DKT. NDUMBARO AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA MWAKILISHI MKAZI WA SHIRIKA LA KIMATAIFA LA MSALABA MWEKUNDU

  Masama Blog      

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi Mkazi (Head of Regional Delegation) wa Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu (International Committee of the Red Cross – ICRC) katika Nchi za Tanzania,Kenya na Djibouti Bw. Olivier Dubois.

Mazungumzo hayo yamefanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Jijini Dar es Salaam,ambapo Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) amesema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua na kuthamini mchango wa ICRC katika utoaji wa huduma na misaada ya kibinadamu hapa nchini hasa katika kambi za wakimbizi zilizopo hapa Nchini.

Amesisitiza kuwa Tanzania ikiwa ni mwanachama hai wa ICRC itaendelea kutimiza wajibu wake wa Kitaifa na Kimataifa na kwa kuzingatia Sheria za kimataifa zilizopo chini ya ICRC,sheria za Tanzania na mkataba wa uenyeji (Head Quarter Agreement) kati ya Tanzania na ICRC uliosainiwa mwaka 2001.

Kwa upande wake Bw. Dubois ameishukuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuishirikisha ICRC katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali hususani ile inayohusu utoaji wa misaada ya kibinadamu (Humanitarian assistance) kwa kushirikiana na Chama cha Msalaba Mwekundu – Tanzania (Tanzania Red Cross Society – TRCS).

Ameongeza kuwa ICRC itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wadau wengine katika utoaji wa huduma kwa wakimbizi walioko hapa nchini,wafungwa/mahabusu waliopo magerezani,mafunzo kwa vyombo vya ulinzi na usalama hususani wakati wa ulinzi wa amani (Training on International Humanitarian Law during peace keeping mission).

Bw. Dubois ameambatana na Bi. Andrea Heath mwakilishi Mkaazi wa ICRC – Tanzania. 

from MICHUZI BLOG https://ift.tt/36QApRk
via
logoblog

Thanks for reading DKT. NDUMBARO AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA MWAKILISHI MKAZI WA SHIRIKA LA KIMATAIFA LA MSALABA MWEKUNDU

Previous
« Prev Post