Ticker

10/recent/ticker-posts

Ndege Tatu za abiria zatengenezwa mkoani Morogoro,Zione hizi hapa

 

Tayari ndege tatu zimeunganishwa katika kiwanda cha kuunganisha na kutengeneza ndege, kilichopo katika uwanja wa ndege wa Mkoa wa Morogoro ambacho kilianza kazi mwaka 2021.

Kiwanda hicho cha kwanza Afrika kinachomilikiwa na kampuni ya Airplane Africa Limited (AAL) kutoka Jamhuri ya Czech, kimefanikiwa kuunganisha ndege hizo zenye uwezo wa kubeba abiria wawili hadi wanne.

Akizungumzia na waandishi wa habari leo Machi 18, 2024 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (TAA), Mussa Mbura amesema hatua hiyo, ni sehemu ya mafanikio ya Serikali katika sekta ya usafiri wa anga na uwekezaji kwa ujumla.

Mbura amesema ndege hizo aina ya Skyleader zinatengenezwa Tanzania kwa mara ya kwanza, huku uwekezaji huo ukifungua fursa ya mapato kwa Serikali na hata ajira kwa Watanzania.

“Hivi karibuni uunganishwaji wa ndege zingine utaongezeka, ndege moja iliwahi kubebwa ikaletwa kwenye maonyesho ya viwanda sabasaba. Kiwanda hiki Afrika kipo Morogoro tu na ulimwengu mzima kina matawi manne katika nchi za Czech, Ujerumani, China na Urusi,” amebainisha.

Mwaka jana Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Profesa Godius Kahyrara alitembelea kiwanda hicho kujionea maendeleo, ambapo alisema ni faida kwa nchi kwani mafundi wengi katika kampuni hiyo wamesoma Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT).

Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Mhandisi Igor Stratl amesema wamevutiwa kuwekeza Tanzania kwa sababu ni nchi yenye usalama, utulivu na amani.

(Imeandikwa na Sute Kamwelwe)

Post a Comment

0 Comments