Wadhamini wa Lissu wahaha kumpata mshtakiwa

  Masama Blog      
Na Karama Kenyunko, Globu ya jamii.


WADHAMINI wa aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu,  wameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa wamemwandikia barua Mwenyekiti wa Chadema,  Freeman Mbowe wakimuomba awasaidie kumleta mshitakiwa Lissu hapa nchini.

Mdhamini Robert Katula ameeleza hayo leo Januari 20, 2020 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba, wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa ambapo amedai,  wamefanya juhudi za kuwasiliana na mshitakiwa ambapo mara ya mwisho aliwaeleza kuwa anawasiliana na Wakili wa chama chake.

Hata hivyo, licha ya wadhamini kudai kuandika barua Mahakama imeendelea kusisitiza kuwa inamuhitaji Lissu mahakamani hapo ili shauri linalomkabili yeye na wenzake wanne liweze kuendelea katika hatua nyingine.

Akiendelea kueleza wakili Katula amedai pamoja na mshtakiwa kuwaeleza hivyo, mpaka leo hawajafanikiwa kupata jibu lolote ndipo walipoamua kumuandikia barua Mbowe ili awasaidie kumleta mshitakiwa huyo nchini ili waweze kumfikisha mahakamani kwani wakati tunamdhamini Lissu hatukujua kama atapigwa risasi na kuondoka hapa nchini,.

"Mheshimiwa, tumemuandikia barua Mwenyekiti wa chama chake ili atusaidie kumleta hapa nchini mshtakiwa na sisi tuweze kumleta mahakamani hivyo tunaomba muda zaidi wa kufatilia majibu ya barua hiyo," ameeleza Katula.

Akijibu hoja hizo, wakili wa Serikali, Sylvia Mitanto alidai kuwa ni jukumu la wadhamini kuhakikisha mtuhumiwa anafika mahakamani na si la mtu mwingine na kwamba wadhamini hao walikubali kumuwekea dhamana mshitakiwa huyo hata kabla ya kuugua na walilidhia asafiri na kuongeza kuwa walikuwa wanajukumu la kujitoa katika nafasi hiyo kabla Lissu hajasafiri.

Baada ya kueleza hayo, Hakimu Simba alisema kuwa suala bado linabaki pale pale kuwa mshitakiwa huyo aletwe mahakamani kwani kupigwa kwake risasi hakumzuii kufika mahakamani na kuhudhuri kesi yake.

"Tunaomba mtuletee mshitakiwa hapa, tena (mdhamini) usije ukafikiri tutakusamehe tunakupa muda mwingine tuletee mtu huyo kabla atujatoa amri nyingine itakayokuwa ngumu zaidi dhidi yenu wadhamini na mshitakiwa mwenyewe," amesema Hakimu Simba.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Februari 20, 2020 na kusisitiza Lissu kufika mahakamani na kwamba dhamana kwa washitakiwa wengine inaendelea.

Mbali na Lissu washitakiwa wengine ni Mkina, Mhariri wa gazeti la Mawio, Jabir Idrisa na Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob.

Lissu na wenzake  wanakabiliwa na mashitaka matano ikiwemo la kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.

Inadaiwa kuwa Januari 12 hadi 14, 2016 katika jiji la Dar es Salaam, washitakiwa watatu, Jabir, Mkina na Lissu, kwa pamoja waliandika na kuchapisha taarifa za uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar’.

Katika mashitaka ya pili, wanadaiwa kuwa Januari 14, 2016 katika jiji la Dar es Salaam, walichapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar.

Mshitakiwa Mehboob anadaiwa kuwa Januari 13,2016 katika jengo la Jamana lililopo Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam, alichapisha gazeti la Mawio lililokua na taarifa za uchochezi.

Inadaiwa mshitakiwa huyo pia alichapisha gazeti hilo bila ya kuwasilisha hati ya sheria ya kiapo kwa Msajili wa Magazeti.

Mbali na mashitaka hayo washitakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kuwa Januari 14, 2016, Dar es Salaam, bila ya kuwa na mamlaka yoyote, waliwatisha na kuwatia hofu wananchi wa Zanzibar wasiweze kuingia kwenye marudio ya Uchaguzi Mkuu.

Septemba 7, 2017, Lissu alishambuliwa kwa risasi akiwa kwenye gari nje ya makazi yake Area D jijini Dodoma akitoka kuhudhuria vikao vya Bunge.
Mwisho


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2ufj4Dm
via
logoblog

Thanks for reading Wadhamini wa Lissu wahaha kumpata mshtakiwa

Previous
« Prev Post