DKT KALEMANI AZINDUA MATUMIZI YA GESI ASILIA UDSM

  Masama Blog      

 Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (wa tatu kutoka kulia) akisikiliza maelezo ya namna mtambo wa gesi asilia uliopo eneo la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam unavyofanya kazi wakati wa hafla ya uzinduzi wa matumizi ya gesi asilia chuoni hapo, Februari 1, 2020.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani akikagua migahawa iliyounganishiwa gesi asilia iliyopo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na baadhi ya nyumba zilizounganishiwa nishati hiyo katika eneo la Mwenge Mlalakuwa, Februari 1, 2020.

…………………………………………………………

Veronica Simba – Dar es Salaam

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani amezindua matumizi ya gesi asilia katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), leo Februari 1, 2020 ambapo kwa hatua hiyo ya awali, migahawa minne chuoni hapo imeanza kutumia huduma hiyo.

Akizungumza katika hafla hiyo ya uzinduzi, Dkt Kalemani amesema dhamira ya serikali ya kutumia gesi asilia inayopatikana nchini kwa maendeleo ya Taifa iko palepale tofauti na wanavyoamini baadhi ya watu kuwa nishati hiyo haipewi kipaumbele katika matumizi yake.

“Gesi hii tutaendelea kuitumia sambamba na matumizi mengine ya nishati ikiwemo kuzalisha umeme ili kujenga uchumi wa viwanda.”
Akifafanua, Waziri amesema mathalani, takribani asilimia 80 ya gesi inayozalishwa kwa sasa hapa nchini inatumika kuzalisha umeme na kwamba umeme unaozalishwa na gesi asilia kwa Tanzania ni asilimia 57 sawa na megawati 892, akibainisha kuwa huo ni mchango mkubwa sana wa sekta ya nishati kwenye uchumi wa nchi.

Hata hivyo amesema, pamoja na kiasi kikubwa cha gesi kutumika kuzalisha umeme, kiasi kingine kinatumika katika shughuli nyingine mbalimbali ambazo ni pamoja na kuunganisha viwandani, kwenye makazi ya watu na migahawa kwa ajili ya kupikia pamoja na kutumika katika magari.
Katika kuweka msisitizo wa matumizi ya gesi asilia katika magari, Dkt Kalemani ametoa agizo kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati pamoja na watendaji wakuu wa Taasisi zote zilizo chini yake, kuhakikisha magari yote yanayoagizwa kuanzia sasa, yawe ni yale yenye mfumo wa kutumia gesi badala ya petroli na dizeli.

Akizungumzia faida za kutumia gesi asilia kwa shughuli mbalimbali, amesema ni pamoja na utunzaji wa mazingira kutokana na uwepo wa kiasi kidogo cha hewa ya ukaa pamoja na  gharama nafuu kwa mtumiaji ambayo inakadiriwa kuokoa asilimia 40 ikilinganishwa na gharama za aina nyingine za nishati.

Kuhusu mipango ya serikali kusambaza gesi asilia kwa matumizi ya kupikia, Waziri ameeleza kuwa, mpango huo umeanza kutekelezwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Lindi, Mtwara na Pwani na baadaye mikoa mingine pia itafikiwa.

Amekipongeza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa uamuzi wa kutumia gesi asilia na kuvitaka vyuo vingine na taasisi za umma kuiga mfano huo.
Awali, akitoa taarifa ya utangulizi mbele ya Waziri, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Dkt. James Mataragio amesema kuwa uzalishaji wa gesi asilia hapa nchini umefikia wastani wa futi za ujazo milioni 200 kutoka futi za ujazo milioni moja, mwaka 2004 ambapo ndipo uzalishaji wake ulianza rasmi nchini.

Aidha, ameeleza kuwa usambazaji wa gesi asilia unafanywa kupitia wakandarasi binafsi na pia kampuni yake tanzu ya GASCO. “Nia yetu ni kuwafikia walaji wengi kadri iwezekanavyo.”Vilevile, ameongeza kuwa, kwa kutumia gesi asilia, viwanda vilivyopo nchini vinapata umeme wa uhakika tofauti na miaka ya nyuma ambapo kulikuwa na changamoto ya umeme kukatika mara kwa mara kutokana na kutegemea chanzo cha maji ambayo wakati wa kiangazi huadimika.

Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa William Anangisye amesema, kwa kutumia gesi asilia katika maeneo yote isipokuwa uzalishaji wa umeme, Chuo hicho kitaokoa takribani shilingi milioni 479.5 kwa mwaka.

Amesema mradi huo wa kuunganisha gesi asilia chuoni hapo umelenga kuhusisha nyumba za wafanyakazi, migahawa, karakana, maabara za utafiti na kufundishia pamoja na jenereta za dharura.Profesa Anangisye ameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Wizara ya Nishati kwa kutoa fursa ya kupeleka mradi huo wa gesi asilia katika Chuo hicho.

Wengine walioshiriki katika hafla hiyo ni Kamishna wa Petroli na Gesi nchini, Adam Zuberi pamoja na baadhi ya viongozi na wafanyakazi wa Wizara ya Nishati pamoja na TPDC.Sanjari na tukio hilo la uzinduzi wa matumizi ya gesi asilia UDSM, Waziri pia amekagua baadhi ya makazi ambayo yalikwishaunganishiwa nishati hiyo katika maeneo ya Mwenge Mlalakuwa na Mikocheni.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/36TNHeV
via
logoblog

Thanks for reading DKT KALEMANI AZINDUA MATUMIZI YA GESI ASILIA UDSM

Previous
« Prev Post