SHULE YA MFANO DODOMA KUZINDULIWA FEBRUARI 5 MWAKA HUU, NAIBU KATIBU MKUU TAMISEMI ATEMBELEA UJENZI WAKE

  Masama Blog      
Charles James, Michuzi TV

SERIKALI imesema ujenzi wa Shule ya Mfano ya Ipagala iliyopo jijini Dodoma unatarajia kukamilika hivi karibuni na itazinduliwa Februari 5, mwaka huu ikiwa na jumla ya wanafunzi 705 kuanzia elimu ya awali hadi darasa la saba.

Akizungumza kwenye ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wake, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI anaeshughulikia elimu, Gerald Mweli amesema shule hiyo imejengwa ikiwa ni mikakati iliyopo ya kupunguza msongamano wa wanafunzi katika Shule za msingi.

Mweli amesema shule hiyo itakua na uwezo wa kuchukua wanafunzi 705 ambao watasajiliwa kutoka shule tano zilizopo jirani ambazo ni Shule ya Msingi Ipagala, Ipagala B, Chadulu, Medeli na Mlimwa C na idadi ya walimu ambao inahitajika ni takribani 20.

" Usajili wa kuwapata wanafunzi watakaojiunga hapa umezingatia vigezo mbalimbali ikiwemo kukagua kadi zao za maendeleo na matokeo ya mitihani ya ndani ya shule ya wanafunzi husika na kujiridhisha na uwezo wa kielimu walionao.

Hii shule ni ya mfano hivyo tofauti na ubora wa miundombinu yake lakini suala la ubora wa wanafunzi kitaaluma ni jambo ambalo tunalizingatia sana. Tunataka kweli iwe ni shule ya mfano," Amesema Mweli.

Amesema kwa miundombinu shule hiyo imefikia asilimia 95 ambapo kwa upande wa samani madawati 295 tayari yameshaanza kutengenezwa kwenye kiwanda cha SIDO kilichopo jijini Dodoma huku wakiendelea pia kutengeneza viwanja vya michezo ukiwemo Mpira wa Miguu, Mpira wa Pete, Mpira wa Mikono na Mpira wa Wavu.

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Elimu Msingi, Joseph Mabeyo amesema Idara yake imepanga kuandaa mkutano na wananchi waliopo jirani na shule hiyo wakiwemo wazazi ambao watoto wao watasoma hapo ili kutoa elimu kwao kuhusu umuhimu wa elimu, umiliki wa shule, ulinzi wa mali za shule na suala la utoaji wa chakula kwa wanafunzi shuleni hapo.

Katika hatua nyingine Naibu Katibu Mkuu pia alitembelea Shule ya Sekondari Dodoma na kufanya mazungumzo na walimu wa shule hiyo ambapo amewapongeza kwa mafanikio waliyoyapata kwa kuongeza ufaulu katika mitihani yake ya kitaifa.

" Ninawapongeza sana shule hii matokeo ya mwaka jana ilikua na zero 67 kwenye matokeo ya kidato cha nne, mwaka huu mmepunguza hadi 19, Daraja la kwanza zilikua tano mwaka jana, mwaka huu zimeongezeka hadi 13, daraja la pili zilikua 20 mwaka huu zimepanda hadi 32 kwa kweli hili ni jambo kubwa licha ya kuwa na changamoto nyingi.

Nimezungumza nao tutashughulikia changamoto zilizopo na tumekubaliana matokeo yajayo tunafuta daraja la nne na sifuri. Niwasihi muongeze bidii na juhudi katika ufundishaji wenu lengo likiwa ni kukuza kiwango cha ufaulu katika shule hii kongwe. Na mimi nimejitolea kuwa mlezi wenu," Amesema Mweli.
 Sehemu ya majengo ya madarasa katika shule ya msingi ya Mfano iliyopo jijini Dodoma kama yanavyoonekana ambapo ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 95. 

 Shule ya Mfano iliyopo jijini Dodoma kama inavyoonekana ambapo Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Gerald Mweli ametembelea kukagaua maendeleo ya ujenzi wake.
 Afisa Elimu Msingi wa Jiji la Dodoma, Joseph Mabeyo akisoma taarifa fupi ya ujenzi wa shule hiyo ya mfano mbele ya Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Gerarld Mweli wakati wa ziara ya kukagua ujenzi wa shule hiyo.
 Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Gerald Mweli akiwa kwenye shule ya mfano ya Ipagala iliyopo jijini Dodoma alipofika kujionea maendeleo ya ujenzi wake.

 Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Gerald Mweli akizungumza na walimu wa shule ya Sekondari Dodoma alipofika kuwatembelea na kuzungumza nao.

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Gerald Mweli akizungumza na walimu wa Shule ya Sekondari Dodoma alipofika kuzungumza nao ikiwa ni pamoja na kusikiliza changamoto zao.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/38Ik5Tn
via
logoblog

Thanks for reading SHULE YA MFANO DODOMA KUZINDULIWA FEBRUARI 5 MWAKA HUU, NAIBU KATIBU MKUU TAMISEMI ATEMBELEA UJENZI WAKE

Previous
« Prev Post