Ticker

10/recent/ticker-posts

SERIKALI KUPITIA TARURA IMEBORESHA MIUNDOMBINU YA BARABARA DODOMA

 

Mhe. Rosemary Senyamule-Mkuu wa Mkoa wa Dodoma

Sekta ya Miundombinu ya Barabara imeendelea kuimarika kupitia Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) pamoja na TANROADS Mkoa wa Dodoma hasa katika kipindi cha miaka miwili ya Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa na uboreshaji mkubwa wa barabara tofauti na kipindi cha nyuma.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule alipokua akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Mkapa katika muendelezo wa vipindi maalumu vya kutangaza Mafanikio Serikali ya Awamu ya sita kwa TARURA Mkoa wa Dodoma.

Amesema kubwa kwa Mkoa wa Dodoma katika miundombinu ni ujenzi wa Barabara za mzunguko zenye urefu wa kilometa 112 ambapo LOT 1 inatoka Nala-Veyula-Mtumba-Ihumwa yenye urefu wa Km52.3 Ujenzi huu unagharimu Shillingi Milioni 100.84 na LOT 2 yenye urefu wa Km 60 inayotoka Dry pot Ihumwa, Ngo’ngo’na, Matumbulu, Bihawana -Nala, Ujenzi unaogharimu Shillingi Milioni 120.8. Ujenzi wa Barabara za mzunguko utagharimu Shilingi Milioni 221 kwa LOT zote mbili.

“Mradi huu ni wa aina yake barani Afrika tunampongeza sana Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoa fedha za kukamilisha ujenzi wa kilomta 112.3 Km za barabara za mzunguko ndani ya Mkoa wa Dodoma ” amesisitiza Mhe. Senyamule.

Mhandisi Lusako Kilembe - Meneja wa TARURA Mkoa wa Dodoma

Naye Meneja wa TARURA Mkoa wa Dodoma Mhandisi Lusako Kilembe akiongea kwa niaba ya Mtendaji Mkuu TARURA ameelezea Mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Serikali ya awamu ya sita 2021/2022 na 2022/2023 kuwa ni kuongezeka kwa vyanzo vikuu vya fedha kutoka chanzo kimoja hadi vitatu ambavyo ni Bodi ya Mfuko wa Barabara , Fedha za tozo ya Mafuta na Fedha kutoka Serikali Kuu (Central Government) ambazo zimewezesha kufanya matengenezo, ukarabati na uboreshaji wa barabara zilizo chini ya Wakala huo.

“Tumetekeleza sehemu kubwa ya mtandao huu ni ya tabaka la udongo na changarawe ambapo sehemu hii ina jumla ya urefu wa Km 7238.584 sawa  na asilimia 95.99 ya mtandao  wote wa barabara lakini tabaka la zege ni Km 302.356 sawa na asilimia 4.01 tu ya mtandao wote wa barabara” Amesema Mhandisi. Kilembe 

Amesema mwaka 2023 katika Halmashauri za Wilaya ya Chemba , Kondoa Mjini, Kongwa na Mpwapwa umefanyika ujenzi wa barabara za kiwango cha lami, changarawe na zege pamoja na Madaraja kwenye Wilaya ya Bahi.

 Amesema katika  utekelezaji wa miradi ya barabara kwa mwaka wa fedha 2022/2023 kiasi cha shillingi Billioni 8 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara za nyongeza za mji wa Serikali na fedha maalumu kiasi cha shillingi Billioni 5 kwa ajili ya ujenzi wa barabara katika eneo la Nala viwandani Km 5.

Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA )katika Mkoa wa Dodoma imejipanga kuhakikisha kuwa miradi inayotekelezwa inakamilika kwa kufanya ufutiliaji wa karibu ili kazi zifanyike kwa ubora na kuleta thamani iliyo kusudiwa na kuhakikisha Barabara zinapitikana wakati wote.

Post a Comment

0 Comments