Ticker

10/recent/ticker-posts

MRADI MKUBWA WA UJENZI WA MIUNDOMBINU BANDARI YA KABWE MKOANI RUKWA WAKAMILIKA KWA ASILIMIA 85, MKANDARASI ATAJA CHANGAMOTO


Baadhi ya nguzo ambazo zinatarajiwa kutumika katika ujenzi wa gati mpya katika bandari ya Kabwe iliyopo mkoani Rukwa.Bandari hiyo ni moja ya bandari ambazo miundombinu yake inaboreshwa katika Ziwa Tanganyika.
Mafundi wakiendelea na kazi ya kusuka nondo kwa ajili ya kutengeneza nguzo ambazo zitatumika kusimamisha gati ya bandari ya Kabwe.
Mmoja wa mafundi akiendelea kuwajibika wakati wa ujenzi wa miundombinu ya bandari ya Kabwe iliyopo katika Ziwa Tanganyika upande wa Mkoa wa Rukwa.
Mafundi wakiendelea na kazi ya ujenzi wa miundombin katika bandari ya Kabwe mkoan Rukwa.
Baadhi ya mafundi wakiendelea na majukumu yao katika shughuli za ujenzi wa miundombinu katika Bandari ya Kabwe.



Na Said Mwishehe, Michuzi Globu - Rukwa

UJENZI wa mradi wa miundombinu katika Bandari ya Kabwe mkoani Rukwa ambao unagharimu Sh.bilioni 7.498 tayari umekamilika kwa asilimia 85 na mkandarasi wa ujenzi huo ambaye ni Sumry's Enterprises Ltd anatarajia kuukabidhi mradi huo Aprili mwaka 2020.

Kwa mujibu wa Meneja Msaidizi wa Mradi wa gati ya Bandari ya Kabwe Usanifu na Ujenzi kutoka Sumry's Enterprises Ltd William Shila amesema kuwa walipewa kazi ya ujenzi wa miundombinu hiyo ikiwemo ya gati, ofisi, majengo ya abiria pamoja na majengo mengine wezeshi Aprili 2 mwaka 2018 na kwa namna ambavyo kazi inakweda watakabidhi mradi kwa wakati.

Ameongeza kuwa utakapokamilika mradi huo utakuwa umesaidia kusogeza huduma ya usafiri wa meli karibu na wananchi wa Rukwa na maeneo yanayozunguka pamoja na nchi jirani ikiwemo ya DRC huku akieleza faida za sasa wakati ujenzi unaendelea ni kwa wananchi wa maeneo hayo kupata ajira kwani kila mwezi wanatumia Sh.milioni 30 kulipa wafanyakazi.

Kuhusu changamoto ambayo wanakutana nayo kwenye ujenzi huo, amesema kubwa ni ya mawimbi ya maji ya ziwa kuwa makubwa kiasi cha kusababisha ujenzi kusimama mara kwa mara. "Changamoto yetu hapa ni hali ya hewa kwa maana mawimbi kuwa makubwa ya maji yanakwamisha kasi ya ujenzi huu, kwani kuna wakati tunalazimika kusimama na mawimbi yanapopungua tunaendelea na ujenzi."

Ametumia nafasi hiyo kutoa shukrani kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania(TPA) pamoja na Serikali ya Awamu ya Tano kwa uamuzi wake wa kutoa kipaumbele kwa wakandarasi wazawa kupewa kazi ya ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini kwetu."Tunaishukuru sana TPA kwa namna ambavyo imefungua fursa kwetu wazawa, miradi mingi ya bandari katika Ziwa Tanganyika inafanywa na Watanzania, tunashukuru kwa uamuzi wao wenye tija kwetu na kwa wananchi kwa ujumla."

Awali Meneja wa Bandari za Ziwa Tanganyika Percival Salama amesema mradi wa Bandari ya Kabwe ni mradi mkubwa kuwekezwa kwenye bandari za Ziwa Tanganyika na kwamba wenzao wa DRC wanafanya usafirishaji mkubwa wa shehena za mahindi na mchele, hivyo ni bandari muhimu na TPA iliamua kuweka fedha Sh.bilioni 7.498.

"Awali tulijenga gati dogo mwaka 2015 ambalo lilikuwa lina saidia maboti kufanya huduma lakini Serikali kupitia Mamlaka ikaona fursa ya Kabwe ni kubwa na kama unaangalia kwenye mchango wa mapato ya Bandari hii ni bandari ya nne kwa kuchangia mapato , ya kwanza ni Bandari ya Kigoma, ya pili Kasanga, ya tatu Kibirizi na kisha hii ya Kabwe,"amesema na kuongeza mwaka jana ilichangia mapato ya Sh.milioni 100 , hivyo si bandari ndogo na kwa kuweka miundombinu maana yake kwamba sasa watawavuta wenye meli kwani awali haukua na gati la meli kuweza kuegesha.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/36VqPwc
via

Post a Comment

0 Comments