Ticker

10/recent/ticker-posts

UKAWA WATOFAUTIANA,WASHINDWA KUELEWANA..SOMA HAPA

UMOJA wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) umeendelea kushikilia hatima ya kupatikana kwa Katiba Mpya yenye maridhiano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayopaswa kupendekezwa na Bunge Maalumu la Katiba kwa wananchi kwa ajili ya kupigiwa kura ya maoni.

Hata hivyo, licha ya UKAWA kuhodhi upatikanaji wa Katiba Mpya yenye maridhiano, taarifa zinabainisha kwamba uamuzi wa jumla wa wajumbe wake wa Bunge la Katiba kutoshiriki mkutano ujao wa Bunge hilo umeanza kuingia dosari, mgongano wa kimtazamo ukianza kuibuka.

Kwa mujibu wa taarifa za uhakika ambazo gazeti hili limezipata kutoka kwa vyanzo kadhaa vya habari, UKAWA imegawanyika kimtazamo katika mapande mawili kwa sasa.

Upande mmoja ni ule wenye msimamo wa kutokurejea bungeni hadi pale Rasimu ya II ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, iliyowasilishwa katika Bunge Maalumu la Katiba na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph Warioba itakaporidhiwa kujadiliwa bila kutiwa viraka vikubwa.

Kwa mfano, kati ya viraka ambavyo kundi hilo la UKAWA halivitaki ni kile kinachopachikwa kuziba muundo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wenye Serikali tatu, ambalo ndilo pendekezo la Tume ya Warioba.

Kundi hili linapingana na mapendekezo ya muundo wa Serikali mbili ambao unapigiwa chapuo na wajumbe wa Bunge Maalumu wengi kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM).

Kundi hili linawajumuisha baadhi ya viongozi wakuu wa vyama vya siasa walioko ndani ya Bunge la Katiba na wale walioko nje ya Bunge hilo.

Hao ni pamoja na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe na Katibu Mkuu wake, Dk. Wilbroad Slaa.

Wengine katika kundi hili ni James Mbatia ambaye pia ni mjumbe wa Bunge la Katiba na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, Profesa Ibrahim Lipumba – Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) na mjumbe wa Bunge la Katiba.

Lakini katika kundi la pili, wamejitokeza baadhi ya viongozi waandamizi wa upinzani ambao wanaamini si hatua muafaka kususia mkutano wa Bunge la Katiba.

Katika kundi hili, viongozi hao wanaungana na ushauri uliowahi kutolewa na Rais Jakaya Kikwete kwamba, mahali muafaka katika kusaka suluhu ya mtanziko uliojitokeza kati ya wajumbe wa Bunge la Katiba ni katika Bunge hilo hilo, kupitia Kamati yake ya Maridhiano.

Katika hali hiyo, vyanzo vya habari vya gazeti hili vimedokeza kwamba kundi la kwanza linatumia zaidi mikutano ya hadhara kuhamasisha wananchi lakini kundi la pili, haliamini katika mbinu hiyo.

Kwamba mbinu ya mikutano ya hadhara haina tija inayojitosheleza dhidi ya kutumia kamati za Bunge, ikiwamo Kamati ya Maridhiano, kutafuta suluhu.

Lakini akizungumzia hatua za kutafuta suluhu, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Slaa, Jumanne wiki hii, alimwambia mwandishi wetu kwamba; “maoni ya wananchi hayawezi kutafutiwa suluhu hata kidogo, bali yanapaswa kuheshimiwa tu.”

Wakati Dk. Slaa na wenzake katika kundi la kwanza la UKAWA wakiamini hivyo, taarifa za uhakika zinabainisha ya kuwa, utayari wa baadhi ya wajumbe wa UKAWA kurejea kwenye Bunge la Katiba umekwishakujipambanua.

“Baadhi yetu, baada ya kufanya mikutano kadhaa ya hadhara, licha ya mikutano hiyo kufanikiwa lakini tathmini yetu inatuelekeza kwamba ni muhimu kurejea bungeni, kusimamia hoja ambazo tumezifafanua kwa wananchi mikutanoni, ikishindikana tutaendeleza harakati zetu wakati wa kampeni kuelekea upigaji kura ya maoni.

“Bunge la Katiba tumebaini ni sehemu muafaka kwetu kuendelea kupaza sauti juu ya kile tulichokisema kwenye mikutano ya hadhara.

"Na katika hali ya kutetea hayo, bila shaka wenzetu wanaweza kutuelewa wakakubaliana nasi au sisi na wao tukatafuta muafaka wa ‘katikati’ wenye kubeba maslahi ya nchi,” alisema mmoja wa viongozi waandamizi wa upinzani kutoka Zanzibar, ambaye ni mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba-UKAWA.

Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta pamoja na Makamu Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samia Suluhu Hassan, hawakuweza kupatikana kufafanua kuhusu juhudi zao kuwashawishi UKAWA kurejea bungeni.

Hata hivyo, Katibu wa Bunge Maalumu la Katiba, Hamad Khamis Yahya, alimweleza mwandishi wetu kwamba suala la kuwashawishi UKAWA kurejea bungeni ni la kisiasa zaidi na si la kiutendaji na kwa hiyo, kazi hiyo ilikuwa ikifanywa na ofisi ya Mwenyekiti wa Bunge hilo.

Alisema wao, wakiwa ni watendaji wakuu wa Bunge la Katiba wanachofanya kwa sasa ni kuweka mpangilio wa shughuli za Bunge ili zikamilike ndani ya siku 60 zilizoongezwa na Rais Jakaya Kikwete, kwa ajili ya kukamilisha kazi ya kuandika Katiba Mpya itakayopigiwa kura ya maoni na wananchi.

Aprili 16, mwaka huu, UKAWA wenye wajumbe takriban 200 wakiongozwa na Profesa Ibrahim Lipumba walisusia vikao vya Bunge la Katiba kwa madai kwamba, kuna mpango wa kuvuruga mapendekezo ya Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Katika ushawishi wake kwa wenzake, Lipumba akiwa ndani ya ukumbi wa Bunge siku hiyo saa 10:31 jioni, alisema: “UKAWA hatuwezi kuendelea kushiriki dhuluma dhidi ya wananchi kwa kupitisha Katiba ambayo ni kinyume cha matakwa yao.”
 
Makala hii imenukuliwa   kutoka kwenye gazeti la RAIA MWEMA "Mgongano UKAWA"

Post a Comment

0 Comments