BAADA YA MBUNGE KUTOA OMBI KWA SERIKALI KURUHUSU BANGI KUWA ZAO LA BIASHARA...MJADALA MKUBWA WAIBUKA NCHINI

  Masama Blog      

Na Mwandishi Wetu, Michuzi Globu ya jamii

MJADALA mkubwa umeendelea kuibuka katika maeneo mbalimbali nchini tangu Mbunge wa Kahama Mjini, Jumanne Kishimba, kuitaka Serikali kuruhusu kilimocha bangi nchini ili wakulima waweze kuchangamkia soko la zao hilo ambalo limepanda kwa kiwango kikubwa duniani kabla halijaporomoka.

Baadhi ya wananchi wameonekana kuunga mkono kauli ya Kishimba ambayo alitoa Bungeni Mjini Dodoma Dodoma madai kuwa mbunge huyo anayo hoja na vema Serikali ikaitafakari Kwa makini na kisha kuruhusu ili wakulima watumbie nafasi ya zao hilo kujipongezea kidato na hasa kwa wale ambao watakuwa wanataka kujihusisha nacho.

Hata hivyo juzi Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Nchini kupitia Kaimu Kamishna Jenerali wa Mamlaka hiyo James Kaji amesema wao hawataruhusu zao hilo kulimwa wala kutumiwa kwani limepigwa marufuku kwa mujibu wa sheria.

Mmoja ya wananchi Shabani Shomari Mkazi wa jijini Dar es Salaam alisema ameufuatilia vizuri mjadala kuhusu bangi iruhusiwe au laa na kwa maoni yake ni mjadala unaohitahi muda wa kutosha sana katika kujadili kwake kwa kuangalia faida na hasara zake.

Hata hivyo wakati anazungumzia kilimo cha bangi, Kishimba alitoa kauli hiyo wakati akitoa mchango wake bungeni jijini Dodoma kuhusu wizara mbili za Wizara ya Kilimo na Wizara ya Viwanda na Biashara.

Alisema ni vizuri sasa bangi yetu ikatumika kwenye masoko ya nje, kwani nchini kuna wazalishaji wazuri zaidi na watu tayari wana utaalamu wa kulima bangi na inaweza kusaidia Wizara ya Afya  kupunguza gharama inazotumia kuagiza dawa kutoka nje.

Kishimba kauli yake hiyo  iliungwa mkono na Spika wa Bunge Job Ndugai, akisema hicho anachochangia Kishimba sio utani, kwani na yeye hivi karibuni alikuwa Canada kwenye mkutano wa maspika wa nchi za Jumuiya ya Madola Duniani na ameliona hilo.

"Bangi ni biashara kubwa kwa Canada... big big business (biashara kubwa kubwa) kwa hiyo mheshimiwa Kishimba anazungumza kitu cha msingi sana wala sio utani, tena linaweza kuwa zao kubwa la biashara likafanya mapinduzi makubwa ya kipato," alisema Spika Ndugai na kuongeza;

"Anachozungumza mheshimiwa Kishimba hazungumzi ili bangi itumike kama tunavyofahamu nchini, tunazungumzia habari ya kilimo cha kuendeshwa chini ya utaratibu wote halafu wanapelekewa wanaohitaji kwa ajili ya kutengeneza dawa za wanyama na binadamu."

Hivyo katika mchango wake Kishimba, alianza kwa kusema mwaka jana alikuja na suala la bangi bungeni na bahati nzuri nchi nyingine  zimeruhusu kilimo hicho.

"Mheshimiwa Spika  mwaka 2015 Bunge lako lilipitisha sheria  kuhusu bangi ambayo ina kifungu cha sheria kinachompa DCIA mamlaka ya kuruhusu ulimaji na usafirishaji wa bangi, mirungi, mikokoa kwa ajili ya matumizi ya tiba," alisema Kishimba.

Alisema bei ya bangi duniani imepanda mara dufu na nchi zote zinazotuzunguka zimesharuhusu kilimo cha bangi. "Naomba mheshimiwa waziri wa Kilimo aje atupe ufafanuzi kwa sababu sheria hii ipo, watu wanaotaka kulima bangi wamuone nani, kwani Sheria hii imetungwa na Bunge hili hili mwaka 2015," alisisitiza.

Alisema waliopiga marufuku bangi ni wazungu miaka ya 1940, lakini wazungu wale wale ndio waliogundua kuwa ndani ya bangi kuna dawa.

"Na sisi wenyewe tunaenda kwenye viwanda vya dawa, je tukiagiza dawa yenye malighafi za bangi tutakuwa tunaagiza kutoka wapi? Na tutathibitisha namna gani?"Alihoji Kishimba.

Wakati akiendelea na mchango wake, alisimama Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Angellah Kairuki akiomba kutoa taarifa.

Alipopewa nafasi na Spika Ngugai, Kairuki alisema anaiona hoja ya Mheshimiwa Kishimba na tayari wao wizarani wamepata wawekezaji  wawili ambao wameonesha nia ya kuwekeza katika kilimo na kuchakata mafuta ya bangi kwa ajili ya matibabu.

"Tunaendelea kulifanyia kazi kama Serikali kwa sababu bado hakuna miongozo kuona kama itakubalika au hapana, na ni hatua zipi na taratibu zipi ziweze kufuatwa," alisema Waziri Kairuki na kuongeza;

"Mheshimiwa mbunge atuachie kama Serikali na mamlaka zinazohusika tuendelee kulichakata pindi litakapokuwa tayari basi majibu yatatolewa."

Baada ya taarifa hiyo, Kishimba aliendelea na mchango wake, huku akisema taarifa yake (Waziri Kairuki) anaiunga mkono. Hata hivyo alisema kwa kuwa duniani bei ya masoko ni bei ya ushindani ni vizuri Serikali ifanye uamuzi huo mapema zaidi.

Wakati akiendelea na mchango wake, alisimama pia Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Kasheku Msukuma  na kuomba kutoa taarifa kwa mzungumzaji na aliporuhusiwa alisema;

"Kwa kuwa Bunge linapotunga sheria kinachofuata ni kanuni, sasa nilikuwa nafikiria waziri (Kairuki) angetuambia kanuni zipo tayari tuanze kulima bangi, kwa maana bangi itaporomoka bei."

Baada ya taarifa hiyo, Kishimba aliruhusiwa kuendelea na mchango wake ambapo alisema anaunga mkono taarifa ya Msukuma, akisema Tanzania kwa Afrika ni nchi ya tatu kwa kulima bangi ya magengo.

"Sasa kama wataruhusu mheshimiwa Spika na sheria kama ilivyo inaweza kutusaidia sana kuongeza mapato na kuondoa magendo," alisema na kuongeza;

"Kwa kuwa waziri wa wizara ya mambo ya ndani ya nchi yupo, atatusaidia sana kama anaweza kutoa msamaha kwa bangi iliyopo hata kwa miezi sita kama anavyotoa msamaha wa silaha, ili wananchi wakawasilisha bangi hiyo polisi, wananchi wakauziana Polisi na TRA watapata pesa inaweza kusaidia mheshimiwa Spika watu wetu wakapata pesa.

Alisema dunia inapobadilika ni lazima  twende haraka sana. Alitoa mfano kuwa Uganda wamepewa dola zaidi ya milioni 500 na EU (Umoja wa Ulaya) kwa ajili ya kilimo cha bangi na wanatoa udongo Malaysia kwa ajili ya kilimo hicho.

"Wakulima wetu wana utaalam wa kulima bangi muda mrefu na kwa kuwa hiyo sheria ipo basi tumuombe mheshimiwa waziri kama miongozo hiyo itapitishwa basi, iwe ni mapema kabla bei haijaporomoka," alisema Kishimba na kuongeza  kwamba bangi kwa sasa ni tiba na Tanzania imekuwa ikiagiza dawa na malighafi kutoka nje ambazo zina bangi.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2vSGCi1
via
logoblog

Thanks for reading BAADA YA MBUNGE KUTOA OMBI KWA SERIKALI KURUHUSU BANGI KUWA ZAO LA BIASHARA...MJADALA MKUBWA WAIBUKA NCHINI

Previous
« Prev Post