Ticker

10/recent/ticker-posts

WAZIRI ANGELA KAIRUKI ASHUHUDIA UTIAJI SAINI DMDP AWAMU YA 2,..KUTEKELEZWA KWA BILIONI 800

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Angellah  Kairuki akizungumza na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff katika hafla ya utiaji saini wa mikataba ya mradi wa uendelezaji Jiji la Dar es Salaam awamu ya pili (DMDP 2) iliyofanyika leo Mei 30,2023  jijini Dodoma.

Waziri wa TAMISEMI, Mhe. Angellah Kairuki, na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwigulu L. Nchemba, (Pichani) wameshuhudia utiaji saini wa mikataba ya kusanifu Mradi Uendelezaji wa Mkoa wa Dar es Salaam awamu ya pili (DMDP 2). Mradi huo unaotarajiwa kuanza kutekelezwa Aprili 2024 utagharimu Shilingi Bilioni 800. Mikataba hiyo imesainiwa kati ya Ofisi ya TAMISEMI na Wakandarasi wanaosanifu mradi huo.
Waziri Kairuki amewataka Wakandarasi hao kuzingatia masharti ya mikataba yao na kuhakikisha kuwa hawatakuwa kikwazo kwenye utekelezaji wa mradi huo. Amesisitiza kuwa ofisi yake itahakikisha utekelezaji wa mradi huo unakuwa na mafanikio makubwa na kuepuka dosari zilizojitokeza katika awamu iliyopita.

“Mradi huu unakwenda kutatua kero mbalimbali ikiwamo ujenzi holela wa makazi, miundombinu duni ya usafiri, mabadiliko ya tabia nchi kwa jiji la Dar es Salaam zinazosababisha mafuriko na utupaji taka ngumu ovyo,”amesema Kairuki

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwigulu Nchemba, ameongeza kuwa mradi huu umekuwa kilio kikubwa kwa wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam, ambao wamekuwa wakihoji kuhusu utekelezaji wake katika bajeti mbalimbali.

Maelezo ya mradi huo yaliyotolewa na Mratibu wa miradi ya Benki ya Dunia, Mhandisi Humphrey Kanyenye, yanaonyesha kuwa asilimia 74 ya fedha hizo zitatumika kwenye miundombinu ya barabara, mifereji, maeneo ya wazi, masoko, vituo vya mabasi, na kurekebisha miundombinu ya taka ngumu.

 

Mratibu wa Mradi wa Miradi ya Benki ya Dunia ikiwepo uendelezaji Jiji la Dar es Salaam (DMDP), Mhandisi Humphrey Kanyenye akiwasilisha taarifa ya maandalizi ya utekelezaji wa mradi wa uendelezaji Jiji la Dar es Salaam awamu ya pili (DMDP 2) katika hafla hiyo fupi iliyofanyika leo Mei 30,2023 ukumbi wa Mkapa jijini Dodoma.

Picha ikiwaonyesha wabunge mbalimbali wakiwemo Jerry Sillaa wa Jimbo la Ukonga na Saaashisha Mafuwe ni baadhi ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Taznania walioshuhudia utiaji saini wa mkataba huo unaotarajiwa kuanza hivi karibuni utakaotekelezwa na wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini  (TARURA)

Post a Comment

0 Comments