Benki ya NMB yapiga jeki shule na zahanati Singida.

  Masama Blog      
 Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Kati Nsolo Mlozi (wa pili toka kulia) akikabidhi msaada huo wa vifaa vya ujenzi ikiwemo bati vyenye thamani ya Sh. Milioni 20/= kwa Mkuu wa Wilaya ya Singida Paskasi Mlagiri, kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa shule ya msingi Misuna na Msange, pia zahanati za vijiji vya Mwachambia na Mwakichenche, wilayani Singida. 
Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Kati Nsolo Mlozi (kulia), akivikwa shuka maarufu kama ‘mgolole’ kutoka kwa mwanamke wa jamii ya Kinyaturu mkazi wa kijiji cha Msange, ikiwa ni ishara ya upendo kwa benki hiyo kwa mchango wake kwenye sekta ya elimu wilayani Singida .
 
***********************************
KERO ya kusoma mazingira yasio mazuri kwa wanafunzi zaidi ya 350, wakiwemo wasichana 169 wa kitongoji cha Misuna, kijiji cha Ngimu wilayani Singida, imepatiwa ufumbuzi baada ya jamii kwa kushirikiana na benki ya NMB kujenga miundombinu ya vyumba vya madarasa.
Wananchi hao wameshirikiana na Benki ya NMB kumaliza kero hiyo, kutokana na watoto wao kupata usumbufu wa kutembea mwendo mrefu kila siku kwenda shule na kurudi nyumbani huku mchana kutwa wakilazimika kushinda na njaa.

Wakipokea msaada wa vifaa mbalimbali kutoka Benki ya NMB, baadhi ya wananchi walisema kuwa, kila siku watoto wao walilazimika kutembea mwendo wa kilomita tano kwenda shuleni, na zingine tano kurudi nyumbani, hali iliyozorotesha taaluma yao.

Akikabidhi baadhi ya vifaa hivyo ikiwemo bati, mbao, nondo, misumari, makoa na waya kwa ajili ya ujenzi, meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Kati yenye mikoa ya Dodoma, Singida na Manyara; Nsolo Mlozi, alisema Benki hiyo itaendelea kuunga mkono juhudi za wananchi.

“Benki ya NMB itaendelea kushirikiana na serikali katika kuhakikisha changamoto zote zinazoikabili jamii zinatatuliwa, kipaumbele chetu ni kwenye sekta za elimu na afya”alisema.

Meneja huyo alifafanua kuwa, msaada huo wenye thamani ya Sh. Milioni 20/=, kwa ajili ya shule mbili za msingi na zahanati mbili, ni mwendelezo wa benki hiyo katika kuhakikisha inarejesha faida inayopata, kwa jamii ili itumike kuleta maendeleo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Singida Paskasi Mlagiri, alisema kuwa msaada katika shule hiyo ya Misuna na mingine iliyotolewa kwenye shule ya msingi Msange, zahanati ya kijiji cha Mwakichenche na Mwachambia, ni chachu kwa jamii katika kujiletea maendeleo yao.
Hata hivyo Mkuu huyo wa Wilaya aliwataka wananchi kuendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo yao, ikiwemo ujenzi wa matundu ya vyoo, vyumba vya madarasa, nyumba za walimu, madawati na zahanati.

Aidha mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Singida Eliya Dighah, kwa niaba ya wananchi wa wilaya hiyo,aliishukuru Benki ya NMB kuwekeza kiwango kikubwa cha fedha za maendeleo katika halmashauri hiyo, hali inayojenga imani kwa jamii.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/3b4nsG3
via
logoblog

Thanks for reading Benki ya NMB yapiga jeki shule na zahanati Singida.

Previous
« Prev Post