Ticker

10/recent/ticker-posts

WAZIRI LUGOLA KUANZA ZIARA MIKOA YA RUVUMA, MTWARA NA LINDI, KESHO JANUARI 9, AWATAKA WANANCHI WAMLETEE KERO MIKUTANO

Na Mwandishi Wetu, MOHA, Dodoma.

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola anatarajia kuanza ziara Januari 9, 2020, katika Mkoa Ruvuma, Mtwara na Lindi kufuatilia masuala ya ulinzi na usalama pamoja na maagizo mbalimbali aliyoyatoa kwa vyombo vilivyopo ndani ya Wizara yake.

Waziri Lugola ataanza ziara hiyo Januari 9, 2020 Mjini Songea Mkoani Ruvuma, Januari 10 Mjini Mtwara na Januari 11 Mjini Lindi, ambapo katika kila Mkoa atapokelewa na mwenyeji wake ambaye ni Mkuu wa Mkoa na kukutana na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa.

Akizungumza na mwandishi wa habari hii, akiwa njiani kuelekea Mkoani Ruvuma, leo, Waziri Lugola alisema katika kila mkoa atafanya mkutano wa hadhara, hivyo anawataka wananchi wenye kero waje kwa wingi ili waweze kutatuliwa kero zao.

“Lengo la ziara hii ni kufuatilia utendaji kazi wa Taasisi zilizopo ndani ya Wizara yangu, na pia kuzungumza na wananchi katika mikutano ya hadhara, ikiwa ni utaratibu ambao nilijiwekea tangu nilipoteuliwa kuiongoza Wizara hii,” alisema Lugola.

Alisema ziara hiyo pia itamwezesha kufuatilia kwa ukaribu zaidi maagizo yake aliyoyatoa kwa vyombo vya ulinzi na usalama ambayo ni dhamana zitolewe saa 24 katika vituo vyote vya polisi nchini, na pia alipiga marufuku tabia ya baadhi ya Polisi kubambikizia kesi wananchi, na pamoja na agizo la pikipiki zote zilizopo vituoni ziondolewe.

“Nitafanya mkutano mkubwa wa hadhara katika Mji wa Songea, Mtwara na Lindi, utaanza saa 10:00 hadi 12:00 jioni, hivyo nawaomba wananchi wa miji hiyo wajitokeze kwa wingi kunisikiliza kile ambacho nimepanga kuwaambia, na pia nitawapa nafasi wananchi waulize maswali bila woga, waniambie kero zao nami nitazitatua katika mkutano huo,” alisema Lugola.

Lugola alisema katika ziara yake aliyoifanya Mikoa ya Kigoma, Kagera, Arusha, Morogoro, Katavi na Rukwa, amegundua wananchi wanakabiliwa na changamoto mbalimbali hivyo hawezi kulala akiwa ofisini, lazima afanye ziara nchi nzima kuwasaidia wananchi kutatua kero zao ambapo wengi wao wakiwalalamikia na baadhi ya Polisi wakiwaonea.

“Napenda kuwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi katika mikutano yangu hiyo, wanapojitokeza itasaidia kusikiliza matatizo yao yanayowakabili, ndio mana nimepanga kufanya ziara kama hizi nchi nzima, hii inasaidia sana kujua matatizo mbalimbali ya wananchi pamoja na kuangalia utendaji kazi wa Taasisi zangu zilizopo ndani ya Wizara hii,” alisema Lugola.

Aliongeza kuwa, Serikali ya Rais Dkt. John Magufuli inawajali wananchi wake ndiyo mana inawafuata mahali walipo, ili wazungumze na Serikali yao uso kwa uso.

Waziri Lugola alisema katika Mikoa yote atakayoitembelea pia atazungumza na Watumishi rai ana askari waliopo ndani ya Wizara yake ambao ni Jeshi la Polisi, Idara ya Uhamiaji, Jeshi la Magereza, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, pamoja na Idara ya Probesheni ambayo jukumu lake kuu ni kupunguza msongamano gerezani na kusimamia wafungwa waliopewa adhabu mbadala na Mahakama au wafungwa waliopata msamaha.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/37Js4Pq
via

Post a Comment

0 Comments