Ticker

10/recent/ticker-posts

WAKURUGENZI WA HALMASHAURI WANA WAJIBU WA KUSIMAMIA UTENDAJI SEKTA YA ARDHI-DKT MABULA


Na Munir Shemweta, WANMM MWANZA
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amewataka Wakurugenzi wa halmashauri nchini kuelewa kuwa pamoja na watumishi wa sekta ya ardhi kuhamishiwa Wizara ya Ardhi lakini bado wana jukumu la kusimamia utendaji wa sekta hiyo.
Dkt Mabula alitoa kauli hiyo jana alipofanya ziara katika halmashauri ya jiji la Mwanza pamoja na Manispaa ya Ilemela akiwa katika ziara ya kukagua utendaji wa sekta ya ardhi katika Kanda ya Ziwa inayojumuisha mikoa ya Mwanza, Simiyu, Mara na Geita.
Alisema, tangu watumishi wa sekta ya ardhi walivyohamishiwa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi wakurugenzi wengi wa halmashauri wameona kama wamejivua kusimamia utendaji wa watumishi wa sekta hiyo jambo alilolieleza kuwa siyo sahihi kwa kuwa mamlaka ya upangaji Majiji, Miji na Manispaa unabaki kwa halmashauri.
‘’kazi pekee inayosimamiwa na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa watumishi wa sekta ya ardhi ni katika masuala ya nidhamu na ajira ambapo katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi anawajibika’’ alisema Dkt Mabula.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisema katika kuboresha sekta ya ardhi nchini huduma za sekta hiyo sasa zimesogezwa katika mikoa badala ya kutegemea ofisi za Kanda alizozieleza kuwa ziko mbali kwa baadhi ya mikoa jambo linalowafanya wananchi kushindwa kupata huduma kwa urahisi.
Katika kufanikisha hilo Dkt Mabula aliwataka Wakuu wa mikoa kuharakisha uanzishwaji ofisi za mikoa kwa kutenga ofisi ili wananchi waweze kupata huduma za ardhi bila usumbufu ambapo alitolea mfano wa mikoa ya Tanga, Ruvuma, Mtwara na Simiyu kuwa tayari ishatenga ofisi kwa ajili ya mikoa yake.
Kwa upande wake Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Ziwa Makwasa Biswalo alisema mkakati wa ofisi yake kwa mwaka huu ni kuhakikisha uanzishaji ofisi za mikoa usaidie kupunguza changamoto za sekta ya ardhi katika mikoa mbalimbali.
Akiwa katika ofisi za Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Dkt Mabula lielezwa na Mkuu wa Idara ya Mipango Miji na Ardhi katika halmashauri hiyo Shukurani  Kyando kuwa, halmashauri hiyo imekuwa na mafanikio makubwa katika utoaji hati, urasimishaji na upimaji maeneo  mbalimbali ingawa imekuwa na changamoto kubwa ya utapeli unaofanywa na madali kwa kuuza kiwanja kimoja kwa mtu zaidi ya mmoja.
Hata hivyo, alisema katika kukabiliana na utapeli huo tayari wamewakama matapeli saba na baadhi yao tayari wamefikishwa katika vyombo vya sheria huku mmoja akikabidhiwa kwa Taasisi ya kupambana na kuzuia Rushwa (Takukuru) na kuwataka wananchi wanaotaka kununua viwanja kuhakikisha wanajiridhisha katika ofisi za ardhi ama ofisi za ardhi za kanda ili kuepuka kutapelewa.
 Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akipata maelezo ya maendeleo ya ujenzi wa kivuko kipya cha Kayenze- Baze jijini Mwanza   kutoka kwa Meneja wa Masuala ya fedha wa Kampuni ya Songoro inayojenga kivuko hicho wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa kivuko hicho jijini Mwanza
 Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiangalia moja ya Majalada katika ofisi za Ardhi Jiji la Mawanza jana akiwa katika ziara yake ya kuangalia utendaji kazi sekta ya ardhi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa. Wa pili kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Dkt Phillis Nyimbi.
 Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiwa ndani ya kivuko kipya cha Kayenze- Baze kinachotarajiwa kuanza majaribio mwezi Novemba 2019 wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa kivuko hicho jijini Mwanza
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiwa katika kivuko kipya cha Kayenze- Baze jijini Mwanza ambacho kinatarajiwa kuanza majaribio Novemba 2019 wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa kivuko hicho jijini Mwanza.


from CCM Blog https://ift.tt/2B6Hy1H
via

Post a Comment

0 Comments