Waziri Jerry Silaa atambulisha Mfumo wa NaPA ,asema Utaboresha Usafiri Nchini namna hii


Na Mwandishi Wetu,  Dodoma.

Mfumo wa kielektroniki wa Anwani za makazi (NaPA) ambao una programu
tumizi yaani ‘Application’ utasaidia kuboresha huduma za usafiri na usalama
wa abiria na madereva ambapo kwa kutumia simu janja madereva wanaweza
kupakua application hiyo itakayowarahisishia kumfikia mteja kwa haraka kwa
kuwa mfumo huo ni wa utambuzi wa maeneo.

Hayo yamezungumzwa na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,
Mhe. Jerry William Silaa (Mb.) Februari 7, 2025 katika Ukumbi wa Mikutano
wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma katika maadhimisho ya Wiki ya Anwani za
Makazi ambapo amezungumza na maafisa usafirishaji wa bodaboda na bajaji
wa Mkoa wa Dodoma.


Waziri Silaa ameuzungumzia mfumo huo wa NaPA ulio chini ya Wizara yake
kuwa ni mfumo unaotumia simu za kiganjani na abiria wanaweza kuita
huduma ya usafiri kwa kuingiza anwani zao za makazi katika mfumo huo, na
maafisa usafirishaji almaarufu kama madereva wanaweza kufika moja kwa
moja kwenye maeneo yao.

“Anwani za Makazi ni muhimu kwa utoaji wa huduma bora za usafiri, kwani
husaidia katika upatikanaji wa maeneo kwa urahisi na usahihi. hata kama ni
mgeni na hauifahamu Dodoma, kwa kutumia mfumo huu wa NaPA utaweza
kumfikia mteja kwa urahisi,”, alisisitiza Waziri Silaa.


Waziri Silaa ametoa rai kwa maafisa usafirishaji kuwa mabalozi wa Mfumo wa
kielektroniki wa Anwani za Makazi kwa kuutangaza na kuutumia katika
shughuli zao za kila siku ili kuboresha huduma kwa kuwa mfumo huu
unatarajiwa kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya usafiri nchini.


Akitoa salamu za Maafisa Usafirishaji, Mwenyekiti wa Umoja Madereva
Pikipiki Dodoma (UMAPIDO), Bw. Marwa Chacha Nyagake, ameishukuru
Serikali ya awamu ya Sita na Rais Samia kwa kufanikisha uundaji wa mfumo
huo, akieleza kuwa faida zake zinaanza kuonekana katika kurahisisha utoaji
wa huduma ikiwemo huduma za usafirishaji.
Previous Post Next Post

نموذج الاتصال