Ticker

10/recent/ticker-posts

MAHAKAMA YAMGOMEA KABENDERA KUAGA MWILI WA MAMA YAKE

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imetupilia mbali  maombi ya  Mwandishi wa Habari za Uchunguzi, Erick Kabendera ya kutaka kwenda kushiriki Ibada ya kumuaga mama yake mzazi, Verdiana Mujwahuzi aliyefariki dunia Desemba 31, 2019.

Kabendera ambaye anakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashitaka ya utakatishaji fedha, alionekana kujifuta machozi huku  ndugu zake ambao walifurika mahakamani walionekana wenye majonzi kutokana na kifo cha maka huyo.

Akitoa uamuzi huo jana, Hakimu Mkazi Mwandamizi, Janeth Mtega alisema  mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza maombi yoyote juu ya kesi hiyo ya uhujumu uchumi  ispokuwa kwa kibali maalum kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP).

Hakimu Mtega pia alisema hakuna fursa ya waombaji kukata rufaa katika uamuzi huo.

Hatua ya kukataliwa kwa maombi ya Kabendera imekuja baada ya Wakili wake, Jebra Kambole kuiomba  mahakama hiyo imruhusu Kabendera akashiriki Ibada ya kumuaga ya Mama yake mzazi katika Kanisa  Katoliki Changombe inayofanyika leo majira ya mchana kabla ya kusafirishwa kwa mwili huo kuelekea Bukoba mkoani Kagera kwa maziko.

Kambole alidai kuwa suala la kushiriki sala ya mwisho ya msiba ni haki ya binadamu na ni suala la faragha.

Alidai kushindwa kwake  kuhudhuria maziko ya mama yake watakuwa wamemuadhibu adhabu kubwa  kwa kuangalia uhusiano wa mshitakiwa na mama yake mzazi kwani alikuwa akimuuguza hivyo, ni vizuri akatoa heshima ya mwisho.

Pia alidai  ni muhimu kwa Kabendera kushiriki ibada hiyo kwa sababu mama mzazi ni mmoja na kwamba anapokufa  anaagwa mara moja.

"Jamhuri haitaathirika kwa lolote kwa sababu mshitakiwa atakuwa chini ya ulinzi na ibada itakuwa mchana kanisani na Temeke sio mbali na gerezani, tunaomba akatoe heshima ya mwisho," alidai Kambole.

Baada ya kueleza hayo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon alimpa pole Kabendera kwa kufiwa na mama yake mzazi na kwamba mahakama isifungwe mikono kwa maombi yaliyowasilishwa ya kutaka kushiriki msiba huo.

Simon alidai  kuwa maombi ya Kabendera kupitia mawakili wake yamewasilishwa wakati ambao si sahihi kwa sababu mahakama haina mamlaka na pia DPP hajaipa mahakama hiyo kibali cha kusikiliza kesi hiyo.

"Katika macho ya kisheria mahakama yako haina mamlaka, hata sisi tuna masikitiko makubwa lakini mahakama isifungwe mikono," alidai Simon.

Awali, kabla ya maombi hayo, Wakili Simon alidai upelelezi wa kesi hiyo unaendelea na shauri limefika hatua nzuri ya maelewano baina ya mshitakiwa na DPP.

Katika kesi hiyo, Kabendera anakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashitaka matatu likiwemo la utakatishaji wa Sh milioni 173.

Katika mashitaka ya kwanza, ilidaiwa kuwa katika kipindi hicho, Kabendera alijihusisha  na mtandao wa kihalifu kwa kutoa msaada kwa genge la uhalifu kwa nia ya kujipatia faida.

Inadaiwa kuwa katika kipindi hicho,bila ya sababu,alikwepa kodi ya Sh 173,247,047.02 ambayo ilitakiwa ilipwe Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Pia inadaiwa Kabendera  alitakatisha Sh 173,247047.02 huku akijua fedha hizo ni mazalia ya kosa la kujihusisha na genge la uhalifu na ukwepaji kodi.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/35jWOoq
via

Post a Comment

0 Comments