MKURUGENZI MTENDAJI MFUKO WA MAENDELEO YA JAMII AANIKA MAFANIKIO YALIYOPATIKANA KWA KAYA MASIKINI ZILIZOFIKIWA NA MFUKO HUO NCHINI

  Masama Blog      
Na Said Mwishehe, Michuzi Globu ya jamii.

MKURUGENZI Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Ladislaus Mwamanga amesema kuwa programu ya TASAF imetekelezwa katika awamu tatu na imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali katika ngazi ya jamii kwa lengo la kupunguza umasikini kwa msingi wa kutoa huduma za jamii katika sekta zote.

Utekelezaji huo umekuwa ukizingatia mahitaji halisi au kero za wananchi wenyewe kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Serikali na kwamba awamu ya kwanza ya TASAF ilitekelezwa kwa miaka mitano kuanzia mwaka 2000 mpaka mwaka 2005 na ikijumuisha halmashauri 40 za Tanzania Bara pamoja na Unguja na Pemba kwa upande wa Tanzania Zanzibar na kwamba jumla ya miradi 1,704 yenye thamani ya Sh.bilioni 72 ilitekelezwa.

Mwamanga ameeleza hayo leo Februari 17 mwaka 2020 mbele ya Rais Dk.John Magufuli wakati wa uzinduzi wa kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya mpango wa kunusuru kaya masikini wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii(TASAF) ambapo amefafanua uwepo wa mfuko huo umeleta tija kubwa kwa jamii ya Watanzania na hasa katika kaya za watu masikini.

"Awamu ya pil ya TASAF ilianza utekelezaji mwaka 2005 hadi mwaka 2013 na hii ilitekelezwa katika halmashauri 126 za Tanzania Bara na Wilaya zote za Tanzania Zanzibar .Jumla ya miradi 12,347 yenye thamani ya Sh. bilioni 430 ilitekelezwa,"amesema.

Ameongeza kuwa awamu ya tatu ya TASAF ndiyo inayotekelezwa sasa na kwamba utekelezaji wa awamu hiyo ulianza Febrauri mwaka 2013 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2023 na kusisitiza kipindi cha kwanza cha awamu hiyo kimekamilika Desemba 31 mwaka 2019 na leo unazinduliwa kipindi cha pili cha awamu hiyo ya tatu.

Amesema katika kipindi cha kwanza cha awamu ya tatu kiasi cha Sh.trilioni 1.46 kimetumika ambapo utekelezaji wa mpango wa kunusuru kaya masikini umefanyika katika mamlaka za Serikali za mitaa 159 kwa Tanzania Bara na kwa upande wa Zanzibar mpango ulitekelezwa katika wilaya zote.

Amefafanua mbele ya Rais kuwa, utekelezaji wa kipindi cha kwanza cha Awamu ya tatu ya TASAF katika mpango wa kunusuru kaya masikini nchini ulijikita katika maeneo mbalimbali yakiwemo kutoa ruzuku kwa kaya masiniki sana zenye watoto ili ziweze kupata huduma za elimu, afya, na kuimarisha lishe na hivyo kujenga rasilimali watu.

Pia kutoa ajira ya muda kwa kaya masikini zenye watu wenye uwezo wa kufanya kazi wakati wa kipindi cha hari na vipindi vya majanga mbalimbali.Kuongeza kipato kwa kaya maskini kupitia uwekeji akiba na shughuli za kiuchumi ili kuboresha maisha.

Kupitia mfuko huo pia wamekuwa wakijenga na kuboresha miundombinu inayolenga sekta za elimu, afya na maji pamoja na kujenga uwezo katika ngazi zote za utekelezaji.

"Mheshimiwa Rais utekelezaji wa kipindi cha kwanza cha awamu ya tatu ya TASAF katika mpango wa kunusuru kaya masikini kwa kushirikiana na wadau mbalimbali hapa nchini umekuwa na mafanikio makubwa,"amesema.
Ametaja baadhi ya mafanikio hayo ni kwamba zaidi kaya masikini sana milioni 1.1 zenye jumla ya watu 5,296,470 ziliandikishwa kwenye mpango na kupata ruzuku stahiki, wanafunzi 1,805,613 kutoka kaya masikini waliandikishwa shule za msingi, wanafunzi 448,409 shule za sekondari na mwaka 2019 wanafunzi 277 waliomaliza kidato cha sita waliopata mkopo wa bodi ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu na kujiunga na vyuo vikuu mbalimbali nchini.

Pia amesema kaya 253,117 kutoka halmashauri 42 za Tanzania Bara , pia Unguja na Pemba kwa Zanzibar zimeshiriki katika miradi inayotoa ajira za muda.Jumla ya miradi 8,809 yenye thamani ya Sh.bilioni 130 kutoka katika vijiji/Shehia 2,578 iliibuliwa na kutekelezwa na jamii ambapo jumla ya Sh.bilioni 97.5 zimetumika kulipa ujira kwa walengwa walioshiriki kufanya kazi kwenye miradi.

Ametumia nafasi hiyo kueleza kuwa kutokana na utekelezaji wa miradi hiyo, wananchi wmenufaika kwa kupata barabara za vijiji zenye urefu wa kilometa 4,412 , madarasa 100, nyumba za walimu 84, mabweni ya wanafunzi 22, matundu ya vyoo 373, madawati 2,498, zahanati 24, nyumba za watumishi wa afya 19, mifereji ya umwagiliaji yenye urefu wa mita 66,253 , mabwawa ya maji yenye ujazo wa mita milioni 34 kwa ajili ya matumizi ya binadamu na mifugo pamoja na uhifadhi wa mazingira na misitu.

"Kupitia baadhi ya miradi ambayo nimeitaja, ni dhahiri kuwa kipindi cha kwanza cha awamu ya tatu ya TASAF kimewezesha kaya masikini kushiriki katika uzalishaji mali na kukuza uwezo wa kukabiliana na majanga ya asili.Mpango umechangia kuounguza umasikini na kuongezeka uwezo wa kaya kumudu mahitaji yake na kuboresha ustawi wa jamii hususani watoto,"amesema.

Amefafanua pamoja na mafanikio hayo ya utekelezaji wa kipindi cha kwanza cha mpango, mapitio yalibaini changamoto kadhaa ikiwemo kaya ambazo hazikuwa na sifa za kuwepo katika mpango na kwamba Serikali ilitoa agizo la kufanya uhakiki kwenye halmashauri zote za Tanzania Bara na Wilaya zote za Tanzania Zanzibar na kuondolewa kwa kaya ambazo hazikuwa na sifa.

"Hivi sasa mikakati thabiti imefanyika ili tatizo la kutambua na kuandikisha kaya hewa lisitokee tena.Tumefanya majaribio ya kutambua na kuandikisha kaya maskini kwa kutumia teknolojia ya mfumo wa dira ya mtandao katika halmashauri tatu.Hivyo tutatumia mfumo huu katika awamu hii ili kudhibiti fedha za mfuko huu,"amesema.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2Hx1NZx
via
logoblog

Thanks for reading MKURUGENZI MTENDAJI MFUKO WA MAENDELEO YA JAMII AANIKA MAFANIKIO YALIYOPATIKANA KWA KAYA MASIKINI ZILIZOFIKIWA NA MFUKO HUO NCHINI

Previous
« Prev Post