Ticker

10/recent/ticker-posts

Mtanzania Mohamed Mansour Nassor Achaguliwa kuwa Rais wa Chuo kikuu cha Patrice Lumumba Urusi..ni Huyu Hapa

Image may contain: 4 people, including Mohamed Mansour Nassor, text
Mtanzania wa kwanza kushinda nafasi ya Urais wa wanafunzi wote wa nchi za Afrika wanaosoma chuo Kikuu cha Patrice Lumumba mjini Moscow nchini Urusi  Bw.Mohamed Mansour Nassor  kabla ya kuingia Kujieleza na kuomba kura kwenye Uchaguzi Mkuu huo jana ambao alishinda kwa Kishindo..Ikumbukwe Mohamed alikuwa mwanafunzi wa Chuo Cha KImataifa Cha Diplomasia Kilichopo Kurasini Dar es Salaam na sasa katika Chuo cha patrice Lumumba anafanya Shahada ya Uzamivu(Phd)...Soma hapa kauli yake baada ya Uchaguzi huo ukumtangaza jana kama mshindi wa Jumla wa uchaguzi huo..

''Shukurani zote kwa Mwenyezi Mungu!...Mungu akisema ndio hakuna wa kusema hapana!
Uwanja wa Siasa,Diplomasia na Mahusiano ya Kimataifa
Ndugu Watanzania ni furaha kubwa inatakiwa iwe kwetu sote, ni habari njema kwa nchi yetu. Na ni heshima kubwa kwangu na kwa nchi yetu!
Uchaguzi wa Umoja wa Vijana na Wanafunzi wa nchi za Afrika katika Chuo Kikuu cha Patrice Lumumba (ASSAFSTU) uliofanyika mjini Moscow nchini Urusi siku ya Jumapili ya tarehe 11/11/2018 haukua rahisi. Lakini nimepata ushindi mkubwa na wa aina yake!. Nilithubutu, nikagombea na nikasimama mbele ya watu nikatoa hotuba na hoja zangu na mipango yangu ya uongozi na nikaulizwa maswali magumu sana na nikajibu na kuyapangua kwa hoja na nikashinda Uchaguzi. Na sasa ni rasmi Raisi wa Umoja wa vijana na Wanafunzi wa nchi zote za Afrika katika Chuo Kikuu cha Patrice Lumumba(PFUR-RUDN).Kwa hakika ni moja ya nafasi kubwa sana hio katika muktadha wa siasa na Mahusiano ya Kimataifa na Diplomasia.
Ni tukio la kihistoria na kumbukumbu kubwa.Hii ni mara ya Kwanza kwa kijana wa Kitanzania kushika nafasi hii kubwa tangu kuasisiwa kwa Chuo hiki mwaka 1960 ambacho kilisaidia sana katika vuguvugu la ukombozi wa nchi za Afrika dhidi ya Ukoloni. Chuo hiki kina Walimu,wahadhiri na maprofesa na wanafunzi kutoka nchi zaidi ya 155 duniani ambapo kinabeba ustaarabu wa dunia,dini mbalimbali, tamaduni za dunia na lugha na makabila ya dunia. Pia baadhi ya watu maarufu na maraisi wa Afrika na Asia na viongozi wengine waliwahi kusoma na kuna waliotembelea Chuo hiki kwa muda tofauti.Hii heshima kubwa kwangu na Taifa letu, Tanzania. Kwa hakika Tanzania inaendelea kupaa Kimataifa.
Image may contain: Mohamed Mansour Nassor, standing
Niliwasili Mjini Moscow nchini Urusi nikiwa kijana mdogo sana miaka 10 iliopita kujiunga na Chuo Kikuu Cha Urafiki cha Watu wa Urusi(Peoples’ Friendship University of Russia) au Chuo Kikuu cha Patrice Lumumba katika masomo ya taaluma ya Uchumi na lugha za kigeni na hadi kufikia kuingia kiwango cha juu cha Shahada ya Uzamivu ya Uchumi(PhD in Economics).Patrice Lumumba ni nyumba yangu ya pili ndio maana Mwaka 2017 Kupitia Mwongozo na lezi wa maprofesa wangu kwanza wakanifunza kufanya machapisho ya kisayansi na hadi leo tayari nimeweza kuandika makala zaidi ya 30 katika na kufanya uchambuzi katika masuala ya Uchumi,Siasa,Diplomasia na Mahusiano ya Kimataifa Katika vyombo vya habari vya Tanzania na vya Kimataifa(BBC,DW,IRIB) na katika Majarida ya Kimataifa nchini Urusi na Ulaya ya Magharibi na katika magazeti makubwa(Daily News,The Citizen) ya Tanzania lakini pia maprofesa wangu wakasema wewe tumekulea wenyewe hapa na tunakujua na tunajua uwezo wako. Hivyo basi nikatunukiwa nafasi ya kufundisha Chuo Kikuu nikiwa kijana pekee kutoka bara la Afrika mwaka huo na nikawa Mhadhiri Msaidizi(Assistant Lecturer) Katika Kitivo cha Uchumi chuoni hapo. Katika kipindi cha Mwaka mmoja na nusu hapo kwa uwezo wa Mungu kupitia maarifa na elimu na uzoefu niliopata Chuo Kikuu Cha Patrice Lumumba na Chuo Cha Diplomasia Cha Tanzania(CFR) na kwengineko(mafunzo ya Kozi fupi mbalimbali) na Mwongozo na ushauri wa watu na viongozi mbalimbali na mabalozi mbalimbali na pia hasa kupitia wana SOYUZ ALUMNI ASSOCIATION OF TANZANIA basi ikanisaidia sana. Kwanza nikaaminiwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Urusi na nikateuliwa nafasi mbili kubwa za uongozi kwa miezi tofauti katika maeneo ya Mahusiano ya Kimataifa nazo ni: Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Kiswahili Cha Moscow(CHAKIMO),Makamu Mwenyekiti wa Diaspora ya Watanzania nchini Urusi(TADIRU). Kisha nikateuliwa kama Balozi wa Watanzania wote waliowahi kusoma nchini Urusi chini ya Chama chetu rasmi (SOYUZ Alumni Association of Tanzania).Daima hakika Mungu ni mjuzi zaidi na Mwema zaidi yetu!
Image may contain: 6 people, including Mohamed Mansour Nassor, people smiling, people standing and text
Vijana na Wanafunzi wa Kitanzania walikuja kumpongeza kwa ujumla wote tunawakilisha na kulitangaza Taifa letu anga za Kimataifa
Mwaka 2016 nilimaliza Shahada ya Umahiri yani Masters nilikua mmoja wa Wanafunzi bora na Mwanafunzi bora kwa Waafrika wote katika Kitivo cha Uchumi Chuoni hapo. Leo hii Mwaka 2018 baada ya miaka hio yote kwa uwezo wa Mungu vijana na wanafunzi wa Kiafrika wa nchi zote wa Afrika wakaamua na kusema mara hii Raisi wetu ni Mtanzania sio kila mara atokee nchi za Afrika Magharibi hasa Nigeria. Wao hawakutizama rangi yangu, dini yangu,kabila langu, nchi yangu wala asili yangu. Kwa hakika naamini kwa walionichagua na walioniteua katika nafasi mbalimbali waliona nidhamu yangu na uwezo wangu pamoja na vigezo muhimu na sifa stahiki. Kwa hakika ni heshima kubwa sana Kukubalika na kuaminiwa na watu wa nchi mbalimbali katika anga za Kimataifa.
Image may contain: 10 people, people standingKama ilivyo desturi ya wanasiasa Mohamed baada ya ushindi alipiga picha ya Pamoja na jopo la wasaidizi wake walliompigia kampeni  kutoka nchi mbalimbali za Afrika (Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu na Mkatibu na Manaibu Katibu wa idara mbalimbali)Mara baada ya kutangazwa mshindi wa Uchaguzi na kushika nafasi ya Urais Chuo Kikuu cha Patrice Lumumba Urusi kama mtanzania wa Kwanza kushika nafasi Hiyo.

Baada ya Mwongozo wa Mungu na dua za Wazazi wangu bado natanguliza Shukurani nyingi sana kwa wanafunzi na vijana wa nchi za Afrika wa Chuo Kikuu cha Patrice Lumumba kwa kuniamini na kunichagua kuwa Raisi wao. Pia Shukrani sana kwa walimu na maprofesa wangu na kwa Chuo Changu Kipenzi, Patrice Lumumba kwa yote mema nilioyapata kutoka kwao.Bila ya kusahau shukurani kwa Walimu wangu na Chuo Cha Diplomasia cha Tanzania kwa ujumla ambao walinisaidia kuwa pia Mwanafunzi bora mwaka 2017 kwa Chuo cha Diplomasia na kwa Tanzania nzima kupitia TAHLISO katika Stashahada ya Uzamili ya Usimamizi wa Mahusiano ya Kimataifa(PGD-MFR) na pia kwa kunipika na kunipa maarifa na elimu kubwa katika Mahusiano ya Kimataifa na Diplomasia.
Naomba Mungu aniongoze zaidi na anipe hekima sana katika uongozi wangu. Dua zenu muhimu sana vijana wenzangu na Watanzania wenzangu kwani kuwa nafasi hii mimi zaidi ni maslahi ya Taifa letu.
Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania!!
Ahsante sana!