Kamati ya Siasa mkoa wa Arusha yaipongeza Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.

  Masama Blog      

Na Kassim Nyaki-NCAA

Kamati ya siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Arusha ikiongozwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha Mhe. Zelothe Stephen Zelothe imefanya ziara ya kukagua utekelezaji wa ilani ya chama hicho katika hifadhi ya Ngorongoro.

Mwenyekiti wa CCM mkoani Arusha Mhe. Zelothe Stephen aliyeambatana na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Mrisho Gambo pamoja na wajumbe wa kamati hiyo mkoani Arusha ameeleza kuwa ziara hiyo imelenga kutembelea na kukagua utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi kupitia kazi mbalimbali zinazofanywa na Mamlaka hiyo hasa miradi mbalimbali inayotekelezwa ndani na nje ya Hifadhi hiyo.

Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Ngorongoro Dkt Freddy Manongi ameieleza kamati hiyo kuwa pamoja na utekelezaji wa malengo makuu matatu ya Uhifadhi, Utalii na maendeleo ya jamii, Mamlaka hiyo imeendelea pia kutoa msaada wa fedha kwa jamii katika miradi ya afya, elimu, maji, mifugo na chakula kwa wakazi wanaoishi ndani ya hifadhi hiyo.

Dkt Manongi ameongeza kuwa katika kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt John Pombe Magufuli, katika mwaka wa fedha 2018//2019 Mamlaka hiyo imetoa kiasi cha shilingi milioni 500 ili kusaidia ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Karatu, pia imetoa shilingi milioni 400 za ujenzi wa Hospitali ya Samunge iliyoko Loliondo, vilevile imechangia kiasi cha shilingi milioni 100 katika ujenzi wa kituo cha afya Arash kilichopo Loliondo Wilayani Ngorongro.

Kamishna Manongi pia amebainisha kuwa takribani asilimia 47 ya mapato ya NCAA kwa kila mwaka zinaelekezwa kwenye shughuli nyingine za Kiserikali ikiwemo kutoa gawio Serikalini na kusaidia shughuli mbalimbali za maendeleo hasa ujenzi wa miundombinu na huduma za kijamii kama maji, elimu, ujenzi wa vituo vya afya, majosho, chanjo za mifugo na kusaidia vikundi vya ushirika vya wananchi ndani ya hifadhi hiyo ikiwa ni sehemu ya mchango wake katika kuunga mkono juhudi kazi Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi.

Kwa upande wake mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Mashaka Gambo ameileza kamati ya siasa mkoa wa Arusha kuwa Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro imeendelea kuwa mdau mkubwa katika kuunga mkono juhudi za Serikali hasa katika kuchangia shughuli za maendeleo na kuupongeza uongozi wa mamlaka hiyo kwa kazi nzuri wanayoifanya.

 Kamishna wa Uhifadhi kwa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Dkt Freddy Manongi (aliyesimama) akitoa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kamati ya Siasa ya Mkoa wa Arusha.
 Kamati ya siasa mkoa wa Arusha wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM wa mkoa huo Mhe. Zelothe Stephen (kulia) wakisikiliza maelezo kuhusu ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Karatu Mkoani Arusha.


 


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2sHFixd
via
logoblog

Thanks for reading Kamati ya Siasa mkoa wa Arusha yaipongeza Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.

Previous
« Prev Post