Ticker

10/recent/ticker-posts

WAUMINI KANISA LA TAG WAJITOLEA UJENZI WA MADARASA KILIMANI SEKONDARI

NA BALTAZAR MASHAKA,Mwanza

WAUMINI wa Kanisa la Tanzania Assemblies Of God (TAG) Kiloleli, wameguswa na changamoto ya uhaba wa vyumba vya madarasa inayoikabili Shule ya Sekondari Kilimani na kuamua kujitolea kuchangia mchanga pamoja na kupanga mawe kabla ya ujenzi kuanza.

Waumini hao wa jinsi zote walijumuika jana kushiriki ujenzi wa miundombinu ya madarasa ili kutatua changamoto hiyo ambapo Mchungaji msaidizi wa Kanisa hilo, Joseph Makala alisema ubinafsi umepunguza uzalendo wa watu kujitolea kufanya shughuli za kijamii.

Alisema kupungua kwa moyo wa uzalendo na kujitolea pamoja na jamii kushindwa kushiriki mambo yanayoihusu kunasababishwa na ubinafsi mkubwa uliopo kwenye maisha ya wanadamu, kila mmoja anajithamini binafsi kuliko moyo wa kuwasaidia wengine wenye shida.

Alisema taasisi yao iliguswa baada ya kuambiwa watoto wanaoanza masomo ya kidato cha kwanza mwaka huu katika Shule ya Kilimani Sekondari hawana mahali pa kuingia kujifunzia kwa sababu ya uhaba wa vyumba vya madarasa usiowiana na idadi kubwa ya wanafunzi .

Mchungaji Makala alisema waliletewa maono hayo na Mkuu wa Shule hiyo, hivyokama taasisi ya dini wakaona washiriki ujenzi wa miundombinu hiyo ili kuwezesha watoto kupata mahali pazuri pa kujifunza kwani sababu wanafahamu wanahitaji kupata elimu wakiwa kwenye mazingira bora.

Makala alieleza baada ya kushikirishwa mioyo yao iliguswa wakaona washiriki kwa sehemu ambayo Mungu atakayowezesha ikizingatiwa taasisi hiyo ya dini ni sehemu ya jamii na inahusika na mahitaji ya jamii bila kujali imani za wanufaika.

“Maandiko katika kitabu cha Methali inazungumza suala elimu kuwa;Usimuache Elimu aende zake.Hivyo tukaona watoto wetu wanahitaji kuwa na mahali pazuri pa kusomea na tuliguswa kama taasisi tukaona ni moja ya tunaoweza kushiriki baraka hizo ili kuhakikisha watoto wetu wanapata mahali pazuri pa kujifunzia, tuna wajibu huo kuwezesha watoto wetu wapate elimu,”alisema Makala.

Kwa mujibu wa mchungaji huyo msaidizi taasisi hiyo imekuwa ikisistiza kama ambavyo Bwana Yesu Kristo alivyotoa maisha yake kwa ajili ya kuokoa maisha ya wengine , vivyo hivyo jamii inawajibu huo na inatakiwa kujua inawajibika kuwasaidia watu wenye mahitaji na yawezekana sababu moyo wa ubinafsi umekuwa mkubwa kuliko wa kusaidia wengine.

Naye Mkuu wa shule hiyo Gerana Majaliwa, alisema wana changamoto kubwa ya miundombinu ya madarasa,ingawa wanazitatua kwa fedha za serikalini huku wakishirikiana na jamii pamoja na taasisi zingine kama Kanisa la TAG kuzipunguza.

Alishukuru jitihada za serikali kuendeleza elimu bure bila malipo lakini pia ushiriki wa wananchi katika kutatua changamoto za shule yao akiwemo Mbunge wa Ilemela Dk. Angeline Mabula,kwa kuwawezesha matofali 8,000,000 na mifuko 51 ya saruji.

“Kipekee hakuna taasisi iliyoakamilika, lazima ishirikiane na zingine wakiweo wananchi, tumeshirikiana na TAG ambao wamefanya kazi lakini pia tunakaribisha makampuni na wadau wengine wa maendeleo ili kusaidia kutatua changamoto na tunaamini ushirikiano huo utawezesha taaluma kukua,”alisema Majaliwa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Wazazi, Joseph Nyanda, alisema ili kutatua changamoto ya uhaba wa madarasa wamepanga kujenga na kukamilisha vyumba vitatu kati ya sita Januari mwaka huu ili kuwezesha wanafunzi wa kidato cha kwanza kupata mahali pa kusomea.

“Watoto wanaoingia kidato cha kwanza mwaka huu ni wengi na hatuna pa kuwaweka sababu vyumba vya madarasa havitoshi, hatuna msaada isipokuwa wazazi kwa kushirikiana na serikali pamoja na taasisi za kijamii na taasisi za dini kama walivyofanya TAG Kiloleli.Pia tulibahatisha mgawo wa matofali 4,000 kutoka kwenye kata lakini tukipata fedha za kujenga boma tutakamilisha mapema na kuwanusuru watoto hao,”alisema.

Aidha, Afisa Mtendaji wa Kata ya Kawekamo, Maarufu Mohamed alisema ujenzi wa miundombinu hiyo ya shule unafanywa kwa nguvu za wananchi na wazazi kuanzia msingi hadi boma kisha halmashauri kupaua na kuezeka ingawa mwitikio wa wananchi ni mdogo ambapo mbunge wa Ilemela amewezesha mifuko 51 ya saruji yenye thamani ya sh. 925,0000.
Shughuli ya kusomba na kupanga mawe ikifanyika kwenye ujenzi wa vyumba vya madarasa ya Shule ya kilimanani Sekondri ikifanywa na waumini wa Kanisa la TAG Kiloleli jana.
Mwalimu wa Taaluma wa Shule ye sekondari Kilimani, Athanas Manyika akiongoza walimu wenzake pamoja na waumini wa Kanisa la TAG Kiloleli, kusawazisha moja ya Msingi wa darasa kati ya sita yanayotarajiwa kujengwa shuleni hapo. Picha zote na Baltazar Mashaka .




from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2F8hhCf
via

Post a Comment

0 Comments