Ticker

10/recent/ticker-posts

KIVUKO KIPYA KAYENZE BEZI CHASHUSHWA KWENYE MAJI


 Kivuko kipya cha MV.Ilemela kikielea majini mara baada ya kushushwa , kivuko hicho ambacho ujenzi wake umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 2.7 za Kitanzania kitakua kikitoa huduma kati ya Kayenze na Kisiwa cha Bezi na kina uwezo wa kubeba abiria 200 na magari 10 sawa na tani 100.
Naibu Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi na Mawasiliano) Mhe. Atashasta Nditiye katikati akiwa ameshikana mkono na Mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongella katika picha ya pamoja mara baada ya kumaliza zoezi za kushusha kivuko kipya cha Kayenze na kisiwa cha Bezi kilichogharimu shilingi bilioni 2.7 ambacho kimepewa jina MV.Ilemela, tukio lililofanyika katika yadi ya Songoro Ilemela jijini Mwanza. Kushoto kwa Mongella ni Mbunge wa Iilemela Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Makazi Mhe. Angelina Mabula na wa tatu kushoto ni Mtendaji Mkuu TEMESA Mhandisi Japhet Maselle. Kivuko cha MV.Ilemela kina uwezo wa kubeba abiria 200 na magari 10 sawa na tani 100.
Naibu Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi na Mawasiliano) Mhe.  Atashasta Nditiye katikati akifurahia jambo na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Maselle wa pili kushoto mara baada ya kumaliza zoezi la kukagua na kukishusha kwenye maji kivuko cha MV.Ilemela. Kivuko cha MV.Ilemela kina uwezo wa kubeba abiria 200 na magari 10 sawa na tani 100 na kimejengwa kwa gharama ya shilingi bilioni2.7.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Maselle akisoma taarifa fupi ya mradi wa ujenzi wa kivuko cha MV.Ilemela wakati wa hafla ya kukishusha majini kivuko hicho iliyofanyika katika yadi ya Songoro iliyopo Ilemela jijini Mwanza. Kushoto ni Mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongella na katikati ni Naibu Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi na Mawasiliano) Mhe.  Atashasta Nditiye. Kivuko cha MV.Ilemela kina uwezo wa kubeba abiria 200 na magari 10 sawa na tani 100 na kimejengwa kwa gharama ya shilingi bilioni2.7.
…………………………………………………

NA ALFRED MGWENO (TEMESA MWANZA) 

Wakazi wa Ilemela mkoa wa Mwanza leo wameshuhudia kwa mara ya kwanza kivuko kipya cha Kayenze Bezi, MV.Ilemela ambacho kimegharimu kiasi cha shilingi bilioni 2.7 kikishushwa kwenye maji baada ya kukamilika kwa ujenzi wake. Tukio hilo limefanyika katika yadi ya Songoro iliyopo Wilaya ya Ilemela ambapo mgeni rasmi alikua Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi na Mawasiliano) Mhe. Atashasta J. Nditiye (MB).

Akizungumza katika tukio hilo Mhe. Nditiye alimshukuru Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na serikali ya awamu ya tano kwa kuendelea kutimiza ahadi ya miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini.

‘’Hadi sasa Mheshimiwa Rais tayari ameshatoa fedha zote kiasi cha shilingi za Kitanzania bilioni 9,953,916,200 iliyokuwa imepangwa kwenye bajeti ya miradi ya maendeleo ya vivuko kwa mwaka wa fedha wa 2019/2020’’, alisema Mhe. Naibu Waziri ambapo aliongeza kuwa kivuko cha MV.Ilemela kitakapoanza kutoa huduma kitaondoa changamoto ya usafiri kwa wananchi kati ya Kayenze na kisiwa cha Bezi. 

‘’Kivuko hiki kitakapoanza kutoa huduma ni dhahiri kuwa kitaondoa changamoto ya usafiri kwa wananchi kati ya Kayenze na kisiwa cha Bezi hivyo kitainua maisha ya wananchi wa maeneo hayo kibiashara, kiuchumi na kijamii, mara tu mtakapokamilisha majaribio anzeni kutoa huduma ’’. Aliongeza Naibu Waziri ambapo pia alitoa wito kwa watumishi wa TEMESA kufanya kazi kwa weledi na kuhakikisha kivuko hicho pamoja na vivuko vingine vinatunzwa vizuri na vinadumu kwa muda mrefu huku wakizingatia usalama wa abiria na mali zao.

Awali, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle, akisoma taarifa kwa mgeni rasmi katika tukio hilo alisema serikali kupitia TEMESA inaendelea na ujenzi wa vivuko vingine vipya kwa ajili ya Mafia Nyamisati kwa gharama ya shilingi bilioni 5.3, Bugorola Ukara kwa gharama ya shilingi bilioni 4.2 pamoja na Chato Nkome kwa gharama ya shilingi bilioni 3.1. 

‘’Vivuko hivi vyote vinagharimu jumla ya shilingi za Kitanzania bilioni 15.3 na fedha zote hizi zinatolewa na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania’’, alisema Mhandisi Maselle ambapo aliishukuru serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutoa fedha zote zilizotengwa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya ununuzi wa vivuko, ukarabati na ujenzi wa maegesho ya vivuko, ambapo alisema Fedha hizo zimewezesha miradi hiyo kuanza na mingine kuwepo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Naye Mbunge wa Ilemela Mhe. Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angelina Mabula akizungumza katika tukio hilo aliishukuru serikali kwa kuweza kutimiza ahadi iliyoitoa. ‘’Nimshukuru Mhe. Rais niwashukuru TEMESA kwa kazi kubwa na nzuri ambayo imefanyika, tunao uhakika sasa kwamba adha ya usafiri katika eneo la visiwa vya Kayenze Bezi sasa litakua ni historia’’, alisema Dkt. Mabula.

Aidha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella alimuomba Mhe. Nditiye kufikisha salamu za shukrani kwa Rais kwa mambo makubwa anayoufanyia mkoa wa Mwanza hasa kwenye sekta ya usafiri wa majini ambapo alisema watu wa mkoa huo wanategemea mwezi wa pili kuona vivuko  vingine vikiingia ziwani tayari kuanza kutoa huduma kwa wananchi.

Kivuko cha MV.Ilemela kina uwezo wa kubeba abiria 200 na magari 10 sawa na tani 100. Hadi sasa Wakala unaendesha na kusimamia vivuko 30 katika vituo (Ferry stations) 20 Tanzania Bara na hivyo kukamilika kwa kivuko cha MV. Ilemela kutafanya idadi ya vivuko kufikia 31 na vituo kuwa 21.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/35vXPKi
via

Post a Comment

0 Comments