Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa, Novemba 07, 2024, amefanya ziara ya kikazi katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Msalato iliyopo katika Jiji la Dodoma kwa lengo la kukagua utekelezaji wa kampeni ya matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Akiwa shuleni hapo, Mhe. Majaliwa amepata nafasi ya kukagua matumizi ya nishati safi ya kupikia, ambapo shule hiyo inatumia kuni mbadala kupikia (kuni poa).
“Hapa Msalato nimeona kitu kipya kabisa kinaitwa ‘kuni poa’ zinatokana na takataka, takataka hizo zinachakatwa, zinatengenezwa kwa ustadi mzuri inakua kuni, kuni hii haitokani na kukata miti na kuileta hapa jikoni, inatokana na maganda ya miwa, pumba za mahindi, mtama mabua ya mahindi ndio yanayotumika hapa kuanzia mwaka jana”
“Matumizi ya nishati safi ni ubunifu wa Rais wetu, ambaye amebobea kwenye uhifadhi wa mazingira, aliona kukemea watu wasikate miti, wasichome mkaa pekee haitoshi,badala yake tuhamasishe wananchi watumie gesi, umeme na mkaa mbadala” Amesema Mhe. Majaliwa.
Aidha, Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali imeunda kamati ya Kitaifa inayojumuisha taasisi na viongozi wa wizara mbalimbali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Zanzibar, kwa ajili ya kuhamasisha Watanzania kutumia nishati safi, ikilenga taasisi zenye idadi ya watu kuanzia 100 ziachane na matumizi ya nishati chafu kufikia Desemba 2024.
Hata hivyo, Mhe. Majaliwa amesema kuwa, Taifa limeweka Mkakati wa miaka 10 kuanzia mwaka 2023 hadi 2033, angalau 80% ya Watanzania wawe wanatumia gesi, umeme, mkaa mbadala na kuachana na ukataji miti kwa ajili ya mkaa na kuni, huku fursa zikitangazwa kwa wajasiriamali kuuza majiko ya gesi, umeme, mkaa mbadala na kuni poa.