JAFO AKERWA NA MAZINGIRA YA SOKO LA SABASABA, ALIAGIZA JIJI LA DODOMA KUANZA UJENZI WAKE MARA MOJA

  Masama Blog      
Charles James, Michuzi TV

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe Selemani Jafo amekerwa na uchafu wa mazingira uliopo katika soko la Sabasaba jijini Dodoma na kumuagiza Mkurugenzi wa Jiji hilo kuhakikisha ujenzi wa soko hilo unaanza kabla ya kuisha kwa Bunge la bejeti.

Mhe Jafo amesema ni jambo la aibu kwa Jiji la Dodoma linaloongoza kwa kukusanya mapato takribani Bilioni 71 kuwa na soko lenye mazingira machafu yanayohatarisha maisha ya wananchi.

Waziri Jafo ameyasema hayo leo alipofanya ziara yake ya kikazi na kukagua ujenzi wa Hospitali ya Uhuru iliyopo wilayani Chamwino kabla ya kupita kujionea hali ilivyo kipindi hichi cha mvua kwenye soko hilo la Sabasaba.

Amesema ni jambo la kushangaza kuona Jiji linaloongoza kwa kukusanya mapato ya ndani likiacha soko lake lililopo katikati ya maji likiwa katika hali chafu na hivyo kuharibu taswira ya Makao Makuu ya Nchi.

" Sijapenda hali niliyoiona hapa, Kaimu Mkurugenzi na Katibu Tawala Mkoa waambieni baraza la madiwani sijafurahishwa na mazingira ya Sabasaba. Hivyo naagiza kabla ya kuisha kwa bunge la bajeti ujenzi wa soko hili uwe umeshaanza.

Mazingira ya hapa ni machafu sana hii haiwezi kukubalika ndani ya Jiji la Dodoma kuwe na soko lenye kuhatarisha afya za wananchi wetu, mnafanya vizuri kwenye mapato basi fanyeni vizuri na huku pia. Nataka ujenzi uanze mara moja na mimi nitarudi tena kukagua," Amesema Mhe Jafo.

Awali Mhe Jafo alitembelea ujenzi wa Hospitali ya Uhuru inayojengwaWilaya ya Chamwino mkoani Dodoma na kumuagiza mkandarasi anaesimamia ujenzi huo kuhakikisha anajenga mchana na usiku ili kumaliza ujenzi huo mapema na wananchi waanze kutibiwa.

" Hii Hospitali Mhe Rais alitoa fedha za Uhuru ili zijenge hapa wananchi waweze kupata matibabu. Nafahamu kumekua na mvua kukawa na changamoto lakini tayari mvua zimepungua hivyo ujenzi uendelee usiku Na mchana.

Nimewaelekeza Suma JKT ambao ndio wanasimamia ujenzi huu kufunga taa kubwa hapa ili ujenzi uendelee mchana na usiku lengo tuweze kumaliza mapema na wananchi wetu wafurahie matunda ya serikali yao," Amesema Mhe Jafo.

Ujenzi wa Hospitali ya Uhuru ulianza rasmi Oktoba 26, 2019 na Novemba 22 Mhe Rais Magufuli aliweka jiwe la msingi la ujenzi ambalo Novemba 23 alitoa maelekezo ya kuhamisha ujenzi huo kutoka kitongoji cha Maduma kwenda eneo la Buigiri, Chamwino ambapo sasa ujenzi huo unatarajia kukamilika Mei 25 mwaka huu.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe Selemani Jafo akizungumza na wananchi na wafanyabiashara wa soko la sabasaba lilipo katikati ya Jiji la Dodoma baada ya kufanya ziara kujionea hali ilivyo kufuatia mvua zinazoendelea nchini.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Selemani Jafo akitoa maelekezo kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge (kushoto) alipofika kukagua maendeleo ya ujenzi wa Hospitali ya Uhuru.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Selemani Jafo akiwa ameambatana na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mkuu wa Wilaya ya Chamwino wamefika katika eneo inapojengwa Hospitali ya Uhuru kujionea maendeleo ya ujenzi wake.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Selemani Jafo akizungumza na mmoja wa wafanyabiashara waliopo ndani ya soko la Sabasaba.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Selemani Jafo akipita ndani ya soko la Sabasaba lililopo katikati ya Jiji la Dodoma kujionea hali ilivyo kufuatia mvua zinazoendelea kunyeesha maeneo mbalimbali nchini.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe Selemani Jafo (kulia) akitoa maelekezo kwa viongozi wa Mkoa wa Dodoma na Jiji hilo baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika soko la Sabasaba.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe Selemani Jafo akizungumza na viongozi wa Mkoa na Wilaya ya Chamwino alipofika katika ujenzi wa Hospitali ya Uhuru kujionea maendeleo yake.
 
 


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/3aI9auE
via
logoblog

Thanks for reading JAFO AKERWA NA MAZINGIRA YA SOKO LA SABASABA, ALIAGIZA JIJI LA DODOMA KUANZA UJENZI WAKE MARA MOJA

Previous
« Prev Post