WASHITAKIWA SITA WA KESI YA MAUAJI WALALAMIKIA KUCHELEWA KWA UPELELEZI WA KESI YAO

  Masama Blog      
Na Karama Kenyunko, globu ya jamii.

WASHITAKIWA sita wanaokabiliwa na kesi ya mauaji ya kukusudia ya aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk. Sengondo Mvungi wamelalamikia mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuhusu upelelezi wa kesi yao hiyo  kuchelewa kukamilika.

Hayo yamekuja baada ya Wakili wa Serikali, Faraji Nguka leo Januari 14, 2020 kudai mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi,Vicky Mwaikambo Kuwa Kesi ilipangwa kwa ajili ya kutajwa, upelelezi bado haujakamilika.

Baada ya Wakili Nguka kueleza hayo, mshtakiwa Msigwa Matonya alidai mahakamani hapo kuwa upelelezi wa kesi hiyo ulishakamilika na kwamba Novemba 22,2018  ilikwenda Mahakama Kuu ambapo ilifutwa, lakini siku hiyo hiyo walikamatwa tena na kufunguliwa kesi hiyo hiyo.

Kufuatia hayo, mshtakiwa Msigwa aliiomba mahakama itumie busara kwa kumuita Mkuu wa Upelelelezi wa Mkoa (RCO) na mpelelezi wa Kesi hiyo ili wafike mahakamani kujieleza kwa nini hawakamilishi upelelezi na pia aliomba iwapo itashindwa hilo, iamuru wapelekwe polisi. Kwa kuwa haiwezekani toka mwaka 2013 mpaka sasa upelelezi haujakamilika.

Kwa upande wa mshtakiwa Longishu Losindo aliieleza mahakamani hapo kuwa hadi wanafikia kueleza hayo,wamekwisha kaa muda mrefu Magereza huu ni mwaka wa saba ama wa nane, wanashindwa kuelewa kama mahakama inatoa haki na kwamba hakuna jibu linalotolewa zaidi ya kusema wakamilishe upelelezi..."tunaiomba mahakama kama inauwezo  ifikie maamuzi, kama kufungwa tufungwe" amedai Longishu.

Hata hivyo Hakimu Mwaikambo alisema mahakama inatumia busara na kwamba inasikiliza kesi yenye mamlaka nazo na pia kuhusu ombi lao la kutaka wapelekwe polisi, Hakimu Mwaikambo alisema hana mamlaka ya kisheria kwa lolote hivyo hawezi kuwapeleka Polisi wala kumuita mpelelezi.

Kesi hiyo imeahirishwa mpaka Januari 28, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.

Katika Kesi hiyo  ya mauaji namba 6 ya mwaka 2018, washtakiwa Msigwa Matonya(35), Mianda  Mlewa(45), Paulo Mdonondo(35), Longishu Losindo(34), Juma Kangungu(34) na John Mayunga(60).

 Kwa pamoja wanadaiwa kuwa Novemba 3, mwaka 2013, walifanya kosa hilo la mauaji ya kukusudia  kinyume na kifungu cha 196 cha sheria na kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Ilidaiwa kuwa siku hiyo  ya tukio, katika eneo la Msakuzi Kiswegere  lililopo eneo la Wilaya ya Kinondoni, washtakiwa hao kwa pamoja walimuua kwa kukusudia Dkt. Sengondo Mvungi ambaye alikuwa mjumbe  wa Katiba Mpya.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2TnFVa4
via
logoblog

Thanks for reading WASHITAKIWA SITA WA KESI YA MAUAJI WALALAMIKIA KUCHELEWA KWA UPELELEZI WA KESI YAO

Previous
« Prev Post