KITUO CHA UTAFITI WA KILIMO-SAT WATOA MBINU YA KUKABILIANA NA VIWAVIJESHI KWA KUTUMIA MIMEA

  Masama Blog      
Mwandishi Mussa Juma akiwa ameshika jani na kunusa harufu yake, Jani hilo nalo hutumika kuua wadudu wanaoharibu mimea ya mazao shambani

Meneja wa Kituo cha Utafiti wa kilimo ambacho kinamilikiwa na Shirika la Kilimo Endelevu Tanzania(SAT) Frank Marwa akielezea hatua nne za ukuaji wa viwavijeshi ambaye ni moja ya wadudu waharibifu wa mazao shambani.
Frank Marwa ambaye ni Meneja wa Kituo cha utafiti wa kilimo akiwa ameshika jani la mpapai ambalo nalo hutumika kuua wadudu wa haribifu wa mazao shambani.
Mkurugenzi Mtendaji wa SAT Janeth Maro akiwa ameushika mmea wa bangi pori ambao majani yake hutumika kuulia au kufukuza wadudu waharibifu wa mazao shambani kutokana na harufu ya mmea hu.
Mmoja ya waandishi wa habari za kilimo hai kutoka mkoani Tanga akiwa ameshika moja ya jani ambalo hutumika kwa ajili ya kuua wadudu wavamizi wa mazao. 


Baadhi ya waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini wakiwa kwenye ziara ya kutembelea shamba la Kituo cha utafiti wa kilimo kinachomilikiwa na SAT wilayani Mvomero mkoani Morogoro.Waadishi hao walikuwa kwenye ziara ya mafunzo kuhusu kilimo hai
Meneja wa Kituo cha utafiti wa kilimo akionesha namna ambavyo mazao ya mahindi yalivyoharibiwa na viwavijeshi
Meneja wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo Frank Marwa (katikati)akitoa maelezo ya namna ambavyo wanatumia mikojo ya mifugo waliyonayo kituoni hapo kwa ajili ya kutengeneza dawa za kuulia wadudu waharibifu wa mazao yawapo shambani.


Na Said Mwishehe,Michuzi Globu ya jamii

SHIRIKA la Kilimo Endelevu Tanzania(SAT) limesema ili kukabiliana na wadudu wa haribifu katika mimea ya mazao yakiwemo ya makundi ya viwavijeshi vamizi ni vema Serikali kupitia Wizara ya Kilimo ikaona haja ya kuwa inatoa mafunzo ya mara kwa mara kwa maofisa ugani ili kupata mbinu mpya za kukabiliana na wadudu hao.

Hayo yamesemwa na Meneja wa Kituo cha Utafiti wa kilimo ambacho kinamilikiwa na SAT Frank Marwa wakati akielezea tafiti mbalimbali ambazo zinafanywa na kituo hicho katika kukabiliana na wadudu waharibifu.

"Kuna wadudu ambao wamekuwa wakiharibu mazao mbalimbali na kwa mfano viwavijeshi amekuwa mharibifu mkubwa wa zao la mahindi na akiingia anasababisha hasara kwa mkulima na kupunguza uzalishaji kwa wastani wa asilimia 85, hivyo lazima kuwepo na mkakati wa kukabiliana na wadudu waharibifu,"amesema.

Marwa amesema baadhi ya maofisa ugani wanashindwa kuwadhibiti viwavi jeshi kwa sababu hawana uelewa wa kutosha kuhusu wadudu hao na jinsi ya kuwadhibiti.“Ili kuwadhibiti mapema kwanza ni muhimu kufahamu tabia zao na namna wanavyoanza kushambulia mazao kabla hawajaanza kukomaa. Kwa sababu viwavi jeshi wanapitia hatua nne za ukuaji."

Amesema hatua ya kwanza ni kutaga mayai kuanzia 2,400 hadi 8,000 kwa wiki moja na mayai hayo huyataga chini ya jani la mmea, hivyo ni vigumu mkulima kugundua kwa haraka.Akishataga hayo mayai huyagandisha kwa ute anaoutoa mdomoni kuyafanya mayai kuganda chini ya jani la mmea.

Wakati hatua ya pili mayai hugeuka kuwa lava ambapo huanza kushambulia mahindi kwenye juu kwenye mbelewele kasha kuingia ndani ya mche na katika kipindi hicho mahindi hushambuliwa kwa kasi na endapo majani yakiwa yameliwa kwa maduara makubwa.Hatua hiyo ni ngumu kumdhibiti kwa sababu ameshaanza kukomaa kwa kuwa na ngozi ngumu.

Amefafanua kwenye hatua hiyo hata dawa ikipulizwa inakuwa vigumu mdudu kufa kwasababu ngozi yake inakuwa ngumu na anageuka kuwa buu ambalo linakuwa na gamba gumu ili kwenda hatua ya tatu ya ukuaji na baada ya hapo anageuka kuwa kipepeo ambayo ni hatua ya nne.

"Madhara ya wadudu hao shambani yamekuwa makubwa na kuna haja kwa maofisa ugani kupewa elimu ya kutosha kumtambua namna ya kumdhibiti.Njia rahisi kuwadhibiti viwavi jeshi shambani ni wakiwa kwenye hatua ya kwanza na ya pili kwenye ukuaji lakini baada ya hapo wadudu hao wanakuwa sugu kufa,"amesema.

Marwa amesema wao wamekuwa wakitumia njia za asili kukabiliana na wadudu wa haribifu wa mazao kwani katika kilimo hai hawatumii kemikali za viwandani kuua wadudu.

"Mkulima anatakiwa kuwadhibiti kwa kutumia maji yaliyotokana na mchanganyiko wa unga wa majani ya muarobaini, pilipili, muarovela, mafuta ya kupikia ya alizeti na maji hayo yanyunyuziwe shambani kabla ya mbelewele za mahindi hazijaanza kuchomoza".

Amesema wadudu hao vamizi kwa mara ya kwanza waliingia nchini kwenye miaka ya 2000 na kwa asili wametokea kwenye mataifa ya Amerika Kusini ambapo wamesababisha madhara makubwa kwa wakulima na kuongeza wadudu hao wanashambulia zaidi mahindi, ulezi, ngano,mtama, pamba, mpunga, viazi na tumbaku.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2PqDNvu
via
logoblog

Thanks for reading KITUO CHA UTAFITI WA KILIMO-SAT WATOA MBINU YA KUKABILIANA NA VIWAVIJESHI KWA KUTUMIA MIMEA

Previous
« Prev Post