Ticker

10/recent/ticker-posts

Waziri Makamba na Africa50 Wajadili namna ya kushirikiana katika miradi ya Maendeleo

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba (MP) amefanya mazungumzo na Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Africa50, Bw. Alain Ebobisse, katika ofisi  za Wizara, Mtumba jijini Dodoma. 

 

Mazungumzo hayo yalijikita kujadili namna bora ya kushirikiana katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini ikiwemo ujenzi wa miundombinu na miradi ya mazingira. Baadhi ya miradi iliyojadiliwa ni pamoja na mradi wa kusambaza umeme, ujenzi wa bandari jumuishi ya Mangapwani na usambazaji wa gesi jijini Dar es Salaam.

 

Bwana Ebobisse ameeleza kuwa Africa50 inaiona Tanzania kuwa sehemu sahihi ya uwekezaji kutokana na mazingira mazuri yaliyowezeshwa kwa sera na sheria rafiki, hivyo imehamasika kuwekeza nchini katika miradi ya maendeleo ili kuunga mkono jitihada za serikali za kuwaletea wananchi wake maendeleo. 

 

Waziri Makamba kwa upande wake ameeleza kuwa Serikali chini ya Uongozi imara wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatilia mkazo wa ushirikishwaji wa Sekta Binafsi katika kuendesha miradi mbalimbali ya maendeleo nchini. Ameongeza kuwa imani hiyo kwa sekta binafsi imeongeza mwitikio wa makampuni binafsi kutoka ndani na nje ya nchi kushirikiana na serikali katika kuendeleza na kuendesha miradi mbalimbali ya maendeleo. 

 

Africa50 ni taasisi ya kifedha yenye Makao Makuu yake  Casablanca, Morocco ambayo imejikita katika nyanja mbili za uwekezaji ambazo ni; Maendeleo ya Miradi  na Fedha za Mradi (Project Development and Project Finance) ikiwa na lengo la kuchagiza maendeleo ya miundombinu barani Afrika kwa kuzingatia umuhimu wa mchango wa mradi husika kitaifa na kikanda.

 

Tanzania ilijiunga na Afrika50 tarehe 14 Februari, 2023, kwa kusaini Mkataba wa Hisa za Usajili. 

 

Katika hatua nyingine Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Australia Mhe. Tim Watts MP. 

 

Mazungumzo hayo yameangazia masuala mbalimbali kuhusu ushirikiano wa Tanzania na Australia na Kimataifa hususan yanayolenga kutatua changamoto za amani na usalama miongoni mwa nchi wanachama wa jumuiya ya madola.

Post a Comment

0 Comments