Ticker

10/recent/ticker-posts

SHEIKH WA MKOA WA AIPA MAJUKUMU HALMASHAURI YA BAKWATA MKOA WA MWANZA


Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, alhaji Sheikh Hasani Kabeke, akiungumza na wajumbe wa Halmashauri ya BAKWATA mkoani humu jana (hawapo pichani) wakati akiizindua hamashauri hiyo kwenye Ukumbi wa Alhaji Salum Ferej.
…………………………………………………………………………
NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA
SHEIKH wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Sheikh Hasani Kabeke, amezindua Halmashauri ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) mkoani humu na kuitaka kubuni miradi ya kiuchumi na vyanzo vipya vya mapato badala ya kuangalia miradi waliyoikuta.
Pia amesema mali za wakfu za Waislamu zilizokuwa zikiuzwa na watu wenye tamaa kwa maslahi yao sasa hazitauzwa  baada ya mali hizo kuingizwa kwenye katiba na hivyo wajumbe wa halmashauri hiyo ni muhimu wakatambua majukumu yao na kujiepusha na migogoro inayosababishwa na kutoheshimu Katiba ya BAKWATA.
Shekhe Kabeke alisema jana jijini hapa wakati akizindua Halmashauri hiyo ya BAKWATA Mkoa wa Mwanza, uzinduzi uliofajyika kwenye Ukumbi wa Alhaji Salum Fereji jijini hapa.
Alisema Halmashauri ya BAKWATA imepewa mamlaka ya kutekeleza mipango ya mkoa, kuweka mipango na wadaawa, hivyo wabuni miradi mipya ya kiuchumi,vyanzo vya mapato na watambue majukumu yao na kuepeuka migogoro kwa kutoiheshimu katiba .
“Tuache tabia ya kutolea macho miradi tuliyoikuta, tufikirie uchumi kwa mipango na kuibua miradi ya kuleta maendeleo yenye manufaa kwenye jamii, tuwatafute wadau wa maendeleo na tuwatumie wataalamu wetu (waumini wa Kiislamu) watusaidie kutengeneza mipango ya maendeleo ili siku tukiondoka tuache alama,”alisema Sheikh Kabeke.
Alisema ili kutoka BAKWATA ya majibizano, majungu na migogoro kwenda BAKWATA ya maendeleo kulingana na kauli mbiu ya Mufti wa Tanzania Abubakar Bin Zuberi Mbwana ya Jitambue, Badilika,Acha Mazoea wanakusudia kujenga maabara ya vipimo na kufungua duka la madawa ya binadamu ili kujenga uchumi.
Aidha, alisema tabia ya kuuza mali za wakfu kwa maslahi ya watu wachache imepata ufumbuzi ambapo sasa  hazitauzwa baada ya kuingizwa kwenye katiba ya BAKWATA na pia kila mradi ndani ya msikiti asilimia 20 mapato yake yatapelekwa Makao Makuu na kwenye kata na kukiri halmashauri zilizopita hazikufanya vizuri.
“Tumefanikiwa kutekeleza baadhi ya miradi sababu ya uwazi katika mapato na matumizi, awali watoaji  walipoteza imani na kukata tamaa lakini kwa mazingira ya sasa Waislamu lazima tuwe wazi kwenye mapato,tuwe na takwimu za Waislamu Mkoa wa Mwanza maana hatuwezi kuwa na mipango bila kuwa na takwimu.Kuwe madaftari ya mali za wakfu baada ya kuzitambua nyaraka za umiliki akabidhiwe Katibu Mkuu BAKWATA,”alisema Sheikh Kabeke.