WAZIRI JAFO AZINDUA JENGO LA OFISI ZA ALAT, AWAPONGEZA KUHAMIA MAKAO MAKUU

  Masama Blog      
Charles James, Michuzi TV

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe Selemani Jafo ameipongeza Jumuiya ya Tawala za Mitaa nchini (ALAT) kwa kufanikiwa kujenga jengo la Ofisi zao jijini Dodoma.

Mhe Jafo ametoa pongezi hizo leo jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa ofisi za Jumuiya hiyo na kusema wametii kwa vitendo agizo la Rais Dk John Magufuli la kuifanya Dodoma kuwa Makao Makuu ya Nchi.

Jengo hilo ambalo lilianza kujengwa Septemba 2018 limekamilika tayari kwa kuanza kutumika ambapo limegharimu kiasi cha Shilingi Milioni 121.3 ambazo ni fedha za ndani.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri Jafo ameupongeza uongozi wa ALAT kwa ujenzi huo ambao umeacha historia kwani kabla ya hapo Jumuiya hiyo haikuwahi kumiliki ofisi zao wenyewe na badala yake walikua wamepanga.

" Nimeridhika na ujenzi wa jengo hili, hakika ni mzuri na thamani ya fedha imeonekana, Viongozi mliopo mtakumbukwa kwa hili ambalo mmelifanya. Mmefanya jambo la kihistoria na hii ndio maana ya uongozi ni alama.

Kwa muda mrefu ALAT ilikua ni kichaka cha watu kunufaisha matumbo yao lakini chini ya Mwenyekiti Gullamal Mukadam hata zile Halmashauri zilizokua haziipendi ALAT zitaanza kutoa michango bila kunung'unika," Amesema Mhe Jafo.

Ameipongeza Jumuiya hiyo kwa namna ambavyo imekua ikisimamia miradi ya serikali za mitaa na kuahidi kuwa serikali itaendelea kushirikiana nao katika miradi mbalimbali ambayo imekua ikitekelezwa.

" Serikali za mitaa ndio utu wa mgongo wa Nchi yetu, tutaendelea kupeleka miradi mbalimbali ya kimaendeleo haswa kwenye afya na elimu na tunaamini hatua kubwa za kimaendeleo ya kiuchumi itapigwa kwa ushirikiano uliopo baina ya serikali na ALAT," Amesema Mhe Jafo.

Pia Waziri Jafo amezitaka Halmashauri zote nchini zinazodaiwa na Mabenki mikopo iliyokopwa na madiwani ziyalipe madeni hayo mara moja ili kuepusha Mabenki hayo kuzuia viinua mgongo vya madiwani pindi watakapomaliza muda wao.

" Nafahamu kuna halmashauri hazijalipa madeni ya madiwani wanayodaiwa benki baada ya madiwani wetu kukopa wakitegemea watakuwa wanakatwa kwenye posho zao za kila mwezi.

Ninawaagiza wakurugenzi wa halmashauri zote zinazodaiwa zikiongozwa na halmashauri ya Gairo kulipa madeni hayo mara moja ili kuondoa usumbufu wa kuzuiliwa viinua mgongo vyao madiwani wetu hawa," Amesema Mhe Jafo.

Awali akisoma taarifa ya ujenzi wa jengo hilo, Katibu Mkuu wa ALAT, Elirehema Kaaya amesema kukamilika kwa ujenzi wa jengo lao hilo kutaokoa kiasi cha Sh Milioni Tano kila mwezi walichokua wakitumia kama pango kwenye ofisi zao zilizopo jijini Dar es Salaam.

" Mhe Waziri ujenzi umetumia takribani miaka miwili na tulijenga kwa fedha zetu wenyewe ambapo kiwanja pia kilikua ni chetu na mhandisi ni kutoka Jiji la Dodoma," Amesema Kaaya.

Nae Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Mhe Gulamal Mukadam amesema malengo yao ni kujenga jengo refu la kitega uchumi ambalo litaongezea kipato kikubwa kitakachowawezesha kuzidi kujiendesha wenyewe.

" Tunaipongeza serikali ya awamu ya tano kwa miradi makubwa ya kimaendeleo inayotekelezwa kwenye serikali za mitaa hasa kwenye sekta ya Elimu, afya na miundombinu.

Lengo letu baada ya kukamilika kwa ujenzi huu ni kujenga jengo kubwa la kitega uchumi ili kuendana na Sera ya Rais Magufuli ya kukuza uchumi ambapo tunaamini licha ya kutupatia fedha nyingi litakua msaada pia kwa halmashauri zetu," Amesema Mukadam.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe Selemani Jafo (katikati) akizindua jengo la ofisi za Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT) leo jijini Dodoma. Kulia ni Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Gullam Mukadam.
Mwenyekiti wa ALAT, Gullam Mukadam akizungumza wakati wa uzinduzi wa jengo la ofisi ya Jumuiya hiyo jijini Dodoma.

Wadau mbalimbali wa ALAT wakifuatilia uzinduzi wa jengo la ofisi za Makao Makuu ya Jumuiya hiyo jijini Dodoma leo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe Selemani Jafo akizungumza wakati wa uzinduzi wa jengo la Ofisi za ALAT jijini Dodoma Leo.
Katibu Mkuu wa ALAT, Elirehema Kaaya akisoma taarifa ya jengo hilo mbele ya mgeni rasmi Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Selemani Jafo (hayupo pichani) wakati wa uzinduzi wa jengo la Ofisi za ALAT jijini Dodoma.
Muonekano wa Jengo la Ofisi za Jumuiya ya Tawala za Mitaa lililozinduliwa leo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe Selemani Jafo jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe Selemani Jafo akiwa na viongozi wa serikali na ALAT wakati wa uzinduzi wa jengo la Ofisi za Jumuiya hiyo.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/36CeEE2
via
logoblog

Thanks for reading WAZIRI JAFO AZINDUA JENGO LA OFISI ZA ALAT, AWAPONGEZA KUHAMIA MAKAO MAKUU

Previous
« Prev Post