PROGRAMU YA ELIMU HAINA MWISHO KUWANUFAISHA WANAWAKE VIJANA ZAIDI YA 2,000 WALIOKATISHWA MASOMO

  Masama Blog      

Na Leandra Gabriel, Michuzi TV
PROGRAMU ya "Elimu haina mwisho" inayotekelezwa na Shirika lisilo la kiserikali la Karibu Tanzania Organization (KTO) kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia vyuo vya maendeleo ya wananchi (FDCs) inataraji kuwafikia wanawake vijana zaidi ya 2,100 waliokatishwa masomo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ndoa za utotoni, mimba za utotoni, ukeketaji na hali duni ya kimaisha huku ikielezwa kuwa programu hiyo itakayoanza mapema Februari mwaka huu itawafikia wanawake vijana na kuwakomboa kiuchumi na kifikra.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa ufungaji wa warsha ya siku mbili iliyotolewa kwa walimu na waratibu wa mafunzo hayo  Mkurugenzi wa taasisi ya KTO; Maggid Mjengwa amesema kuwa, wamekuwa wakishirikiana na serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia katika kujibu changamoto mbalimbali za kijamii kupitia vyuo vya maendeleo ya wananchi vilivyopo kote nchini.

"Kwa kushirikiana na Wizara husika pamoja na wadau wa elimu na washirika wa maendeleo tumekuwa pamoja katika Kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma katika kuyafikia malengo haya na hii ni pamoja na lile la kuwa nchi ya uchumi wa kati na viwanda" ameeleza.

Amesema kuwa Programu hiyo inalenga kutoa maarifa na ujuzi kwa wanawake vijana na hiyo ni kwa kutoa mafunzo ya sekondari, elimu ya ufundi, ujasiriamali na stadi za maisha kupitia vyuo vya maendeleo ya wananchi;

"Vyuo hivi vilianzishwa mwaka 1975  kwa mawazo ya baba wa taifa na vimekuwa chachu ya maendeleo  kwa kuwa vimekuwa vikitoa mafunzo nje ya mfumo rasmi kulingana na mahitaji ya wakati na eneo husika" amesema.

Aidha amesema kuwa vyuo hivyo vinatoa mafunzo kwa kila mwananchi bila kujali itikadi wala dini na kubwa zaidi na la kujivunia ni kuwa Tanzania ni nchi pekee barani Afrika yenye vyuo vya maendeleo ya wananchi ukitoa nchi za Sweden, Finland, Denmark na Norway ambazo hufanya idadi ya nchi tano duniani ambazo zina vyuo vya namna hiyo.

Kwa upande wake mshiriki ambaye pia ni mkuu wa Chuo cha maendeleo ya wananchi Newala Geofrey Nchimbi amesema kuwa Programu hiyo hiyo imekuwa na manufaa makubwa sana na tangu kuanza kwake mwaka 2018 wamewafikia vijana wanawake wengi zaidi;

" Tulikuwa wanufaika wa kwanza wa programu hii, masomo ya sekondari kwa mfumo usio rasmi wanafunzi   (QT) wanafunzi 26 Katia ya 34 walifaulu vyema na kuendele na masomo ya sekondari na wanafunzi nane walioshindwa walipata fursa ya kujifunza fani mbalimbali, ujasiriamali na stadi za maisha ili waweze kujikwamua kiuchumi na kuhudumia vyema watoto wao" Ameeleza Nchimbi.

Amesema kuwa vyuo vya maendeleo ya wananchi 55 vilivyopo katika Mikoa yote nchini vimekuwa vikitoa huduma bora kwa washiriki hasa katika kuboresha mitaala na miundombinu ili kuwawezesha washiriki kunufaika na kutimiza ndoto zao.

Licha ya kushirikiana na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia shirika la KTO pia Wana ushirikiano wa karibu na Shirikisho la mpira nchini (TFF) kupitia programu ya kukuza vipaji kwa vijana wanawake waliopo katika vyuo hivyo.
Mkuu wa chuo cha maendeleo ya wananchi Msinga FDC Miriam Juma akiongoza mjadala katika warsha iliyowakutanisha walimu na waratibu ikiwa ni sehemu ya mkakati wa utekelezaji wa Programu ya Elimu haina mwisho itakayoanza mapema Februari mwaka huu, leo jijini Dar es Salaam.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/31kM1dl
via
logoblog

Thanks for reading PROGRAMU YA ELIMU HAINA MWISHO KUWANUFAISHA WANAWAKE VIJANA ZAIDI YA 2,000 WALIOKATISHWA MASOMO

Previous
« Prev Post