Ticker

10/recent/ticker-posts

NINI MAANA YA DIPLOMASIA YA UCHUMI NDANI YA SIKU 365 ZA MHE.RAIS SAMIA SULUHU HASSAN?SOMA HAPA


Na  Shabani Shabani

Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amekuwa akiishi Sera ya Diplomasia ya Kiuchumi. Tangu kuapishwa kwake kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 19 Machi 2021  amekuwa akifanya ziara mbalimbali ambazo zimeendelea kujenga na kuboresha mahusiano baina ya Nchi yetu na Nchi zingine na eneo mahususi ni katika Diplomasia ya Uchumi. 

Makala hii inaangazia mafanikio makubwa ambayo kama Nchi tunapaswa kujivunia katika Mwaka mmoja wa Mhe. Samia Suluhu Hassan katika nyanja ya Diplomasia ya Kiuchumi. 

Kwa mujibu wa Profesa Kishan Rana (2007) Mbobezi wa masuala ya Diplomasia kutokea Nchini India ameeleza  kuwa Diplomasia ya uchumi ni mchakato ambao Nchi hushirikiana na dunia ya nje, ili kujiongezea faida katika maeneo ya kibiashara, uwekezaji na aina nyingine ya mafanikio ya kiuchumi. Inaweza kuwa mahusiano kati ya Nchi na Nchi, Nchi Kikanda, na Nchi na Mashirika ya Kimataifa. 

Kuna msemo wa waswahili usemao “Mtembea bure sio sawa na mkaa bure” au ule mwingine usemao “Mguu wa kutoka una baraka”. Mhe. Rais Samia amefanya ziara katika Nchi mbalimbali Duniani ikiwemo Uganda, Rwanda, Burundi, Kenya, Ufaransa na Ubelgiji pamoja na Marekani ambapo alihutubia Mkutano wa Baraza la Umoja wa Kimataifa. Zipo faida nyingi sana za Mhe. Rais kufanya ziara katika Nchi mbalimbali kama alivyosisitiza mwenyewe mara kadhaa kuwa  “ziara hizi zinafungua Nchi”. Ni kweli ziara hizi zinafungua Nchi sana. 

Mwalimu Nyerere aliwahi kusema “Kitu kimoja tunapaswa kujivunia ni kuwa sisi ni Wananchi wa Dunia, na Nchi yetu ni Nchi uhuru lakini ni sehemu ya Dunia” , kwa maana ya kwamba upo umuhimu mkubwa wa mashirikiano kati ya Nchi yetu na Nchi zingine katika kudumisha hilo Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akifanya juhudi kubwa sana katika kuimarisha mahusiano kati ya Tanzania na Nchi zingine pamoja na taasisi za kifedha duniani, ndani ya siku 365 ameshafanya mikutano 12 kwa njia ya mtandao na Viongozi mbalimbali wa Nchi zingine pamoja taasisi za kimataifa, ikiwemo Rais wa China Mhe. Xi Jinping, Waziri wa mambo ya nje wa Marekeni Mhe. Antony Blinken, aliyekuwa Kansela wa Ujeruman Mhe. Angela Merkel, Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Mhe. Dkt. Adesina Akinumwi na Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Kimataifa kupambana na ugonjwa wa UKIMWI, Kifua kikuu na Malaria Bwana Peter Sands, na  Viongozi wengine amekuwa akikutana  nao ana kwa ana  hapa kwetu Tanzania na amefanya ziara 14 nje ya Nchi kati ya hizo 2 ni za Bara la Ulaya, moja Amerika na moja Bara la Asia.

Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali za Ikulu Mawasiliano Mhe. Rais amekuwa akiweka mkazo  mahusiano yetu kati ya Nchi na Nchi au na mashirika ya kimataifa kushirikiana nayo katika maeneo ya kukuza uchumi wa Nchi, kushirikiana katika fursa zinazopatikana kwetu na kwao na kuvutia wawekezaji. Juhudi hizo za Mhe. Rais zimeimarisha sana mahusiano kati ya Tanzania na nchi zingine pamoja na taasisi za kifedha, ni mafanikio makubwa. 

Yafuatayo ni mafanikio kwa uchache kati ya mengi katika uwanda wa diplomasia ya uchumi ambayo yamepatikana katika kipindi cha mwaka mmoja wa Mhe. Samia Suluhu Hassan. 

Kupatikana kwa pesa za Msaada: Suala la  Nchi kupokea misaada kutoka kwa nchi zingine ni la muda mrefu na sio geni, Mwaka 1945 baada ya Vita ya pili ya Dunia Nchi nyingi za Ulaya ziliathirika kiuchumi hivyo ili kurekebisha hali ya Uchumi wao, Nchi hizo zilipokea misaada kutoka kwa Nchi ya Marekani katika mpango uliyojulikana kama Marshall Plan. Katika utafiti wa Profesa Ramiarison Herinjatovo ( 2010) wa Japan  ameeleza misaada kwenye Nchi zinazoendelea zimechangia sana katika kukuza Uchumi wa Nchi hizo. Kwa Taifa linaloendelea kama letu kupewa pesa za misaada sio vibaya kwani ni kichocheo kikubwa cha Uchumi, tunachojivunia  Viongozi wetu wote ikiwemo Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan wamekuwa wawazi katika misaada tunayopokea jambo linaloleta ujasiri kuwa misaada hiyo haina hila yoyote nyuma yake. Na kupokea misaada ni kielelezo kuwa Diplomasia yetu ya Uchumi ina imarika sana.

Mfano ziara ya siku 10 ya Mhe.  Rais Samia Bara la Ulaya, amefanikiwa kupata fedha za msaada kiasi cha Euro milioni 450 sawa na Shilingi trilioni1.17 kutoka Umoja wa Ulaya (EU) pesa hizi ni karibu makusanyo ya mwezi mzima hapa Nchini, na  katika kipindi  cha miaka mitatu ijayo fedha hizo zitatumika kukwamua miradi iliyokwama ya viwanja vya ndege vya Kigoma, Shinyanga na Pemba, ukarabati wa uwanja wa ndege wa Julius Nyerere Dar es Salaam (Terminal II), mafunzo, mradi wa mabasi ya umeme, ukamilishaji wa mradi wa mabasi ya mwendo wa haraka na kilimo, hii itachochea maendelea ya mtu mmoja mmoja na Nchi yote kwa ujumla. Misaada ni mizuri haswa ikitumika vizuri kama inavyofanyika sasa. 

Kuondoka kwa vikwazo vya kibiashara: Ziara za Mhe. Rais zimekuwa na mafanikio makubwa katika kuondoa vikwazo vya kibiashara kati ya Nchi yetu na Nchi zingine Mfano mzuri ni ziara ya Mhe. Rais katika Jamhuri ya Kenya Mei 2021  imepelekea Tanzania na Kenya kutiliana Mikataba ya Kibiashara na kuondoa vikwazo vya kibiashara vilivyokuwepo, ikiwemo mahindi kutoka Tanzania yaliyokuwa yamezuiliwa mpakani mwa Kenya kuruhusiwa kuingia Kenya. Aidha,  umesainiwa  mkataba wa kujenga bomba la gesi kutoka Dar es Salaam hadi Mombasa, hiyo itarahisisha bei ya stima na kusaidia, viwanda  kupata nishati safi. Faida nyingine ni kuwa umeongezeka  uhuru wa  kibiashara kwa wawekezaji wa Tanzania kwa kupata ruhusa ya  kuwekeza nchini Kenya bila kuwa na visa za biashara wala kibali cha kazi ni mafanikio makubwa ya ziara ya Mhe. Rais Samia Samia Suluhu Hassan Nchini  Kenya.

Ujenzi wa miundombinu: Suala la kuunganisha Nchi yetu na Nchi jirani kimiundo mbinu ni matunda ya Diplomasia bora ya Uchumi ya Mhe. Samia Suluhu Hassan mfano Kuimarika kwa mahusiano kati ya Tanzania na Burundi, na kwa kipekee umepelekea makubaliano ya kuharakishwa kwa ujenzi  wa kituo cha huduma za pamoja  kwenye eneo la mpakani la Manyovu Mugina. Aidha Kuendelea kwa makubaliano ya  Ujenzi wa mradi wa bomba la mafuta ghafi wa jumla ya Kilometa 1,443 kutoka Magharibi mwa Uganda mpaka kwenye bandari ya bahari ya Hindi, Tanga. Ni matokeo ya Ziara ya Mhe. Rais Uganda April 2021 Mwaka jana, Nchi hizi zinatarajia  kukuza uchumi na kuzalisha ajira zipatazo 10, 000 wakati wa ujenzi wa bomba hilo na uendeshaji wa mradi huu mkubwa Afrika Mashiriki. Na kuendelea kwa mikakati dhabiti ya kuendeleza mradi wa gesi asili (LNG) wenye thamani karibu shilingi trilion 70 ambapo hadi sasa Serikali imeshasaini mkataba na Kampuni ya Baker Botts, (UK) wa huduma wa ushauri elekezi haya ni mafanikio ya diplomasia ya uchumi. 

Kuvutia wawekezaji: Wawekezaji wanachochea ukuwaji wa Uchumi katika nyanja nyingi na hii inategemeana sana mazingira wezeshi ya uwekezaji wenyewe, mfano ndani ya Mwaka mmoja wa  Mhe. Rais Samia ameonyesha amedhamiria  kuboresha mfumo wa kodi na kupunguza urasimu, mfano mzuri ni mfumo mpya wa Uwasilishaji wa Kodi za Ritani za Ongezeko la Thamani (VAT) unarahisisha uwasilishaji wa kodi hiyo na ukokotoaji wa kodi stahiki,  mfumo wa vibali vya wafanyakazi na upitishwaji wa miradi ya wawekezaji vyote vimeboreshwa haya yote huvutia uwekezaji Nchini. Pamoja na hayo  Ziara za Mhe. Samia Suluhu Hassan zimerudisha imani na kujiamini kwa Wawekezaji wa ndani na wa nje, kwa sababu Mhe. Rais ametamka kwa maneno na ameonyesha kwa vitendo utayari wake wa kutengeneza mazingira rafiki na yanayotabirika ya wawekezaji. Katika kutangaza Nchi yetu,  fursa zake na utayari wa ushirikiano wa Nchi yetu na Nchi zengine kimataifa Mhe. Rais alihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Jukwaa kubwa zaidi Duniani tarehe 21 Septemba 2021, Jukwaa ambalo kwa miaka mitano mfululizo nyuma hatukupata Rais aliyelihutubia, Mhe. Samia alisisitiza kwa kusema “Tunataka Nchi tajiri zitekeleze ahadi zake kwa vitendo”. 

Aidha  Mhe. Rais kashiriki maonyesho ya kibiashara Dubai ambapo Nchi 192 zilishiriki Tanzania ilisaini jumla ya hati za makubaliano ya uwekezaji  37, pamoja na kushiriki mikutano mbalimbali yote hayo yanatoa fursa ya kuitangaza Nchi yetu na  kuvutia wawekezaji. Kwa mujibu wa Waziri wa Uwekezaji Dk. Ashatu Kijaji Serikali ya Mhe. Samia ndani ya mwaka mmoja imesajali miradi ya uwekezaji 294 yenye thamani ya shilingi trilion 18.75. Haya ni mafanikio makubwa ya diplomasia ya uchumi ndani ya mwaka mmoja wa Mhe. Samia Suluhu Hassan

Mwisho, Diplomasia ya uchumi imepelekea Nchi yetu kupata madarasa 15,000 ndani ya kipindi cha miezi mitatu, ununuzi wa magari ya wagonjwa ya kisasa 20 na 365 ya kawaida, ununuzi wa mashine za X Ray 85, madawati 462,795, kumalizia vyuo vya VETA 32, magari 25 ya kuchimba visima vya maji, mitambo 5 ya kujenga mabwawa ya maji  na  kadhalika. Ukweli ndani ya mwaka mmoja wa Mhe. Samia Suluhu Hassan ameonyesha utayari mkubwa katika kuitumia diploamsia ya uchumi kukuza uchumi wa Nchi yetu ni vyema sasa Watanzania tukamuuga Mkono na wale wanaofanya shughuli mbalimbali ikiwemo biashara, kilimo na uwekezaji  kuona hii ndio fursa sasa ya kutanua wigo wa shughuli zao Kimataifa ili kuendelea kupata faida zaidi wao na Nchi yetu na kutangaza zaidi Nchi yetu Kimataifa..

 Kazi iendelee. 

Shabani Shabani Hamimu

Afisa CCM – Makao Makuu

Mawasiliano: 0672869090

Barua pepe: shabanishabani3@gmail.com


Chapisha Maoni

0 Maoni