Ticker

10/recent/ticker-posts

TRA YAVUNJA REKODI NYINGINE KWA KUKUSANYA TRILIONI 1.987 DESEMBA 2019

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Dkt. Edwin Mhede akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam (hawapo pichani) wakati akitangaza makusanyo ya kodi ya kipindi cha Robo ya Pili ya mwaka 2019/20 ambapo amesema kwa mara nyingine, TRA imevunja rekodi kwa kukusanya jumla ya kiasi cha sh. trilioni 1.987 kwa mwezi Desemba 2019 sawa na ufanisi wa asilimia 100.20 kutoka katika lengo la kukusanya kiasi cha sh. trilioni 1.983 kwa mwezi huo. Kulia kwake ni Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo Bw. Msafiri Mbibo.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Dkt. Edwin Mhede akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam (hawapo pichani) wakati akitangaza makusanyo ya kodi ya kipindi cha Robo ya Pili ya mwaka 2019/20 ambapo amesema kwa mara nyingine, TRA imevunja rekodi kwa kukusanya jumla ya kiasi cha sh. trilioni 1.987 kwa mwezi Desemba 2019 sawa na ufanisi wa asilimia 100.20 kutoka katika lengo la kukusanya kiasi cha sh. trilioni 1.983 kwa mwezi huo. Kulia kwake ni Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo Bw. Msafiri Mbibo na kushoto kwake ni Kamishna wa Idara ya Walipakodi Wakubwa Bw. Alfred Mregi.
******************************
Na Veronica Kazimoto
Dar es Salaam.

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa mara nyingine, imevunja rekodi kwa kukusanya jumla ya kiasi cha sh. trilioni 1.987 kwa mwezi Desemba 2019 ambayo ni rekodi ya kwanza kufikiwa tangu kuanzishwa kwake ikilinganishwa na rekodi ya mwezi Septemba, 2019 iliyokuwa sh. trilioni 1.767.  

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo Dkt. Edwin Mhede amesema kuwa, makusanyo hayo ya mwezi Desemba 2019 ni sawa na ufanisi wa asilimia 100.20 kutoka katika lengo la kukusanya kiasi cha sh. trilioni 1.983 kwa mwezi huo.

“Ni kweli kwamba, kitaalam, miezi tofauti hailinganishiki moja kwa moja. Hata hivyo, kwa makusanyo haya ya sh. trilioni 1.987 kwa mwezi Desemba 2019, TRA imevunja rekodi yake yenyewe iliyoiandika mwezi Septemba 2019 ambapo ilikusanya jumla ya sh. trilioni 1.767 ikiwa ni sawa na asilimia 97.20 ya lengo la kukusanya sh. trilioni 1.817 katika kipindi hicho,” alisema Dkt. Mhede.

Akizungumzia makusanyo ya kipindi cha Robo ya Pili ya mwaka 2019/20 inayohusisha mwezi Oktoba, Novemba, na Desemba yenyewe, Kamishna Mkuu Mhede amesema kuwa, TRA imefanikiwa kukusanya jumla ya sh. trilioni 4.972 sawa na ufanisi wa asilimia 97.49 ya lengo la kukusanya jumla ya sh. trilioni 5.100.

“Makusanyo haya ya robo ya pili ya mwaka 2019/20 ni sawa na ukuaji wa asilimia 19.78 ikilinganishwa na kipindi kama hiki cha Robo ya Pili ya mwaka 2018/19 ambapo Mamlaka ilikusanya sh. trilioni 4.151 ikiwa ni sawa na ufanisi wa asilimia 87.59 kutokana na lengo la kukusanya mapato kiasi cha sh. trilioni 4.739 katika kipindi hicho,” alifanunua Kamishna Mkuu Mhede.

Ameeleza kuwa, kwa upande wa makusanyo ya mapato ya Serikali kwa mwezi Oktoba 2019, TRA ilikusanya kiasi cha sh. trilioni 1.484 na Novemba 2019, Mamlaka ilikusanya sh. trilioni 1.501 sawa na ufanisi wa asilimia 93.98 na asilimia 97.59 kutoka katika malengo ya kukusanya sh. trilioni 1.579 na sh. trilioni 1.538 kwa mwezi Oktoba na Novemba 2019.

Kamishna Mkuu Mhede ameongeza kuwa, makusanyo hayo ni muendelezo wa kiashiria cha wazi kwamba Walipakodi na Watanzania walio wengi wameendelea kuelewa, kukubali, na kuitikia wito wa Serikali ya Awamu ya Tano wa kuongeza mapato ya ndani kwa ajili ya maendeleo ya Taifa zima. 

“Kwa kuwa Walipakodi wengi wameitikia wito wa kulipa kodi kwa mujibu wa Sheria, ni rai yangu kwamba asiwepo mlipakodi hata mmoja ambaye atathubutu kubaki nyuma. Ni busara wafanyabiashara wote wakaungana na kundi kubwa la Washindi, yaani, kundi kubwa la wanaolipa kodi kwa hiari, kwa ukamilifu, na kwa wakati, alisisitiza Dkt. Mhede.

Pia, amewashukuru walipakodi waliolipa kodi kwa wakati na hivyo kupelekea kuongezeka kwa makusanyo ambayo yatapelekea utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini.

“Kwa namna ya kipekee, napenda kuwashukuru Walipakodi wote waliolipa kodi ya Serikali na kupelekea Mamlaka kufikia makusanyo haya ya kihistoria kwa mwezi Desemba 2019. Pia, tunaishukuru sana Serikali ikiwa ni pamoja na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bodi ya Wakurugenzi ya TRA, Taasisi za Maendeleo, na Sekta Binafsi kwa kuendelea kuipatia TRA ushirikiano stahiki katika kutekeleza majukumu yake ya kukadiria, kukusanya, na kuhasibu mapato ya Serikali,” Alisema Kamishna Mkuu Mhede.

Aidha, ametoa wito kwa wamiliki wote wa majengo nchini kujitokeza kulipia kodi za majengo ili kuepuka usumbufu wa kulipa mwishoni mwa mwaka wa fedha 2019/2020 ambapo amesema kuwa, kwa sasa viwango ni rafiki na vinalipika kwa urahisi.

Amevitaja viwango hivyo kwa mwaka kuwa ni sh. 10,000 kwa nyumba ya kawaida, sh. 50,000 kwa kila sakafu ya nyumba ya ghorofa katika Majiji, Manispaa, na Halmashauri za Miji, na sh. 20,000 kwa jengo la ghorofa katika maeneo ya Halmashauri za Wilaya.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2tjTzAb
via

Post a Comment

0 Comments