Haya ndiyo Matokeo yanayotokana na Bomba la Mafuta EACOP


📌 *Ni kupitia fursa za Ajira, Kilimo, Biashara, Afya*

📌 *Halmashauri ya Muheza yaeleza inavyonufaika na fidia; ushuru wa huduma*

📌 *Mradi wafikia asilimia 45.5*

Wananchi kutoka mikoa mbalimbali nchini  wanaozunguka Mradi wa ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) linalojengwa kutoka Uganda mpaka Chogoleani mkoani Tanga,  Tanzania wameipongeza Serikali kwa utekelezaji wa mradi huo ambao umeibua fursa mbalimbali ikiwemo za ajira, biashara, kilimo, maji, utunzaji wa Mazingira na umeme.


Wananchi hao wameeleza hayo kwa nyakati tofauti wakati wa ziara ya ukaguzi wa  utekelezaji wa Mradi wa EACOP  katika maeneo mbalimbali nchini iliyojumuisha Waandishi wa Habari na watendaji kutoka Wizara ya Nishati na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).


Mradi huo umewanufaisha baadhi ya wakazi katika mikoa ya Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singinda, Dodoma, Manyara na Tanga ambapo bomba la mafuta linapita huku Watanzania 7,584 wakipata ajira za muda mfupi na muda mrefu.


Mratibu wa kitaifa wa Mradi huo, Asiadi Mrutu amefafanua kuwa, 
"Mradi huu wa EACOP umeajiri makundi mbalimbali ya watu ikiwemo Wanawake wanaoishi eneo la mradi ili  kuwawezesha kiuchumi, kubadilishana uzoefu na kukuza ujuzi wa Vijana wanaofanya kazi katika kambi mbalimbali nchini," 


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Muheza, Dkt. Juma Mhiza ameipongeza Serikali kwa kutekeleza mradi huo ambao umefikia asilimia 45.5 na kueleza kuwa ni chachu ya maendeleo kwa wananchi wa Muheza na maeneo mengine nchini.

Amesema mradi huo ni fursa kwa Wananchi wa Muheza kwani umeongeza mzunguko wa fedha kwenye jamii ambapo Sh. bilioni 5.4 zimelipwa kwenda kwa wananchi ikiwa ni  sehemu ya fidia ya ardhi kwa maeneo yanayopitiwa na mradi. 

Amesema mradi umeongeza mapato ya ndani kwa Halmashauri kupitia tozo na ushuru wa huduma kwa wakandarasi wanaohudumia mradi huo.

Dkt. Mhiza amesema mapato hayo yamewezesha Vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu wenye mahitaji maalum kuboresha afya za lishe kwa makundi maalum ya watoto ili kuepuka utapiamlo kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano.

Afisa Uhusiano wa Jamii kutoka (EACOP), Bi. Anna Samwel amesema mradi huo unashirikiana vyema na jamii kwa kuwajengea uwezo wananchi waliopo karibu na mradi kwa kutoa elimu ikiwemo ya usalama barabarani, afya, utunzaji wa mazingira, uendelezaji wa miradi ya kilimo na shughuli nyingine ikiwemo ulinzi.

Amesema Mradi unakutana mara kwa mara na wanavijiji kupitia  vikao vya maendeleo ili kueleza utekelezaji wake na fursa zilizopo kwenye mradi ikiwemo ajira.

Bi. Anna amesema wafanyakazi wazawa walioajiriwa katika mradi wamenufaika kwa kupata kipato na kusomesha watoto, kuboresha makazi, uendelezaji wa shughuli za kilimo na ufugaji kwenye kaya na jamii.


 

Previous Post Next Post

نموذج الاتصال