WANAOTUHUMIWA KWA MAUAJI YA KUKUSUDIA YA DK. SENGONDO MVUNGI WAMKATAA HAKIMU ANAYESIKILIZA KESI YAO, WADAI HAWANA IMANI NAYE

  Masama Blog      
Na Karama Kenyunko, Globu ya jamii.

WASHTAKIWA sita wanaokabiliwa na kesi ya tuhuma ya mauaji ya kukusudia  ya aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk Sengondo Mvungi wamemkataa Hakimu Victoria Mwaikambo wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu anayesikiliza kesi yao hiyo kwa madai kuwa hawana imani nae.

 Mshtakiwa, Longishu Losingo amewasilisha maombi hayo leo Januari 28, mwaka 2020 wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa, upelelezi bado haujakamilika.

Mapema, Wakili wa Serikali, Ashura Mzava alidai mahakamani hapo kuwa kesi leo ilikuja kwa ajili yankutajwa upelelezi bado haujakamilika hivyo akaomba kesi hiyo iahirishwe na kupangiwa tarehe nyingine.

Baada ya hoja ya Jamhuri ya kuahirishwa kesi, mshtakiwa Longishu alinyoosha kidole na kuomba nafasi ya kuzungumza ndipo aliporuhusiwa na kisha akadai kesi yao ni ya muda mrefu na hakuna kinachoendelea hivyo hawana imani na Hakimu, hivyo aliomba jalada lao lirudishwe kwa Hakimu Mfawidhi kwa ajili ya kupangiwa Hakimu mwingine.

Hata hivyo,  Hakimu Mwaikambo aliwelekeza washtakiwa hao waandike barua  ya kutokuwa na imani na yeye kwa Hakimu Mfawidhi. Kesi hiyo imehirishwa hadi Februari 10, 2020.

Awali mwaka 2018, upelelezi wa kesi hiyo ulikamilika na baadhi ya washtakiwa waliachiwa huru na jalada lilienda Mahakama Kuu kwa ajili ya kusikilizwa ambapo Novemba 11, 2018 kesi hiyo iliondolewa lakini washtakiwa walikamatwa na kurudishwa kituoni na kushtakiwa upya katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni pamoja na Msigwa Matonya (35), Mianda  Mlewa(45), Paulo Mdonondo (35), Juma Kangungu (34) na John Mayunga (60).

Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao kwa pamoja  wanadaiwa kuwa Novemba 3, mwaka 2013, walimuua kwa makusudia Dk. Sengondo Mvungi  huko katika eneo la Msakuzi Kiswegere  wilayani Kinondoni.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2S2mRw6
via
logoblog

Thanks for reading WANAOTUHUMIWA KWA MAUAJI YA KUKUSUDIA YA DK. SENGONDO MVUNGI WAMKATAA HAKIMU ANAYESIKILIZA KESI YAO, WADAI HAWANA IMANI NAYE

Previous
« Prev Post