THBUB,IRELAND KUELIMISHA UMMA KUHUSU HAKI ZA BINADAMU

  Masama Blog      


 Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Paul Sherlock (wa pili kushoto) akijadiliana jambo na Mwenyekiti wa THBUB, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu (katikati) muda mfupi baada ya kikao chao katika ofisi za ubalozi huo jijini Dar es Salaam. Wa kwanza kulia ni   Aran Corrigan, Mtaalamu Mwandamizi wa Jinsia na Utawala Bora wa ubalozi wa Ireland, na wa pili kulia ni Kamishna wa THBUB, Nyanda Shuli. Wa kwanza kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mipango wa THBUB, Laurent Burilo
Mwenyekiti wa THBUB, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu(wa nne kutoka kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Mwenyeji wake Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Paul Sherlock ( wan ne kutoka kulia). Wengine ni Viongozi wa THBUB na Maafisa wa Ubalozi wa Ireland.
Kaimu Katibu Mtendaji wa THBUB, Hajjat Fatuma Muya (wa kwanza kushoto aliyevaa hijab) akieleza jambo katika kikao hicho kilichofanyika katika ofisi za ubalozi wa Ireland.
Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Paul Sherlock (kulia) akimkaribisha  Mwenyekiti wa THBUB, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu (kushoto) muda mfupi baada ya kuwasili katika  ofisi za ubalozi huo jijini Dar es Salaam.
………………………………………………………………………………………….

Na Mbaraka Kambona, 

Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Paul Sherlock  ameonesha nia ya kushirikiana na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) katika kutoa elimu ya kukuza uelewa wa wananchi kuhusu  haki za binadamu na misingi ya utawala bora nchini. 

Sherlock alionesha utayari huo wa kushirikiana na THBUB wakati wa mazungumzo yake na ujumbe wa tume, ulioongozwa na Mwenyekiti wake, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu ulipomtembelea katika ofisi zake jijini Dar es Salaam Februari 13, 2020.

Wakati akijibu  ombi la Mwenyekiti wa tume ambapo alimuomba kuangalia uwezekano wa kushirikiana katika kuelimisha wananchi wa Tanzania kuhusu haki ya ardhi, Balozi alisema kuwa hilo ni jambo zuri na wataangalia uwezekano huo.

Kwa mujibu wa Jaji Mwaimu, maeneo mengi nchini kuna migogoro ya ardhi, huku akitaja baadhi ya maeneo kama ya Kilosa na Kilombero kama mfano wa maeneo yenye migogoro, na kusema kuwa wanawake ndio wahanga wakubwa linapokuja suala la umiliki wa ardhi.

“Nafikiri hilo litakuwa jambo zuri,  tutakaa tuone namna bora tunaweza kushirikiana katika kazi hiyo ambayo ipo katika mamlaka yenu, tutajadiliana na kuona wapi tunaweza kushirikiana”, alisema Sherlock
Akiongea mapema katika kikao hicho, Kamishna wa Tume, Nyanda Shuli alisema kuwa kwa sasa THBUB inapokea malalamiko mengi yanayohusu mafao, watu kuachishwa kazi bila kuzingatia taratibu, upatikanaji wa haki kwa wakati na malalamiko kuhusu migogoro ya ardhi.  

Nyanda alisema kufuatia hali hiyo, THBUB inajipanga kujikita katika kuandaa mbinu zitakazo saidia kutoa majawabu ya matatizo hayo.
“ katika utatuzi wa migogoro tume tunahimiza kukaa katika mazungumzo ili kupata ufumbuzi, sisi tunaamini katika kuleta watu pamoja na kuzungumza kuhusu matatizo yao na kuyapatia ufumbuzi”, alisema Shuli

Kaimu katibu Mtendaji wa THBUB, Hajjat Fatuma Muya alieleza katika kikao hicho kuwa tume imekuwa ikifanya kwa karibu na taasisi mbalimbali za ndani na za kimataifa likiwemo Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).

Aidha, Muya alisema kuwa tume imeingia mkataba wa ushirikiano na AZAKI ishirini na moja (21) nchini kwa lengo la kuunganisha nguvu ili kuhakikisha haki za binadamu zinalindwa, zinakuzwa na kuheshimiwa.

Aliendelea kueleza kuwa kupitia ushirikiano huo, hivi Karibuni THBUB kwa kushirikiana na taasisi ya Haki Maendelea walitoa mafunzo ya haki za binadamu na misingi ya utawala bora kwa Madiwani ishirini na saba (27) wa Halmashauri ya Mkoa wa Lindi.

Ziara ya THBUB katika ubalozi wa Ireland ililenga katika kujenga mahusiano na na kutafuta ushirikiano wa kikazi kwa muelekeo wa kuhakikisha kuwa haki za binadamu na misingi ya utawala bora inatunzwa na kuheshimiwa nchini.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/320RWEY
via
logoblog

Thanks for reading THBUB,IRELAND KUELIMISHA UMMA KUHUSU HAKI ZA BINADAMU

Previous
« Prev Post