Ticker

10/recent/ticker-posts

Djuma Shaban afunguka kusepa Yanga "Simba waliniambia nimrudishie Hersi pesa zake"

Beki wa kulia Djuma Shaban kwa sasa yupo huru akisubiri kusajiliwa wakati wa dirisha dogo la usajili baada ya kuachana na Yanga msimu uliopita.

Djuma, raia wa DR Congo kwa mara ya kwanza kuja kucheza soka nchini aliletwa na Yanga aliyoitumikia kwa misimu miwili ambayo ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

Hata hivyo, beki huyo anaonekana kufanya mazoezi na matajiri wa soka nchini, Azam FC huku kukiwepo tetesi za kujiunga na timu hiyo ambapo kwenye mahojiano aliyofanya na Mwanaspoti beki huyo wa kulia anaelezea mambo mbalimbali katika soka.

YEYE NA DIARRA

Djuma anasema licha ya kuwa na marafiki wengi ndani ya Yanga, lakini wakati anaichezea alimudu kuwa karibu zaidi na kipa Djigui Diara.

“Napenda kuwa sawa na mtu yeyote, lakini mara nyingi nilikuwa karibu sana na Diarra. Tulijikuta tunakuwa karibu nikiwa kule (Yanga) lakini sasa tunaonana mara mojamoja kutokana na majukumu na utofauti wa timu,” anasema.

“Kwa wachezaji wa hapa Tanzania nilikuwa karibu na Mauya (Zawadi). Nilipenda tu alivyo mtu mzuri. Mpole mwenye ushirikiano hana tatizo na mtu yeyote. Anapenda kuona anafanikiwa haina maana kwamba sikuwa na ukaribu na wengine. Hapana, ila hawa wawili waliwazidi wengine.”

MSIMU BORA KWAKE

Nyota huyo aliyejizolea sifa katika msimu yote miwili Jangwani, anasema msimu wa kwanza aliufurahia zaidi kikosini. “Ule msimu wangu wa kwanza nikiwa Yanga ndio ulikuwa bora kwangu. Nilicheza nikiwa nafurahi kila kitu nilikiona kipo sawa. Nilifanikiwa kufunga mabao manne na kutoa pasi saba za mabao. Kwangu ulikuwa mwanzo mzuri,” anasema beki huyo.

“Msimu uliofuata haukuwa mzuri maana nilianza kuwa majeruhi mara kwa mara. Ilinitesa sana ukizingatia ulikuwa msimu ambao unakwenda kuamua mkataba wangu. Majeraha yalinifanya kupunguza muda wa kucheza, lakini baadaye nilirudi uwanjani na kuongeza mkataba tena.”

KUONDOKA YANGA

Sakata la nyota huyo kuondoka Yanga baada ya msimu uliopita kumalizika liwaacha baadhi ya mashabiki hawaamini kulikoni?

“Tuliporudi Tanzania kuendelea na mkataba wa mwaka ule ambao tuliongeza kuna mambo yaliibuka. Kulikuwepo tofauti kati ya meneja wetu mimi na Bangala (Yannick) alipotofautiana na uongozi wa Yanga. Yale mambo yalikuwa mazito ikashindikana kupatikana muafaka kwa haraka.

“Mambo yaliyokuwa yanasemwa sitaki kuyaweka wazi ila yalinivunja nguvu na nikaona bora tufikie hatua ya kuachana. Tukakubaliana na uongozi kusitisha mikataba na tukaondoka,” anasema Djuma mwenye uwezo pia wa kucheza kama beki wa kati.

“Baada ya kuachana ugumu ukawa kunipa barua ya kuniacha. Nilikuwa tayari na ofa mbalimbali lakini Yanga hawakutaka kunipa barua yangu. Niliambiwa na watu wangu kwamba walidhani ningekwenda Simba. Hatua ile ilinikosesha kupata timu haraka, nilipopewa barua muda wa usajili ulikuwa umekwisha ndio maana sina timu hadi sasa.”

PENALTI YA FAINALI

Wakati Yanga ikicheza fainali ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita dhidi ya USM Alger ya Algeria, Djuma ndiye aliyefunga bao pekee la ushindi ugenini wakati ambao Yanga ikibakiza hatua chache kuchukua taji na hapa anaeleza ilivyokuwa.

“Tulipopata ile penalti niliona kila mtu amezubaa hakuna ambaye alionyesha kuitaka. Nikaenda kuchukua mpira na kujiandaa kupiga. Wengine walishtuka kuona naamua vile. Nakumbuka kuna mchezaji mwenzangu aliniuliza unataka kupiga, nikamjibu ndio.

“Sikuwa na presha hata kidogo kuhofia nitakosa. Watu hawajui kwamba penalti napiga sana hata kama kuna wakati na kosa, lakini hainivunji moyo wa kusema niogope. Nilijiandaa kiakili kwamba huu mpira lazima niuweke wavuni,” anasema Djuma ambaye ni shabiki wa mwanamuziki Daimond Platnumz.

“Ilikuwa ni penalti muhimu ambayo kama ningekosa nilijua kwamba ningeipunguzia nguvu kubwa timu yangu na mashabiki wetu, lakini nilijua kama nitafunga, basi wapinzani wetu itawapunguza nguvu na kutuogopa na baada ya kutakiwa kupiga na mwamuzi nikafunga.



“Nimecheza fainali nyingi za Afrika. Ile haikuwa ya kwanza nilicheza fainali na Raja, kwa hiyo sikuwa na presha yoyote kwenye mwili wangu nilifurahi kwamba niliisaidia timu yangu wakati huo kupata bao muhimu kwenye mchezo muhimu.”


SIMBA WALIKOSEA

Djuma anafichua kwamba alibakiza hatua chache kutua Simba, lakini makosa madogo yalimfanya rais wa Yanga, Hersi Said kumsajili.


“Tulipokutana na Simba kwenye zile mechi za CAF walivutiwa na uwezo wangu. Tukaanza mazungumzo kidogo kidogo na kukaribia kumalizana kabisa. Tulipofika hapo wakawa kimya kwa muda kidogo. Niliwahi kuwatafuta mara moja wakaniambia nisubiri. Kwa kuwa nilikuwa na klabu yangu sikupata presha hata kama mkataba ulikuwa unakwenda mwisho.


“Baada ya muda mfupi kiongozi wangu wa juu wa klabu akaniambia Yanga wananihitaji. Nikajiandaa kuanza nao mazungumzo ghafla nikaambiwa kingozi wao amekuja Congo kunifuata kuzungumza na mimi. Nikakutana na Hersi wakati huo akiwa bado si kiongozi wa juu wa klabu.

“Tulizungumza na kukubaliana kila kitu. Tukamalizana mara moja. Baada ya hapo nikasubiri kuja kujiunga na timu. Baada ya msimu kumalizika wakati nasubiri kujiunga na Yanga, Simba wakarudi tena wanataka nirudishe fedha za Yanga nikaona siyo jambo zuri. Kwanza niliwaheshimu Yanga kwa kuwa walikuja kunifuata kulekule Congo tofauti na Simba ambao tulikuwa tunaongea kwa simu tu muda mrefu.


ISHU YAKE NA AZAM FC

Baada ya kuondoka Yanga, Djuma alitajwa kukaribia kujiunga na Azam FC ambayo ilionyesha nia ya kumtaka, lakini anaweka wazi kuwa kuchelewa kupata barua ya kuachwa Yanga ndiko kulikomnyima ulaji.

“Bado sijamalizana na Azam, lakini nashukuru baada ya kushindikana kunisajili walinipa fursa ya kufanya nao mazoezi ili nijiweke sawa. Ile barua ilichangia kunichelewesha kujiunga. Azam walipoona ugumu wakaendelea na usajili. Kama ningepata ile barua mapema nadhani sasa ningekuwa ndani ya timu hiyo,” anasema Djuma mwenye kadi nyekundu moja tangu aanze kucheza soka la ushindani akiwa na AS Vita.


ANAUZA MAGARI

Nje ya soka, Djuma anafanya biashara na anaelezea zaidi: “Nafanya biashara ya kuuza magari. Nachukua Dubai na Asia nayauza Congo pale Kishansa. Ni kitu ambacho nakifanya kwa muda mrefu sasa, nimeshakizoea.”


YAO BEKI MZURI


Baada ya Djuma kuondoka Yanga akashuka Muaivory Coast, Yao Akouassi ambapo Mcongo huyo anasema jamaa anajua. “Yao ni beki mzuri. Namjua ila hatukuwahi kukutana. Bahati nzuri amefika na kuzoea haraka ligi ya hapa akifanya vizuri. Napenda jinsi anavyopambana uwanjani, ni beki ambaye atawasaidia kwa namna ambavyo anajituma,” anasema Djuma anayependa kusikiliza zaidi nyimbo za Fally Ipupa anapokuwa amepumzika.


Kila kitu kinatokea kwa ruhusa ya Mungu. Naona haikupangwa nicheze naye Yanga, lakini ukiniuliza itakuwaje kama ningekuwa nashindana naye namba nadhani hapo watu wangemjua Djuma ni nani. Mimi sio beki wa kukubali kushindwa nadhani waliona nilipokuwa pale Yanga, tungeshindana sana kwa kutumia uwezo wangu.”


TATOO SITA

Djuma amechafuka mwilini akiwa na michoro (tattoo) mingi yenye sura tofauti, na hapa anaeleza juu ya hilo:  “Hizi ni tattoo ziko sita. Moja ni ya mama, baba. Nyingine ni watoto wangu wanne. Fally Ipupa na nyingine mbili ambazo ni kama urembo hizi zote nimetumia kama Sh700,000 (kuchorwa),” anasema Djuma anayefahamika pia kwa jina la Soldat ya Bemba alilopewa na mashabiki akiwa AS Vita.