizi za kila aina.

Hata hivyo, ipo simulizi kutoka kwa mawaziri wake, kwamba Mwinyi alikuwa mkali na hakuwa akitaka majadiliano mengi pale alipotaka lake.

Jakaya Kikwete ni Rais wa nne wa Tanzania. Alipanda ngazi za juu uongozi kipindi Mwinyi akiwa Rais. Mwaka 1988, Mwinyi alimteua Kikwete kuwa Naibu Waziri wa Maji, Nishati na Madini.

Mwaka 1990, Kikwete akapandishwa kuwa waziri kamili wa Maji, Nishati na Madini. Na mwaka 1994, Mwinyi alimhamisha Kikwete kuwa Waziri wa Fedha.

Septemba 20, 2018, Kikwete akiwa Chuo Kikuu cha New York, Kitivo cha Afrika, alisimulia mambo ambayo yamo kwenye kitabu kijacho kinachohusu maisha yake, “"The Journey of My Life: From a Barefoot Schoolboy to President” – “Safari ya Maisha Yangu: Kutoka Mwanafunzi Mtembea Peku hadi Rais.”

Katika simulizi hiyo, Kikwete alielezea upande wa ukali alionao Mwinyi alipotaka lake. Kwanza, ni siku ambayo Mwinyi alimteua Kikwete kuwa Naibu Waziri wa Maji, Nishati na Madini, papo hapo akapewa na ubunge.

Kikwete alisimulia kuwa mwaka 1988, alipokutana na Mwinyi, ofisini kwake, alibaini kitu tofauti. Kwanza Mwinyi alimuuliza Kikwete kama alikuwa mbunge. Wakati huo, Kikwete alikuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) CCM, vilevile Katibu wa CCM, Wilaya ya Masasi, Mtwara.

Kikwete akamjibu Mwinyi: “Hapana, mimi sio mbunge.”

Mwinyi akamwambia: “Basi nakuteua kuwa mbunge.”

Kikwete akashukuru. Kwa maelezo yake ni kuwa alifurahia uteuzi huo kwa sababu aliona angepata fursa zaidi ya kusafiri kutoka wilayani kwenda Dodoma na Dar es Salaam, katika vikao vya Bunge na chama.

Alipokuwa mjumbe wa NEC, alisafiri mara nne kwa mwaka, safari za mikutano ya Bunge alihesabu zingekuwa nne. Hapo akaona alikuwa ameshaukata.

Wakati Kikwete akiwaza hivyo, Mwinyi akamwambia: “Nakuteua kuwa Naibu Waziri wa Maji, Nishati na Madini.”

Kwa uteuzi huo, Kikwete akaona alikuwa anapewa majukumu makubwa ghafla, akakataa. Akamwambia Mwinyi: “Ubunge inatosha, huko kwingine hapana.”

Mwinyi akamjibu: “Utaweza, haya nenda.”

Baada ya Mwinyi kusema hivyo, hakuwa na habari nyingine, akamwambia Kikwete aondoke, akasubiri taratibu nyingine. Kikwete hakujua kama Mwinyi ni mtu asiyependa majadiliano marefu anapokuwa ameshafanya uamuzi. Siku hiyo alishuhudia.

Ushuhuda wa ukali wa Mwinyi ni mwaka 1990. Kikwete alisimulia kuwa akiwa Naibu Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Mwinyi aliita kikao cha mawaziri na manaibu.

Kila waziri na naibu alifika Ikulu, Dar es Salaam. Na kwa sababu waliamini ni mkutano na ungechelewa kuisha, waliwaruhusu madereva waondoke na magari.

Mawaziri na manaibu waziri walipokuwa kwenye chumba cha mkutano Ikulu, huku madereva wao wakiwa wameondoka na magari, Mwinyi aliingia, kisha akasema: “Nawashukuru kwa muda wote tuliofanya kazi pamoja. Nawaagiza ninyi wote mjiuzulu nafasi zenu.”

Kwa mujibu wa Kikwete, Mwinyi aliposema maneno hayo, aliondoka. Akawaacha mawaziri na manaibu mawaziri wakiwa kwenye hali ya kutoelewa, kwani hakutoa nafasi ya kuuliza swali na hakutaka kufafanua chochote.

Kwa vile wakati huo hakukuwa hata na simu za mkononi, haikuwezekana hata kuwaita madereva ili wawape usafiri wa kuondoka Ikulu, ikabidi watoke na kuanza kutembea kwa miguu, wakiwa wameongozana. Kikwete alisema, ni bahati hazikuwa zama za mitandao ya kijamii, vinginevyo picha zao zingezagaa mno mitandaoni.

Rejea hizo mbili za Kikwete zinaweza kuonesha ni kiasi gani Mwinyi si mpole kama wengi humtafsiri, bali huwa mkali anapokuwa ameshafanya uamuzi. Asiyetaka kutoa nafasi ya ufafanuzi au kusikiliza hoja za upande wa pili ili kukandamiza kile anachokusudia.

Kwa waliofanya kazi na Mwinyi, wanasema kuwa uongozi wake haukuwa mwepesi, kwani Mwalimu Julius Nyerere, alikuwa anafuatilia nyendo zote za Serikali na kukosoa mabadiliko. Kitendo cha kuhamisha nchi kutoka sera za Ujamaa na Kujitegemea hadi Soko Huria, Nyerere akiwa hai, halikuwa jambo jepesi.

Ugumu wa Mwinyi hutafsiriwa pia kwenye mageuzi ya Azimio la Arusha, lilipoibuka Azimio la Zanzibar, ambalo lilibadili baada ya vipengele na masharti yaliyokuwemo kwenye Azimio la Arusha. Mwalimu Nyerere aliumizwa sana lakini Mwinyi hakurudi nyuma.

Pamoja na hoja hizo kuwa Mwinyi alikuwa kiongozi mkali na mwenye msimamo mkali, bado upole na uvumilivu zinabaki kuwa sifa zake kubwa na muhimu. Alikosolewa mara nyingi lakini hakuwa na muda wa kujibu waliomkosoa na alivumilia mashambulizi.

Sifa ya upole na utulivu wa Mwinyi inaonekana hata kwenye mashambulizi ya Mwalimu Nyerere. Ndani ya kitabu “Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania” kilichaondikwa na Mwalimu Nyerere na kutoka mwaka 1994, Mwinyi ameitwa ni kiongozi dhaifu. Hata hivyo, hakujibu kitu.

pMwalimu Nyerere ameandika “Mwinyi ni mtu mzuri lakini dhaifu”. Na kwa udhaifu huo, akasema aliamua kujitolea kusaidia katika mchakato wa kumpata mrithi wa kiti cha urais katika Uchaguzi Mkuu 1995. Utulivu wa Mwinyi kupokea mshambulizi ni mambo yanayopambanua upole na uvumilivu wake.

Kipindi cha Mwinyi iliwahi kuripotiwa na vyombo vya habari kuwa alioa mwanafunzi wa kidato cha tatu. Wanafunzi wa sekondari wakawa wanamwita shemeji. Habari hiyo ilikuwa uongo mkubwa. Hata hivyo, hakuna aliyefungwa, aliyechukuliwa hatua, halipo gazeti lililofungiwa au kuadhibiwa. Hakika, alikuwa kiongozi mpole.

Kati ya mwaka 1992 hadi 1995, ni kipindi ambacho mfumo wa vyama vingi vya siasa uliruhusiwa. Na ruhusa hiyo, yaliibuka mashambulizi makubwa dhidi ya Mwinyi na Serikali aliyoiongoza kutoka kwa wanasiasa hasa wa vyama vya upinzani na wachambuzi wa siasa, lakini Mwinyi alivumilia kila shambulizi na kubaki mpole.

 

Post a Comment

0 Comments