Ticker

10/recent/ticker-posts

ROSE MHANDO ‘ALIPUGWA’ KWA KUBADILI DINI.

Na Moshy Kiyungi,Tabora.

“Mchumia Juani hulia kivulini” msemo huu unajionesha wazi kwa mwimbaji wa nyimbo za injili Rose Mhando, alifukuzwa nyumbani na familia yake, hivi sasa yupo vizuri kimaisha.

Aliwahi kutamka kuwa maisha yake yalianzia katika hali duni sana, alikuwa akiombaomba baada ya kufukuzwa katika familia yake huko Dumila mkoani Morogoro kwa kosa la kubadili dini.

Rose Mhando kabla hajawa mkristo alikuwa Muislam, aliyesoma vyema Koraan.

“Nilikuwa mwimbaji mzuri sana wa Kaswida, nikihudhuria kila siku Madrasa nikiwa Dumila. Baadaye maisha yangu yalikuwa magumu sana, chanzo cha hayo yote ilikuwa ni ugonjwa uliosababisha afya yangu kudhoofu. Nilipimwa kila ugonjwa sikukutwa na tatizo. Ndipo siku nilipoamua kwenda kwenye maombi” alieleza Rose Muhando.

Alimpokea Yesu Kristo pale alipokuwa anaumwa yuko kitandani akiwa na umri wa miaka 9.

Rose alisumbuka na maradhi hayo kwa kipindi cha mitatu, baada ya maombi hayo alipopona aliamua kubadili dini yake na kuwa Mkristo akiwa na umri wa miaka 12.

“Nilipobadili dini, wazazi wangu walichukizwa na uamuzi wangu, waliona ni busara kunifukuza nyumbani, kumbe walizidi kunihatarishia maisha yangu. Niliendelea kutangatanga na baadaye nilipata waume, ambao walinizalisha watoto watatu” anasimulia Rose.


Wasifu wa Rose Mhando unaeleza kuwa alizaliwa mwaka 1976, katika kijiji cha Dumila, wilaya ya Kilosa, Mkoa wa Morogoro.Alianza muziki wa injili katika kwaya iliyoko Dodoma, akawa mwalimu wa Kwaya ya Dodoma St. Mary’s katika Kanisa la Kianglikana la Chimuli.

Rose hutunga na kuimba nyimbo za injili kwa lugha ya Kiswahili, ambaye weledi wake, Januari 31, 2005, alizawadiwa tuzo ya Mtunzi mzuri wa nyimbo, Mwimbaji Bora na Albamu Bora ya mwaka.

Tuzo hizo zilitolewa katika Tamasha Tanzania Gospel Music Awards, 2004.
Rose Desemba 2005, alihudhuria katika Tamasha la Nyimbo za Injili katika kusaidia kuchangia kwa watoto na wajane, jijini Dar es Salaam.

Aidha Februari 2011, alisaini mkataba na Mult Album Recording Deal with sony Music.Hafla ya kusaini mkataba huo, ilitangazwa katika mkutano wa Waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, ikiwa ni mara ya kwanza kufanyika Afrika Mashariki.

Baadhi ya albam za Rose Muhando ni, ‘Mteule uwe macho’ ya mwaka 2004, ‘Kitimutimu’ ya mwaka 2005, ‘Jipange sawasawa’ ya mwaka 2008, ‘Utamu wa Yesu’ ya 2012 na ‘Kamata pindo la Yesu’ ya mwaka 2015.
Tuzo alizopata 2005 Tanzania Music Awards, Best Female Vocalist & Best Religious Song ya ‘Mteule uwe macho’ya mwaka 2009, The Best Tanzanian Gospel Singer Awards, Rose Mhando The Best Singer in Tanzania, Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) lilimtunuku zawadi ya shilini 200, 000 kwa wimbo wa ‘Nibebe’ na mwaka 2008 alipata tuza ya Kenya groove kama msanii bora wa nyimbo za injili Afrika.

Baadaye nguli huyo alitangaza kurudi tena katika dini yake ya Kiislamu, akidai kugundua kuwa ule upendo aliwahi kuambiwa upo katika Ukristo hauoni zaidi ya majonzi na maumivu kila siku.

Habari za Rose Muhando zilisambaa sana kutokana kuwa mwanadada huyo kwa sasa aliyekuwa akinekana kama amechanganyikiwa, amefirisika na hata watoto wake hawana tena mahali pa kuishi. 

Ikumbukwe kwamba Rose alikuwa moja ya wasanii wakubwa sana wa injili huku akisifiwa kila kona ya humu nchini na nje ya mipaka ya Tanzania kwa kazi zake ambazo zikipendwa na kila mtu bila kujali umri wala dini.

Maisha uliyoishi zamani hayawezi kukukwamisha kufikia malengo uliyojiwekea.

Leo hii hakuna mtu ambaye alifikiri Rose Muhando angeweza kuwa mwanamuziki mkubwa wa nyimbo za Injili anayelipwa fedha nyingi kutokana na muziki wake, hasa kwa wale waliomjua tangu utoto wake.

Msanii huyo alisaini mkataba mnono wa miaka mitano na Kampuni ya Sony Music Africa ya Afrika Kusini, alioanza kuutumikia mwaka huu 2014.

Rose Mhando aliendelea kusimulia machungu aliyokuatana nayo wakati akiwa na mtoto wake mchanga akisema:

“Nikiwa na mtoto wa miezi sita niliwahi kufukuzwa na mchungaji mmoja jijini Arusha kwa kuwa tu nilikwenda kumwomba msaada wa fedha kidogo za kurekodi studio. Kitu hicho kiliniuma sana na sitakisahau katika maisha yangu. Kila nikikaa hukumbuka na kuumia sana.”

Alisema kwamba alifika Arusha kwa ajili ya kurekodi wimbo wake wa kwanza, ambapo kutokana na kutokuwa na fedha, aliona ni busara kumuomba msaada mchungaji huyo, lakini ilishindikana.

“Alinifukuza nikiwa na mtoto mchanga aliyekuwa na mgonjwa wa pumu, niliumia sana na hapo ndipo nilipomwambia Mungu nikasema yeye anajua ameniandalia nini kwenye maisha yangu,” anaeleza Rose.

Alisimulia kuwa alianza safari ya kurejea nyumbani, lakini kwa bahati nzuri njiani alikutana na watu wenye asili ya Somalia, akajitambulisha kwao kuwa aliwahi kuwa muumini wa dini ya Kiislamu, nao walimsaidia na kumsafirisha hadi mkoani Morogoro.

Baada ya kufika Morogoro aliendelea na maisha na baadaye alirudi Dodoma ambako alijiunga na kwaya moja mjini humo, wakati huo alikuwa tayari ana watoto watatu, akiwa pia ameshaokoka.

“Nilianza muziki katika kwaya iliyopo Dodoma, baadaye nikawa mwalimu wa kwaya hiyo ya Dodoma St. Mary’s katika Kanisa la Kianglikana la Chimuli. Niliendelea hivyo mpaka nilipoamua kuanza kutunga nyimbo zangu mwenyewe kwa msaada wa mfuko wa kwaya yetu,” anabainisha na kuongeza:

“Januari mwaka 2005, ndipo nilipoanza kuona uwepo wa Mungu, nilipokea tuzo mbalimbali ikiwamo ya Mtunzi Bora wa nyimbo za Injili, Mwimbaji Bora na Albamu Bora ya Mwaka, zilizotolewa na Tanzania Gospel Music Awards 2004.”

Rose Mhando alisema hana furaha katika maisha ya Ukristo tofauti na alivyokuwa akielezwa wakati akihubiriwa kuokoka. Pia Rose aliwaponda baadhi ya wachungaji kwa kumhukumu kwa maneno ya walimwengu bila kutumia hekima za kidini.

“Wakati ninaokoka niliambiwa maneno ya faraja sana kwamba nitakutana na upendo, badala yake nimekuwa nikikutana na matusi kila siku. Mfano mtu anakualika sehemu unashindwa kufika na unatoa taarifa, kesho yake unasikia kuwa anatangaza umemtapeli! Wanashindwa kujua na kukumbuka hata jema moja kutoka kwangu! Nafikiria kurudi kwenye dini yangu ninaamini nitapata faraja” alitamka Rose Mhando kwa uchungu.

Nyota huyo wa nyimbo za injili aliendelea kusimulia eneo fupi la maisha yake magumu ambapo amewahi kutekwa mwanaume mmoja akiwa na bastola, akampeleka msituni ambako alimlazimisha kufanya naye mapenzi, lakini ‘alidunda’.

"Dunia ina mambo mengi sana ndugu zanguni, wengine wema, wengine waovu. Mimi nakumbuka siku moja kuna mwanaume ambaye nilikuwa na ukaribu naye, huyu Bwana ana jina kubwa sana Dodoma.

Alinichukuwa kwenye gari lake kwa ajili ya kunisaidia mambo fulani maana tangu awali alikuwa ananisaidia katika kazi zangu.

"Nilishangaa kumuona anaelekeza gari nje ya mji, nikamuuliza tunakwenda wapi, akasema tulia utajuwa. Sikuwa nimemuwazia ubaya, hivyo nilitulia lakini matokeo yake akanipeleka hadi porini ambako alikutana na watu wengine, nikaamini kuwa walikuwa wasaidizi wake” alisimulia Rose.

Kumbe ulikuwa mpango kabambe, wale watu wakamuweka chini ya ulinzi, wakamfunga kamba kisha wakanioneshea mtutu wa bastola usoni.

Rose huku aliendelea kudai kuwa, mpaka hapo hakuwa amejuwa kisa cha kuwekwa chini ya ulinzi, akaambiwa kuwa, anatakiwa kuwa chini ya himaya ya kimapenzi na mwanaume huyo aliyekuja naye, la sivyo siku zake zilikuwa zinahesabika.

“Niliona ni jambo la ajabu, kwani mwanaume kumtaka mwanamke ni mpaka silaha na kutishia kuua?" alihoji nyota huyo mkubwa wa nyimbo za ijili.

Ili kuyanusuru maisha yake, akatumia mbinu ya kuwa mpole kwa pale akakubali kuwa tayari kuwa mpenzi wake, lakini nikamwambia warudi mjini wakae waongee kwa kirefu. Kwa bahati njema bwana huyo akakubali.

“Tulifika mjini nikiwa najisikia kuumwa sana maana wale wasaizidi wake walikuwa wakinisulubu kwa kunipiga, pia ile kamba niliyofungwa ilichangia kunipa maumivu makali" alilalama Rose.

Mhando alisema walipofika mjini walipanga kukutana ili wayaongee, lakini yeye akakacha kutokea kwenye kikao hicho, badala yake akaenda polisi (hakutaja kituo) ambako alifungua jalada la uchunguzi.

“Nimekuwa nikisita kumwanika kwa jina huyo mwanaume huyo ambaye ni adui yangu mkubwa. Naishi kwa tahadhari kubwa sana, naamini siku nikimtaja ataniua”

"Mbaya zaidi najua mambo yake mengi, mabaya kwa mazuri lakini mabaya ni mengi sana kwani hata wakati ananisaidia kuhusu kazi zangu, alinitenda maovu mengi, nimemwachia Mungu" alisema Rose Mhando.

Akieleza sababu ya kuyaeleza haya katika kipindi hicho, Rose alisema:

"Nimeamua kusema ili moyo wangu uwe mweupe, nimekuwa nikiwaza siku hadi siku kuhusu lile tukio, ni kumbukumbu mbaya sana kwangu, lakini kwa kukiri kwangu huku sasa nitakuwa na amani."
Amani”

Alisema alifungua jarada Polisi, walisema watafanya uchunguzi wa kina lakini hakuwahi kuambiwa walifikia wapi!Rose, alisema kuwa jamaa huyo alishawahi kuanza kuonesha dalili za kunitaka kimapenzi, lakini yeye alimuonesha kuwa hataki, akisisitiza kuwa yeye anataka kazi kwake na si mapenzi.

Rose Mhando hivi sasa anatamba na wimbo ‘Wololo’ alioutoa chini ya kampuni ya Sony Music Africa.


Makala hii inatoa Kongole kwa ujasiri mkubwa kukabiliana na maovu ambayo ungelitendewa.

Makala hii imeandaliwa kwa msaada mkubwa wa mitandao.

Mwandaaji anapatikana kwa namba: 0713331200, 0736331200, 0767331200 na 0784331200.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2ZPdB48
via

Post a Comment

0 Comments