Ticker

10/recent/ticker-posts

Usiku wa manane na Hayati Bill Shankly uwanjani Anfield

Chemba ya Anfield

Usiku wa manane na Hayati Bill Shankly uwanjani Anfield

Charles James, Michuzi TV

USIKU mkubwa. Usiku mnene ndani ya uwanja wa Anfield ilipo pepo ya Soka duniani. Usiku wenye kiza kinene.

Sauti kali yenye mtetemo uliojaa hisia kali unapenya kwa fujo ndani ya masikio yangu. Sauti nzito ya Hayati Bill Shankly.

Huyu ndiye Baba wa Liverpool, Mzee Kiongozi kati ya wazee wenzake sita wenye heshima pale Anfield.

Kisha nikaisikia sauti ile ikinitaka nikae chini ya goli lililopo kaskazini mwa uwanja wa Anfield. Goli lililo upande ambao hukaa watukutu wa Spion Kop.

Ndilo goli ambalo Liverpool imefunga magoli mengi katika historia yake. Goli la ushindi. Upande wenye hisia kali kwa Liverpdulian wote.

Babu Bill ananieleza kiu ya mizimu ya Liverpool juu ya taji la Ligi Kuu ya England.Ananieleza namna ambavyo yeye na wazee wenzake John Holding (mwanzilishi wetu) na Kocha mwenye mataji mengi, Bob Paisley walivyo na njaa ya EPL.

Hakuna wanalotaka kusikia msimu huu zaidi ya EPL wamechoka kuona kelele za Manchester United na timu mbili za kitoto, Man City na Chelsea.
Kumbe hawana taimu na Arsenal hawaihofii maana haina mvuto kwa sasa wanakerwa na namna United, Chelsea na City wanavyotusumbua.

Bill anafunguka namna alivyoinyanyasa United enzi zake, anadai hawa Manchester City na Chelsea ni akina nani kwa sababu enzi zake zilikua ni kama timu za mitaani.Anaumia kuiona Liverpool yake aliyoijengea misingi ikiwa haijachukua ubingwa wa England kwa miaka 30.

Anasikitika sana maana huo ni umri ambao mjukuu wake Bill Shankly Jr (Mimi) naukaribia.

Ghadhabu inapanda juu yake anasema hawa akina Firmino, Van Djik wanapaswa kufahamu deni walilonalo kwa Kopites na wasidhani kuchukua mataji matatu ya Ligi ya Mabingwa, UEFA Supercup na Klabu bingwa Dunia ndio watakua wamemaliza, wale Scouser kiu yao no EPL.

Inabidi wakumbushwe kila saa thamani ya jezi walizovaa. Waelezwe nini maana ya kucheza Anfield.Bill ananinyanyua tena na kunipeleka eneo wasimamalo makocha kipande cha Liverpool (demarcation zone).

“ Klopp anapaswa kujua maana pia ya kusimama katika kizimba hiki, hawa watu 54,000 waliopo nyuma yake wanamuamini yeye.

Ni yeye pekee ambaye anaweza kuiamua furaha yetu sisi mashabiki wa Liverpool, ni yeye ambaye ameshika funguo ya mafanikio yetu,” anazungumza kwa hisia kali Bill.

Bill anatamani kumuona Allison akivaa gloves za Grobbellar, anataka kumuona Firmino akigeuka Kenny Dalglish. Mohammed Salah afunge mithili ya Iron Rush.

Wachezaji wa sasa wajue kuna watu waliipigania Klabu kwa jasho jingi lenye damu na machozi.

Yupo yeye Bill Shankly ambaye kwa mapenzi yake alisema Siku akifa mwili wake uchomwe moto na majivu yafukiwe Anfield.

Bill ndiye alianzisha utamaduni wa wachezaji na benchi la ufundi kugusa kibao kilichoandikwa This is Anfield wakiwa wanaingia uwanjani.

Alifanya hivyo ili kuwakumbusha wachezaji thamani ya klabu wanayoichezea.

Na sasa ananieleza jinsi gani amefurahishwa na Klopp kuwapiga marufuku wachezaji kugusa kibao kile hadi watakapobeba ubingwa wa EPL.

Shankly ananishika mkono tena na kunipeleka juu ya jukwaa la Spion Kop. Hapa ndipo ushindi wa Liverpool huanzia.

" Njaa ya hawa watu itamalizwa na ubingwa wa Ligi kuu," Bill ananiambia kisha anaongeza "kama hujawahi kuona uhuni wa Spion Kop basi ngoja tubebe taji.

Tunaelekea ndani ya uwanja wa Liverpool, mzee Bill ananionesha chumba cha Boot Room Tradition walichokua wakikitumia kuandaa mipango ya Liverpool.

‘ Hiki ndicho chumba ambacho tulikua tunajifungia mimi, Bob, Fagan, Bennett na wengine kuhakikisha na kupanga mipango kazi yetu.

Naona pia Klopp kama anajaribu kurudisha utamaduni huu, mwambieni akaze buti,” ananieleza Shankly.

Tunatoka hapo na kuelekea eneo lenye mataji yote ya Liverpool, 18 ya Ligi Kuu, Nane ya Kombe la Ligi, manne ya FA, Sita ya Ligi ya Mabingwa na matatu ya Europa na moja la Klabu Bingwa Dunia.

Bill anasema wachezaji wa sasa wataingia kwenye historia kubwa kuliko wengine wote waliowahi kutokea kama watabeba ubingwa.

Fikiria kikosi chenye Gerrard, Alonso, Mascherano, Kuyt na Torres kilishindwa kubeba halafu hawa akina Anord Trent wachukue ubingwa. Ni heshima ilioje.

Shankly anatania kidogo, “Hivi Gerrard atajisikiaje alishindwa kuiongoza Liverpool kubeba EPL halafu Henderson ameweza”? Kweli nitaamini Soka halitendi haki.

Ni jambo kubwa kama Liverpool itabeba ubingwa msimu huu, Bill anaamini majivu yake yaliyotandazwa uwanjani Anfield yatakua yametendewa haki.

Tunapaswa tutambue tupo katika nyakati bora mno kwenye historia yetu kwa kipindi cha miaka 30.Liverpool hii inatajwa kuwa ya ajabu na yenye kuogopwa na kila mtu.

Miaka 10 nyuma Manchester United ilikua ndio timu inayochukiwa na mashabiki wengi duniani. Kwanini?

Kwa sababu ilikua bora na yenye uhakika wa ushindi. Safari hii sisi ndio tunaochukiwa. Tumetimiza ndoto yetu ya kwanza. Na sasa tunakaribia kukamilisha ndoto yetu kuu ya ubingwa.

Shankly anasema mafanikio ya Liverpool yapo katika miwani za Klopp, kwa kipindi cha miaka 30 leo hii Liverpool inazungumzwa na wapinzani zaidi kuliko sisi tunavyowazungumza wao.

Ni hatua kubwa tumepiga, fikiria hatujabeba ubingwa kwa miaka yote hiyo lakini wana wivu na sisi, tunawanyima usingizi kuliko wao wanavyotunyima sisi.Kwanini wanaangaika na sisi hivyo? Bill anasema hivyo ndivyo Liverpool inapaswa iwe, izungumzwe vibaya na wapinzani siyo vizuri.

Shankly ananipeleka hadi nje ya uwanja wa Anfield. Ananiuliza umeziona hizo sanamu mbili?Namjibu ndiyo, moja ni yako Baba yetu nyingine ni ya mzee Holding.

Ananiambia inahitajika sanamu ya tatu nje ya uwanja wa Anfield, sanamu yenye sura ya Scouse aliedaptiwa, Jurgen Klopp.

Lakini ili ajengewe sanamu hilo na kuingia mioyoni mwa Scouses duniani, basi sharti ni Ligi Kuu tu. Hatutaki lingine.

Kwa sauti yenye mtetemo mkuu tena, Shankly akapaza sauti akisema, “ Ni zamu yetu, Ubingwa wa 19 unakuja Anfield nami nausubiri kwa hamu nikiwa chini ya uwanja wa Anfield”.

Ghafla akatoweka nami nikabaki nikitweta kwa hisia kuu, hisia zilizotawaliwa na hasira. Hasira ya kubeba Ligi Kuu.

Ni zamu yetu, ni wetu na tutasimama tukiwa wekundu. Forza Redmen

0683 015145

 Kikosi cha Liverpool kikishangilia goli lilofungwa katika moja ya michezo yao ya Ligi Kuu ya Soka nchini England ambapo wao ni vinara wa msimamo wakiwa na alama 61.
 Kocha wa Liverpool, Mjerumani Jurgen Klopp akiwa na tuzo yake ya Kocha bora wa mwezi Desemba. Klopp ametwaa tuzo nne za kocha bora wa mwezi kati ya tano ambazo zimeshatolewa mpaka sasa kwenye msimu huu.
 Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp akiwa katika picha tofauti na wachezaji wake, Roberto Firmino, Jordan Henderson na Divork Origi



from MICHUZI BLOG https://ift.tt/35L60CP
via

Post a Comment

0 Comments