Ticker

10/recent/ticker-posts

SIMANZI: Polisi Watafuta Kichwa cha Mwanachuo Aliyetekwa na Kuuawa

Nairobi. Maofisa wa polisi wa Nairobi nchini Kenya, wanatafuta kichwa cha mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Jomo Kenyatta (JKUAT) anayedaiwa kuuawa na mtu aliyekutana naye mtandaoni.


Taarifa iliyoandikwa na tovuti ya Taifa Leo ya nchini humo inaeleza mwanafunzi huyo, Rita Waeni (20) alitekwa na mtu huyo kwa lengo la kujipatia fedha kutoka kwa familia yake.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa ripoti ya polisi imebaini aliyetekeleza mauaji ya Rita alitumia msumeno kukata mwili wake vipande vipande Jumapili ya Januari 14, 2024.

Akisimulia ilivyokuwa kabla ya kufikwa na mkasa huo, msemaji wa familia ya marehemu, Dk Lilian Mutea amesema mapema Jumamosi Rita aliondoka nyumbani kwa shangazi yake mtaani Syokimau, Machakos kwa ajili ya kukutana na rafiki yake.

“Lakini ilipofika Jumapili, saa 11:00 alfajiri, baba yake alipokea ujumbe mfupi wa simu, akitakiwa kutoa KSh500,000 (Sh7,801,857 za Kitanzania), ili kumkomboa Rita ndani ya saa 24,” imesema familia hiyo kupitia Dk Mutea.

Familia imesema iliripoti polisi tukio hilo na uchunguzi ukaanza huku ikizidi kupokea jumbe za kutaka fedha hizo. Hata hivyo, familia hiyo imesema haikupata maelezo zaidi kuhusu fidia hiyo pamoja na nafasi ya kuilipa.

“Tulikuja kumtambua mtoto wetu ameuawa kikatili asubuhi ya Jumapili karibu na Thika Road Mall (TRM), wazazi wake, ndugu zake na familia yetu yote bado hatujakubali tukio hilo la kusikitisha.


“Binti yetu alikuwa msichana mwenye akili na mwerevu. Alikuwa mtu mwenye roho nzuri na anayejali, mkarimu, mcheshi na mwenye furaha,” imesema familia hiyo.

Hata hivyo, juzi Jumanne, mwanaume anayeaminika kuwa mshukiwa mkuu wa mauaji hayo alinaswa Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA) alipokuwa akijaribu kuondoka nchini huku ikidaiwa kuwa walikutana mtandaoni na marehemu Rita.

Post a Comment

0 Comments