Ticker

10/recent/ticker-posts

Kuhusu Katiba Mpya:Vyama 11 vya siasa vyataka mchakato wa Katiba uendelezwe,...Soma hapa zaidi

 Dar es Salaam. Umoja wa vyama 11 vya siasa visivyokuwa na wawakilishi bungeni umetaka mchakato uanzie ilipoishia Katiba inayopendekezwa, wakati Serikali itakapokuwa tayari.

Akizungumza leo Alhamisi Agosti 19 jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa DP, Abdul Mluya amesema wanakubaliana na watu wanaotaka mchakato wa Katiba mpya ufufuliwe, lakini sio kwa mtindo unaotakiwa na vyama vingine vya siasa.

“Hakuna sababu ya kuingiza nchi kwenye hasara nyingine ya kuanza mchakato wa katiba, tuanzie pale tulipoishia. Tumeshaambiwa kuna kazi kubwa ya kurejesha uchumi baada ya kuathiriwa na janga la Uviko 19,” amesema Mluya

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa ADC Doyo Hassan amewataka wanasiasa kupunguza mihemko na kutumia lugha nzuri wanapotaka kuwasilisha maombi yao.

 “Rais ameshasema atakutana na sisi, kumtolea maneno ya hovyo haisaidii, tusubiri atakapokuwa tayari tutakutana naye tumuelezee yote tunayotaka.

“Kumshambulia kwa maneno haina tija hayo yote na hoja zetu tutuyatoe tutakapokutana nae, kwa kifupi sisi vyama tusivyo na uwakilishi bungeni tuna mengi ya kuzungumza naye hivyo tunaumia wenzetu wanavyotaka kuiharibu hiyo fursa,” amesema Doyo.

Kuhusu chanjo ya Uviko 19 Doyo amewakemea wanaopotosha na kueleza umma kuwa ina madhara kitu ambacho hakina ukweli.

“Maneno ya askofu Gwajima yanachefua wengi msione tunanyamaza, mimi nimechanja na hadi sasa sijaona madhara yoyote hivyo watu kama hawa ni wa kupuuzwa.”

Imeandikwa

Elizabeth Edward na Irene Meena

Mwananchi

Post a Comment

0 Comments