Ticker

10/recent/ticker-posts

KITUO KINGINE CHA HIJA KWA BIKIRA MARIA CHAZINDULIWA MKOANI SINGIDA


Askofu wa Jimbo Katoliki Singida, Mhashamu Edward Mapunda, akipanda kwenye sehemu ya juu ya Kituo cha Hija Sukamahela kwa ajili ya kutoa baraka kabla ya misa takatifu. Kituo hicho kimejengwa eneo la Sukamahela, wilaya ya Manyoni mkoani Singida eneo ambalo lipo katikati ya Tanzania.

Mwonekano wa Kituo kipya cha hija cha sukamahela, kilichojengwa kwa heshima ya Bikira Maria na kuzinduliwa ( juzi) eneo la Sukamahela, wilaya ya Manyoni mkoani Singida.

Waumini wakipanda juu ya mwinuko wa eneo kilipojengwa kituo hicho.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi akihutubia.



Msafara kwa ajili ya uzinduzi.

Shughuli ya uzinduzi ikiendelea.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi akipata upako wa maji ya Baraka kutoka kwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Singida, Mhashamu Edward Mapunda.

Na Mwandishi Wetu, Singida
KAULI ya kwamba Singida ni njema tena ni njema sana, imezidi kujidhihirisha baada ya mkoa huo kubarikiwa kuanza mwaka wa 2020 kwa tukio la aina yake la uzinduzi wa kituo cha hija kwa heshima ya Bikira Maria kilichopo eneo la Sukamahela, mahali ambapo ni katikati ya nchi ya Tanzania, wilaya ya Manyoni mkoani hapa

Kituo cha Sukamahela ambacho watu watakuwa wakikusanyika kila ifikapo Desemba 9, na ambacho kimejengwa kwa ustadi mkubwa kinakuwa ni cha pili ndani ya mkoa wa Singida, kikitanguliwa na kile cha kwanza kilichopo eneo la Kimbwi nje kidogo ya mji, ambacho pia kwa lengo lile lile hutoa fursa ya watu kukutana na Mungu kwa njia ya Bikira Maria ifikapo Septemba kila mwaka.

Akizindua Kituo hicho juzi, Askofu wa Jimbo Katoliki la Singida, Mhashamu Edward Mapunda, alisema kituo cha hija Sukamahela kinakwenda kutoa fursa ya watu kujikabidhi kwa mama Bikira Maria msaada wa daima kwa maombezi.

“Kituo hiki hakikuzinduliwa kwa bahati mbaya ni zawadi ya Mwenyezi Mungu kwa binadamu wote. Na tusisubiri hadi tarehe 9 Desemba pekee ndio tukusanyike hapa bali kila mara tukipata nafasi tufike…kila anayepita eneo hili asiache kuchepuka hapa au usisahau kupiga ishara ya msalaba ukimwambia mama napita hapa,” alisema Mapunda.

Alisema kwa kuzingatia kwamba binadamu wote wanakwenda kwa Yesu Kristu kupitia Bikira Maria ni dhahiri uwepo wa kituo hicho utasaidia sana kuimarisha imani na kuleta chachu ya uinjilishaji, pia ni fursa ya Baraka na neema katika kuombea amani ya familia, mkoa na taifa, sambamba na kuimarisha ibada za waumini kupitia mama huyo.

Hata hivyo, Askofu Mapunda kwa namna ya pekee alimshukuru na kumpongeza Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk Rehema Nchimbi, ambaye mbali ya kuwa rafiki mzuri wa Bikira Maria lakini pia ndiye mwasisi wa wazo hilo takatifu kwa kuona na hatimaye kushauri jumuiya ya kanisa hilo kujenga kituo cha hija mahali hapo.

“Tunamshukuru sana Mkuu wa Mkoa mama Nchimbi, wazo hili limetoka kwa Mungu kupitia yeye. Siku aliponiletea wazo hili na nilipotafakari nikaona ni wazo la Mungu na ni ufunuo, maana mambo haya ni ya kimungu na Mwenyezi Mungu anaweza kumfunulia yeyote…na hatimaye tulilipokea kwa mikono miwili,” alisema Askofu wa Jimbo Katoliki la Singida.

Aidha, Mapunda kupitia Mkuu wa Mkoa, alimshukuru Rais John Magufuli kwa mchango wake katika kufanikisha ujenzi wa kituo hicho cha hija, alioutoa hivi karibuni akiwa safarini wakati alipopita mkoani hapa kuelekea chato mkoani Geita kwa mapumziko.

Akiwasilisha ujumbe wa siku ya amani kwa mwaka mpya 2020 kutoka kwa Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francisco, Askofu Mapunda alisema amani ni safari ya matumaini, majadiliano, upatanisho, uongofu wa ekolojia (mazingira) na haiwezi kujengeka kwa vitisho na hofu ya maangamizi.

“Amani ya kweli inafumbatwa katika mifumo ya kisiasa, kijamii na kiuchumi inayozingatia haki na msamaha, hivyo tujitahidi kila mmoja wetu kuwa chombo cha amani,” alisema Askofu Mapunda akimnukuu Papa Francisco.

Zaidi, wakati taifa likielekea kwenye uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika mwaka huu, Askofu Mapunda aliwasihi watanzania kote nchini kuiweka nchi katika sala, hasa kupitia Bikira Maria ili aweke uchaguzi huo kwenye moyo wake mtakatifu, kwasababu yeye ni ‘Malkia wa Amani’.

Kwa upande wake mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Nchimbi, alisema kila Mtanzania anapaswa kuwa shahidi juu ya ushuhuda wa wazi usio na mashaka kuhusu upendo mkubwa na uwajibikaji wa Bikira Maria kwa ulinzi wake, malezi, maombezi na usalama wa Taifa.

Alisema anakumbuka jinsi uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka 2015 ulivyojaa misukosuko, hofu na mashaka, wasiwasi na hata wengine walitamani kuikimbia Tanzania, huku akikiri kwamba kilichotuvusha salama sio kingine bali ni Bikira Maria.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2QNDJWG
via

Post a Comment

0 Comments