Ticker

10/recent/ticker-posts

MPYA: Yule Jamaa Aliyefunga Ndoa na Wake Watatu Kwa Mpigo Matatani

 

Katavi. Athuman Yengayenga aliyefunga ndoa na wake watatu hivi karibuni mjini Mpanda ameingia matatani baada ya kushindwa kukamilisha kandarasi ya ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa shule ya msingi Mnyagala wilayani Tanganyika.

Yengayenga ni kati ya watu wawili waliochukua kandarasi ya ujenzi wa vyumba 6 vya madarasa na matundu 10 ya vyoo katika shule hiyo, ambapo yeye anajenga vyumba vitatu vya madarasa.

Akizungumza na mwananchi katika ziara ya Katibu Tawala Mkoa wa Katavi Hassan Rugwa, wakati wa ukaguzi miradi ya BOOST wilayani Tanganyika, Yengayenga amesema alipata tenda hiyo kupitia jina la Majaliwa Lusambo.

"Maandalizi ya harusi yangu yamesababisha mradi kutokamilika kwa wakati, niliweka mtu wa kusimamia lakini vifaa vilichelewa kufika site, msimamizi badala ya kutoa taarifa kwa maandishi yeye alitoa kwa mdomo,” amesema na kuongeza;

"Mimi hakunishirikisha, kitu ambacho kilisababisha pia wahusika kutotilia manani, najenga vyumba vitatu na kila kimoja kinagharimu Sh2.4 milioni, nimelipwa nusu yake na zimenisaidia kwenye harusi," amesema.

Aidha amesema alianza kutekeleza mradi huo Mei 15, 2023 na alitakiwa kukamilisha June 30, 2023 na kwamba mpaka sasa amefikia asilimia 60.

"Nipo hatua ya upauaji na upigaji lipu muda nilioongezwa nitakamilisha, nina kikundi shupavu na mimi mwenyewe najenga,"

Akisoma taarifa ya mradi huo Mwenyekiti wa kamati ya ujenzi Mwalimu Kuya Mandago ametaja Changamoto zingine zilizokwamisha mradi huo ni ubovu wa barabara eneo la sentaredio.


"Hali hiyo ilikwamisha usafirishaji wa tofali kutoka kwa mzabuni lakini vyumba 6 vyote tumekamilisha maboma tupo hatua ya upauaji,"

Diwani wa Kata ya Mnyagala Mathias Nyanda amesema licha serikali kupeleka mradi huo, wananchi pia wameanzisha ujenzi wa madarasa mengine ili kupunguza msongamano wa wanafunzi darasani.

"Tunashukru Serikali kwa mradi huu pia kwa nguvu za wananchi tunaongeza madarasa mengine kwasababu mahitaji ni makubwa maana shule ina zaidi ya wanafunzi 2000," amesema Nyanda.


Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi, Hassan Rugwa, baada ya kukagua mradi huo ametoa siku 10 kwa wajenzi wa mradi huo kuhakikisha unakamilika.

"Mkataba ulitaka mkamilishe ujze huu mwezi Juni 30, ili shule zikifunguliwa wanafunzi waanze kutumia madarasa haya, japo hamjachelewa sana, jitahidini mkamilishe katika muda niliowapeni," amesema na kuongeza;

"Majengo mliyoanza kujenga wenyewe, Serikali itaunga mkono, nawapongeza sana kwa ushirikiano wenu wananchi."

Post a Comment

0 Comments