Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imetangaza taarifa ya maamuzi ya Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini kuhusu nauli za abiria wa daraja la kawaida kwa Treni ya Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Makutupora.
Kwa mujibu wa Bw. Salum Pazzy, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano LATRA alipotoa taarifa hiyo Juni 10, 2024 katika ofisini za LATRA Mkoa wa Dar es Salaam, amesema kuwa nauli hizo zimepitishwa na Bodi ya Wakurugenzi LATRA kwa kuzingatia umbali wa kilomita. Kwa mfano, kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma ni kilomita 444.0 ambapo nauli yake ni TZS. 15,500/=, na pia zimepatikana baada ya kufanyia kazi maombi yaliyowasilishwa na Shirika la Reli Tanzania (TRC) na taarifa zilizopokelewa kutoka TRC na wadau wengine.
“Nauli hizi ni kwa daraja la kawaida kwa watu wazima na watoto kuanzia umri wa miaka 4 hadi 12 ambapo nauli zitalipwa na abiria kwa kilomita. Nauli itakayolipwa na mtu mzima na mtoto mwenye umri zaidi ya miaka 12 ni TSH. 69.51 kwa kilomita, na mtoto kuanzia kuanzia miaka 4 hadi 12 atalipia TSH 34.76 kwa kilomita. Aidha mtoto mwenye umri chini ya miaka minne (4) hatalipa nauli, hata hivyo, taarifa zao na wasafiri wote zitatunzwa kwenye mfumo wa taarifa za abiria wanaosafiri kila siku,” ameeleza Bw. Pazzy.
Vilevile amebainisha masharti ya kuzingatia kabla ya kuanza kutumika kwa nauli hizo kuwa ni mtoa huduma (TRC) kuwa na leseni ya usafirishaji, kuwa na ithibati ya usalama wa miundombinu ya reli na mabehewa, kutumia mfumo wa utoaji wa tiketi za kielekroni, kuunganisha mfumo wa tiketi za kieletroni na mifumo ya LATRA, kukokotoa malipo na utunzaji taarifa za abiria, nauli iliyolipwa, tiketi za kielektroni zilizotolewa, kodi za Serikali na tozo za kisheria na kuwa na watumishi wa kada muhimu kwa masuala ya ufundi na uendeshaji wa treni ya SGR ikiwa ni pamoja na madereva waliothibitishwa na wahudumu waliosajiliwa na LATRA.
Pia, Bw. Pazzy amesema kuwa, maeneo ya msingi ya kuzingatiwa na mtoa huduma ni pamoja na kuweka mfumo wa usimamizi wa utoaji taarifa kwa wasafiri na mfumo wa ufuatiliaji wa mwenendo wa treni, kuweka nauli za safari ya kituo kwa kituo katika maeneo yanayoonekana na abiria kiurahisi kwa wakati wote, kuhakikisha uwepo wa huduma bora kwa wateja ikiwemo mazingira ya vituo (stesheni), usafi wa mabehewa, chakula na vinywaji, maji safi na salama, mwanga wa kutosha, na kuweka utaratibu wa fidia dhidi ya majanga na upotevu wa mizigo ya abiria na kuzingatia vigezo vya usalama wa mabehewa na miundombinu ya reli kwa mujibu wa Sheria, Kanuni za Taratibu zilizopo.