UBORESHAJI WA DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA JIJINI DAR, PWANI KUFANYIKA FEBRUARI 14 HADI 20, 2020

  Masama Blog      
Na Leandra Gabriel, Michuzi TV
UBORESHAJI wa daftari la kudumu kwa mkoa wa Dar es Salaam na Pwani unatarajiwa kufanyika kwa siku saba, kuanzia Februari 14 hadi 20 mwaka huu na hiyo ni baada ya kukamilika kwa zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu kwa Mikoa yote ya Tanzania bara na Mkoa mitano ya visiwani Zanzibar.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano ulioikutanisha tume ya Taifa ya uchaguzi na wadau wa uchaguzi wa Mkoa wa Dar es Salaam Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi nchini, Jaji Semistocles Kaijage amesema kuwa maandalizi kwa ajili ya zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura katika mikoa hiyo umekamilika na kuwataka wale wote wenye sifa kutumia haki yao ya kikatiba kwa kujiandikisha ili kuweza kushiriki katika katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka huu.

Amesema kuwa uboreshaji wa daftari la kudumu hautahusisha wapiga kura wote walioandikishwa kwenye daftari la kudumu la wapiga kura mwaka 2015.

"Uboreshaji huu unawahusu wapiga kura wapya ambao wametimiza miaka 18 na wale ambao watatimiza umri wa miaka 18 siku ya uchaguzi mkuu mwaka huu." Ameeleza.

Aidha amesema kuwa kwa wale ambao wamehama kutoka maeneo yao ya awali na kuhamia maeneo mengine, wenye kadi zilizoharibika au kupotea na wale wanaotakiwa kuondolewa kwenye daftari kwa sababu za kufariki au kupoteza sifa watahusika katika maboresho hayo.

Vilevile amesema katika uboreshaji huo Kuna baadhi ya asasi za kiraia ambazo zimepewa vibali vya kutoa elimu kwa mpiga kura kwa ajili ya uboreshaji na kuwashauri wananchi kutumia nafasi hiyo kwa kujifunza kuhusu uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura na amezitaka asasi hizo ambazo zimepewa kibali na tume kutumia mwongozo wa utoaji wa elimu ya mpiga kura uliotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi juu ya uboreshaji wa daftari hilo.

Jaji Kaijage ametoa rai kwa wananchi wote kutunza kadi zao hadi siku ya uchaguzi na hata baada ya uchaguzi kwa kuwa moja ya changamoto kubwa iliyojitokeza katika baadhi ya maeneo yaliyokamilisha mchakato huo ni pamoja na upotevu wa kadi, kadi kuharibika na wananchi kushindwa kukumbuka majina yao hivyo kuchukua muda mrefu katika kutafuta majina yao kwa usahihi.

Pia amesema wananchi wajitokeza mapema na sio kusongamana misururu mirefu kwenye vituo vya kuandikisha wapiga siku za mwisho na kusema kuwa hilo litafanikiwa ikiwa wadau, tume na wananchi watashirikiana katika zoezi zima la uchaguzi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Dkt. Wilson Charles Mahera amesema kuwa wananchi wenye sifa wajitokeze ili kutimiza haki zao za kiraia na kueleza kuwa Tume inatambua mchango wa wadau mbalimbali katika kuleta mabadiliko chanya na mwamko wa kimaendeleo katika jamii yetu.

Amesema kuwa Tume itaendelea kuzingatia Sheria na kanuni zake katika zoezi zima la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura na kuviomba vyama vya siasa na wadau wengine kuzingatia Sheria za uchaguzi, kanuni za uboreshaji na maelekezo kwa vyama vya siasa kuhusu zoezi la uboreshaji.

Mkutano huo umewakutanisha wajumbe wa Tume, viongozi wa vyama vya siasa, dini, Wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam, wawakilishi wa watu wenye ulemavu, wanawake, vijana, asasi za kiraia na wahariri na waandishi wa habari.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi jaji Semistocles Kaijage akizungumza na wadau wa uchaguzi wa Mkoa wa Dar es Salaam wakati wa kupeana taarifa juu ya zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwa Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani utakaoanza mapema mwezi huu, leo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Dkt.  Wilson Charles Mahera akizungumza na wadau wa uchaguzi wa Mkoa wa Dar es Salaam na kuwashauri wananchi kutumia haki yao ya kikatiba ya kushiriki katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka huu, leo jijini Dar es Salaam. 
Baadhi wa wadau wa uchaguzi wakifuatilia mjadala uliowakutanisha na Tume ya Taifa ya Uchaguzi na kujadili namna bora ya kufanikisha zoezi zima la uchaguzi na uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, leo jijini Dar es Salaam.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/38ij7xr
via
logoblog

Thanks for reading UBORESHAJI WA DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA JIJINI DAR, PWANI KUFANYIKA FEBRUARI 14 HADI 20, 2020

Previous
« Prev Post