DKT NCHIMBI AWATWISHA MZIGO TBS NA SIDO

  Masama Blog      

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi


Na John Mapepele

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi amelielekeza Shirika la Viwango nchini (TBS) na Shirika la Viwanda Vidogo nchini (SIDO) kuanzisha mara moja operesheni maalum ya kuwatafuta wamiliki wa viwanda na wazalishaji wakubwa wa mafuta ya alizeti katika Mkoa wa Singida.

Lengo kubwa ni kukagua viwango vya mafuta hayo na kuwaelimisha ili kuhakikisha ubora wa mafuta hayo yaweze kuingia kwenye masoko ya kimataifa hatimaye kuinua uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Dkt. Nchimbi ametoa maelekezo hayo kwenye mafunzo maalum ya kudhibiti ubora wa bidhaa yaliyotolewa na TBS kwa wajasiliamali wa zao la alizeti na asali yaliyofanyika katika ukumbi wa VETA hivi karibuni.

Ambapo pia amelipongeza TBS na SIDO kwa kubuni utaratibu wa kutoa mafunzo hayo nchi nzima huku akiwataka kwenda mbali zaidi kwa kuwa karibu na kufanya tathmini ya mara kwa mara kwa mafunzo wanayoyatoa kwa wajasiliamali na kuchukua hatua stahiki.

Amesema katika dunia ya sasa suala la kuzingatia viwango katika bidhaa zote hususan bidhaa za vyakula kwa binadamu la lazima na la kisheria hivyo mafunzo yanayotolewa na TBS na SIDO lazima yawaguse wahusika ili mafunzo hayo yawe na tija badala ya kuendelea kutoa mafunzo hayo kwa mazoea.

“Inapofika suala la viwango na ubora wa mafuta yetu ya alizeti kwenye Mkoa wetu wa Singida linakuwa siyo suala la kubembelezana tena ili kinachozalishwa kufika salama kwa mlaji” alisisitiza Mkuu wa Mkoa

Amewataka wazalishaji na wamiliki wa viwanda vya alizeti na asali kuondokana na fikra potofu za kuona kuwa TBS ni adui badala yake kujenga ushirikiano wa karibu ili kuhakikisha kuwa wananufaika na huduma zinazotolewa na hatimaye kuboresha bidhaa wanazozizalisha na kupata ushindani kwenye masoko ya ndani na nje ya nchi.

Aidha amesema TBS ni daraja baina ya mzalishaji, soko na mlaji na kuwataka wajasilia mali kuwa karibu ili kutengeneza fursa za biashara zao.

Amesema tafiti nyingi zimeonesha kuwa magonjwa mengi ya binadamu yanatokana na vyakula tunavyokula hivyo udhibiti wa ubora ni jambo lisilokwepeka kwa sasa ili kunusuru vifo ambavyo vingeweza kuepukika.

Akitolea mfano katika kitabu kitakatifu cha Mungu cha Biblia amesema maandiko yanasema hata kabla ya kumuumba binabamu Mwenyezi Mungu alimtengenezea chakula na pia kinasisitiza kuwa mtu asiyefanya kazi na asile hivyo ni muhimu kuangalia chakula tunachokula kwa afya ya mlaji.

Aliongeza kuwa vitabu vyote vitakatifu hakuna sehemu yoyote vinaposema mfanyabiashara awe muongo akawataka wasifanye mchezo na maisha ya binadamu kwa kukiuka viwango ili kupata faida ambapo alisisitiza kwamba baada ya masomo hayo wajasiliamali wote watoke na viapo vya moyoni vya kutenda haki na kuwa na hofu ya Mungu katika utekelezaji wa biashara zao.

Amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli imedhamilia kwenda kwenye safari ya uchumi wa kati wa viwanda kwa kuwashirikisha wajasiliamali wote hapa nchini hivyo kila mjasiliamali ana haki sawa kwenye safari hii ambayo imeshatoa mafanikio makubwa.

Naye Mwalimu Hamis Sudi ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa udhibiti ubora amemshukuru Mkuu wa Mkoa na kumhakikishia usimamizi shirikishi kwenye udhibiti wa ubora kwenye bidhaa zinazotokana na zao la alizeti katika mkoa wa Singida na kwamba operesheni maalum itafanyika ili kuwafikia watengenezaji na wamiliki wa viwanda vya alizeti badala ya kutoa mafunzo kwa wajasiliamali waliofika kuhudhulia mafunzo hayo.

“Mkuu wa Mkoa naomba nikuhakikishie hatujafika hapa Singida kupoteza fedha na muda wa Serikali bali kuwafikia wadau wetu wote ambao tutawafikia na tutaleta taarifa ya utekelezaji katika ofisi yako” aliongeza Sudi.

Mkuu wa Idara ya Uhusiano wa TBS, Rhoida Andusamile amesema Shirika lilianzishwa kwa Sheria ya Bunge – Sheria ya Viwango Na.3 ya mwaka 1975,iliyofanyiwa marekebisho na Sheria Na. 1 ya mwaka 1977.Sheria hiyo ilifutwa na nafasi yake kuchukuliwa na Sheria ya Viwango Na.2 ya mwaka 2009 ambayo ililipa Shirika uwezo mkubwa zaidi wa kutekeleza majukumu yake.


Ameongeza kuwa Shirika lina majukumu mengi kama yalivyoainisha katika Sheria ya Viwango Na.2 ya mwaka 2009, lakini majukumu makuu manne.

Aliyataja mambo hayo ni kuweka viwango vya kitaifa vya bidhaa,huduma na mifumo ya usimamizi wa ubora katika sekta zote kutekeleza viwango vya kitaifa katika sekta za viwanda,biashara na huduma kwa kutumia skimu mbalimbali za udhibiti ubora.

Hata hivyo aliongeza kwamba pamoja na hayo lakini pia upimaji wa bidhaa kwa lengo la kuhakikisha ubora wake,pamoja na uthibitisho wa usahihi wa vipimo vinavyotumika viwandani na kutoa mafunzo kwa wazalishaji pamoja na wafanyakazi katika taasisi na viwanda kuhusiana na uzalishaji wa bidhaa bora,uzalishaji salama na usimamizi wa ubora.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/380dH9l
via
logoblog

Thanks for reading DKT NCHIMBI AWATWISHA MZIGO TBS NA SIDO

Previous
« Prev Post