NAIBU WAZIRI MABULA AZITAKA HALMASHAURI KUTENGA BAJETI ZA MABARAZA YA ARDHI YA KATA NA VIJIJI

  Masama Blog      
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na vibarua wa mradi wa ujenzi wa Ofisi ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Obadia Kita na Yusufu Kijalo wakati alipokwenda kukagua maendeleo ya mradi huo unaojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwenye Shamba la Misitu la Iyondo Msimwa Ileje mkoani Songwe mwishoni mwa wiki. Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akioongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Ileje Joseph Mkude (kulia kwake) kwenda kukagua maendeleo ya ujenzi wa Ofisi ya Meneja Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania kwenye Shamba la Miti la Iyondo Msimwa wilayani ileje mkoa wa Songwe mwishoni mwa wiki alipokwenda kukagua mradi huo unaojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa. Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (Kulia), Meneja Mawasiliano wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Muungano Saguya, Mkuu wa wilaya ya Ileje Joseph Mkude na Kaimu Meneja wa NHC mkoa wa Mbeya Pauline Kamaghe wakitazama maendeleo ya ujenzi wa nyumba ya Meneja Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwenye Shamba la Miti la Iyondo Msimwa wilayani ileje mkoa wa Songwe mwishoni mwa wiki alipokwenda kukagua maendeleo ya mradi huo unaojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC). Mkuu wa wilaya ya Ileje Joseph Mkude akisisitiza jambo kwa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula wakati Naibu Waziri alipotembelea wilaya ya Ileje kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi pamoja na ujenzi wa miradi inayofanywa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) mwishoni mwa wiki. Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akisisitiza jambo alipozungumza na viongozi pamoja na watendaji wa sekta ya ardhi katika wilaya ya Mbozi mkoa wa Songwe mwishoni mwa wiki wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika mkoa wa Songwe.Anayemuangalia ni Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brigedia Jenerali Mstaafu Nicodemus Mwangela.

(PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)

…………………………………………………………

Na Munir Shemweta, WANMM ILEJE

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amewataka wakurugenzi wa Halmashauri nchini kutenga bajeti kwa ajili ya Mabaraza ya Ardhi ya Kata na Vijiji sambamba na kufuatilia tozo zinazotozwa na Mabaraza hayo ili yafanye kazi kwa ufanisi.

Dkt Mabula alitoa agizo hilo mwishoni mwa wiki wilayani Ileje na Mbozi wakati akizungumza na viongozi pamoja na watendaji wa sekta ya ardhi akiwa katika ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi na ujenzi wa miradi inayofanywa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) mkoani Songwe.

Naibu Waziri Mabula alisema, Wakurugenzi wa Halmashauri nchini wamekuwa hawatengi bajeti kwa ajili ya Mabaraza ya Ardhi ya Kata na Vijiji jambo linalosababisha Wajumbe wake kujifanyia mambo wanavyotaka ikiwemo kuweka viwango tofauti vya tozo za kwenda uwandani.

Kwa mujibu wa Dkt Mabula, Mabaraza ya Ardhi ya Kata na Vijiji yanapaswa kusimamiwa na Wakurugenzi wa Halmashauri kwa kuyapatia kwa kuyatengea bajeti za kuendesha ofisi kama vile Shajala sambamba na kujua yanayofanyika ikiwemo tozo zake ili kuepuka uonevu unaoweza kujitokeza kwa wananchi wanaoshitakiana.

‘’Katika Mabarza ya Ardhi ya Kata na Vijiji watu wanalipa tozo kulingana na sura kama mtu kavaa tai basi anapigwa shilingi elfu hamsini jambo linalowaumiza wananchi’’ alisema Mabula

Alizitaka ofisi za Wakurugenzi wa halmashauri nchini kuyasimamia Mabaraza hayo na kutoa semina kwa wajumbe wake na kuyapangia viwango vya tozo na kusisitiza kuwa hayo yasipofanyika kuna hatari wajumbe wake kufanya maamuzi kwa matakwa ya wenye uwezo.

Amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kubadilika katika kuyasimamia mabaraza ya ardhi ya kata na vijiji na kubainisha kuwa Mabaraza hayo yakifanya vizuri yatapunguza mlundikano wa kesi za ardhi zinazokwenda Mabaraza ya ardhi ya nyumba ya Wilaya.

Awali Afisa Mipango Miji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje mkoa wa Songwe Dismas Ndinda alimueleza Naibu Waziri Mabula kuwa halmashauri hiyo pamoja na kuwa Mabaraza ya Ardhi ya Kata na Vijiji sabini na moja lakini haina Baraza la ardhi la wilaya jambo linalowafanya wananchi wanaoshindwa kupata suluhu kusafiri hadi Mbeya kupata huduma za Baraza la Ardhi la Wilaya.

Wakati huo huo, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alikagua maendeleo ya ujenzi wa Ofisi na nyumba ya Meneja ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) unaofanywa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) katika shamba la Miti la Iyondo Msimwa wilaya ya Ileje mkoa wa Songwe.

Akikagua maendeleo ya ujenzi huo, Dkt Mabula mbali na kuridhishwa na maendeleo ya mradi huo alisema mradi wa ujenzi wa ofisi na nyumba ya Meneja wa TFS utasaidia ufuatiliaji wa msitu huo kwa kuwa Meneja wake atakuwa akiishi karibu na msitu huo. Aidha, ameuelezea mradi huo kuwa umesaidia pia kutengeneza ajira ya muda kwa wakazi wa eneo hilo na kuwawezesha kupata kipato cha mahitaji madogomadogo.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa NHC mkoa wa Mbeya Pauline Kamaghe alisema mradi huo unaojengwa na Shirika lake unatarajiwa kugharimu kiasi cha milioni 426.8 na kukamilika mwezi April mwaka huu wa 2020 na kubainisha kuwa kwa sasa mradi umefikia asilimia 38 ya ujenzi.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2tFMLgZ
via
logoblog

Thanks for reading NAIBU WAZIRI MABULA AZITAKA HALMASHAURI KUTENGA BAJETI ZA MABARAZA YA ARDHI YA KATA NA VIJIJI

Previous
« Prev Post